Wednesday, November 8, 2017

TEMBO WAHARIBU MAZAO KIWANGWA/MKANGE.



Diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga,akitoa taarifa ya kata kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Chalinze .(picha na Mwamvua Mwinyi)
...........................................

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze.

WIMBI la tembo limeibuka na kuharibu mazao ya wakulima wa baadhi ya vijiji vya kata ya Kiwangwa ,Mkange na Kibindu vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Saadan na vilivyo karibu na Mto Wami .

Aidha watu watatu wanadaiwa kuuawa kutokana na wanyamapori wakiwemo tembo na fisi.

Kati ya watu hao wawili wamefariki baada ya kujeruhiwa na fisi katika kijiji cha Kiwangwa na mtu mwingine alikufa kutokana na kujeruhiwa na tembo huko kwa Kwamduma.

Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha madiwani cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ngazi ya kata kipindi cha robo mwaka ,diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga ,alisema tembo wamekuwa tatizo na kutishia maisha ya watu .

Alieleza mazao yaliyoliwa zaidi ni matikitimaji ,mapapayi,mahindi,migomba na nyanya.

Kwaga alisema ,zipo hatua alizozichukua ambazo ni kupeleka taarifa halmashauri na wilaya idara ya ardhi maliasili na utalii.
“Idara husika ilisema ipo sheria ya kulipa kifuta jasho walioathiriwa ama kuuawa na wanyamapori “
“Kwa upande wangu kauli hii hainifurahishi na haina mashiko kwani wakulima wameshapata hasara lakini badala ya kulipwa fidia wanaambiwa wanalipwa kifuta jasho” alieleza Kwaga.

Kwaga alisema pia hifadhi ya Taifa -TANAPA na baadhi ya viongozi wa halmashauri walikwenda kuzungumza na wananchi juu ya tatizo hilo na kutoa elimu .

Alisema kwasasa wakulima walioliwa mazao yao wameshaorodheshwa majina yao na watakwenda kufanyiwa uhakiki kwa ajili ya kulipwa fedha hizo .

Nae mkuu wa idara ya ardhi na maliasili katika halmashauri ya Chalinze ,Zaina Kijazi alikiri kuwepo kwa tatizo la wanyamapori tembo na kiboko kula mazao ya wakulima.

Alisema tembo wameharibu mazao hekari zaidi ya 200 ,kifo cha mtu mmoja kilichosababishwa na tembo na  vifo viwili vilivyotoka na fisi.

Zaina alisema tembo wanangia kwenye maeneo ya wakulima ni kutokana na kukariri njia ya mapito yao kutoka Saadan wakielekea Wamimbiki na Mikumi .
Tembo ni wanyama wanaopenda kula maboga,miwa na matikitimaji hivyo ni changamoto kwani ndio mazao yanayolimwa zaidi na wakulima hao.

Kwa upande wake mkulima wa kijiji cha Matipwili Deus Mabirika alieleza ,mazao yake yameharibiwa katika hekari moja ambapo miche ya mipapayi 294 aliyoinunua kila mche 5,000 imeharibiwa yenye gharama ya mil.1.470.

Alisema kati ya hasara aliyoipata ameambiwa atapatiwa kifuta jasho 50,000 kiasi ambacho ni kidogo .

Mabirika aliiomba wizara ya maliasili kuangalia suala hilo kwani fedha hizo ni ndogo hazikidhi mahitaji.


Baadhi ya madiwani,watendaji na wakuu Wa Idara katika Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani ,wakisikiliza taarifa kutoka kwa diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga, wa pili kulia ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya  Chalinze, Zaina Kijazi. (picha na Mwamvua Mwinyi)

VIJIJI VYOTE KUPATA UMEME IFIKAPO 2020/21.



Serikali imesema itahakikisha vijiji vyote visivyo na umeme vinapata umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme vijijini awamu ya Tatu (REA-III) unaotegemewa kukamilika mwaka 2020/21.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea Hassan Masala juu ya mpango wa Serikali katika kusambaza umeme katika kata zilizobaki wilayani Nachingwea kupitia REA III.
“Mradi wa REA III utajumuisha vipengele vitatu vya Densification, Grid Extension na Off grid renewable ambapo Mkoa wa Lindi chini ya miradi ya uendelezaji wa grid (Grid extension) katika Mzunguko wa kwanza unatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na Kampuni ya Stategrig & Technical Works Ltd,” alifafanua Naibu Waziri huyo.

Aliendelea kwa kusema, katika wilaya ya Nachingwea mpango wa Awamu ya Tatu utavipatia umeme vijiji 30 ambapo kazi za utekelezaji wa mradi zilianza Julai mwaka huu na zinatarajiwa kukamilika Juni 30, 2019.

Mgalu amesema, vijiji vilivyobakia vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA III utakaoanza Aprili, 2019 hadi Desemba 2021.

Vile vile amesema, kazi ya kupeleka umeme mzunguko wa kwanza itahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 380, ufungaji wa transfoma 18, ujenzi wa njia za msongo wa kilovoti 0.4 zenye urefu wa kilomita  360 na uunganishaji wa wateja 5,710 katika Mkoa mzima wa Lindi.

Aidha amesema, kwa upande wa Wilaya ya Nachingwea jumla ya wateja 1,200 wataunganishwa, ambapo kwa sasa Mkandarasi anaendelea na upimaji wa njia za umeme na tayari amefikia asilimia 30 na kazi za upimaji zitakamilika mwishoni mwa Novemba 2017.

Saturday, November 4, 2017

ZAO LA KOROSHO LAONGEZEKA BAGAMOYO.

 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga, akikagua godaoni la Korosho lilipo kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo ambapo Godaoni hili mpaka sasa limekusanya Tani 48 kutoka kwa wakulima zikisubiri siku ya mnada.
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga amefanya ziara ya kukagua magodaoni ya korosho wilayani Bagamoyo na kubaini ongezeko la zao la korosho ukilinganisha na mwaka 2017.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka wakulima wa korosho wilayani Bagamoyo kuzikusanya korosho zao kwenye magodaoni yaliyotengwa kwenye kila kata ili ziuzwe kwenye mnada wa serikali.

Aidha, ameonya wale wote watakaouza nje ya mnada kwamba korosho hzo zikikamatwa zitataifishwa na kuwa mali ya sehemu iliyokamata.

Alisema kuuza korosho nje ya mnada kunaipunguzia Halmashauri ruzuku ya upatikanaji wa pembejeo ambazo zinatolewa kulingana na takwimu ya mauzo ya kwenye mnada.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kuhakikisha hakuna walanguzi wanaokuja kununua korosho nje ya mnada ili kuiongezea korosho thamani na hataimae mkulima afaidike na kile alichokivuna.

Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Saidi Zikatimu aliwataka wananchi kuimarisha kilimo cha Korosho kwani ni zao ambalo linaiingizia serikali mapato na kukuza pato la mkulima kulingana na be yake kuwa juu kwa sasa.

Alisema kulingana na thamani ya korosho, Korosho kwa sasa inajulikana kama Dhahabu ya kijani hivyo kila wananchi wanapaswa kupanda miche mipya ya korosho badala ya kutegemea ile iliyopandwa zamani.

alisema agizo la serikali kila kaya inapaswa kupanda miche 30 huku kijiji kikitakiwa kupanda miche  elfu tano.

Kwa upande wao wakulima wa Korosho wilayani Bagamoyo walisema changamoto inyowakabili ni kuchelewa kwa mbolea ambapo mbolea inaletwa wakati tayari maua yameshatoka na hivyo ni vigumu kuwazuia wadudu wanaoshambulia zao hilo la korosho.
  
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga, akikagua godaoni la Korosho la kata ya Kiwangwa, kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chainze, Saidi Zikatimu wa  pili kushoto ni Diwani wa kata ya Kiwangwa, Malota husein Kwaga, mpaka sasa tani tisa zimekusanywa kijiji cha Kiwangwa.

 

Maafisa Kilimo, Ushirika, wa Halmashauri ya Chainze, wakijadili jambo wakati wa zoezi la kukagua magodaoni ya Korosho.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chainze, Saidi Zikatimu akizungumza na wakulima wa Korosho katika kijiji cha visezi kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze wialayani Bagamoyo.