Saturday, November 12, 2016

DC. NYAMAGANA ATOA SIKU SABA UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA WASANII WA FILAMU.

Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji mkoani Mwanza, Ramadhan Mustapha (kushoto), akipokea cheti cha ushiriki kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha, aliyemwakilishwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye ufungaji wa mafunzo kwa wasanii wa filamu mkoani Mwanza hii leo.
.................................
 
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,Mary Tesha, amemtaka Afisa Utamaduni mkoani mkoani hapa, kuhakikisha maadhimio yaliyoafikiwa na wasanii wa filamu mkoa wa Mwanza yanaanza hatua za utekelezaji ndani ya siku saba.

Nje ya hotuba ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, Tesha amesema Afisa Utamaduni mkoa wa Mwanza, James Willium, kwa kushirikiana na maafisa utamaduni wa halmashauri zote za mkoa wa Mwanza wanapaswa kuhakikisha wanatoa mikakati ya utekelezaji wa maadhimio yaliyotolewa kwenye mafunzo hayo ili utekelezaji huo uanze mara moja.

Miongoni mwa maadhimio saba ya wasanii walioshiriki mafunzo hayo ambayo yamewasilishwa na Mwakilishi kutoka Chama cha Waongozaji wa Filamu mkoani Mwanza, Mwanaharusi Hela, ni pamoja na uongozi (Serikali) wa mkoa wa Mwanza kusaidia upatikanaji wa kituo cha sanaa (studio ya kisasa) kwa ajili ya kurekodia filamu na vipindi vya runinga pamoja na kushirikishwa kwenye dhifa mbalimbali za kimkoa na kitaifa ili kuonesha kazi sanaa zao.

Katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Sanaa Asilia, Mzee Fumbuki Lubasa, ametoa bure kiwanja chenye ukubwa wa hekta 50 kwa 40 kilichopo Nyegezi Jijini Mwanza ili wasanii wa filamu mkoani Mwanza wajengewe studio kwa ajili ya kurekodia kazi zao ambapo Mfuko wa Pensheni wa PPF umeonesha nia ya dhati ya kufadhiri ujenzi wake.

Zaidi ya washiriki 300 wamepata mafunzo hayo ambapo Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Joyce Fesso, amesema yamelenga kuwajengea weledi wadau wa filamu wakiwemo waigizaji, waongozaji na wahariri, kutengeneza kazi zenye ubora, kutambua majukumu ya bodi hiyo, hakimili na hakishirikishi ili kukuza soko la filamu na hivyo kunufaika na kazi zao.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mary Tesha (kushoto), akipokea cheti cha utambuzi kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Joyce Fesso (kulia), wakati wa ufungaji wa Mafunzo kwa Wasanii wa Filamu mkoani Mwanza yaliyoanza juzi Novemba 10 na kutamatika leo Novemba 12,2016 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.Tesha amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella.
 
Meneja Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA, Innocent Mungy (kushoto), akipokea cheti cha utambuzi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha, aliyemwakilishwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye ufungaji wa mafunzo kwa wasanii wa filamu mkoani Mwanza hii leo.
 
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifwamba (kushoto), akipokea cheti cha utambuzi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha, aliyemwakilishwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye ufungaji wa mafunzo kwa wasanii wa filamu mkoani Mwanza hii leo.
 
Mwakilishi kutoka Chama cha Waongozaji wa Filamu mkoani Mwanza, Mwanaharusi Hela (kushoto), akipokea cheti cha ushiriki wa mafunzo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha.
 
Mshauri wa sanaa ya Filamu mkoani Mwanza ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Sanaa Asilia, Mzee Fumbuki Lubasa (kushoto), akipokea cheti cha utambuzi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha.
 
Washiriki wa mafunzo ya filamu mkoani Mwanza wakifuatilia burudani kutoka kwa msanii wa nyimbo za asili, Chifu Mwananzengo kutoka wilayani Kwimba hii leo.
 
Washiriki wa mafunzo ya filamu mkoani Mwanza, wakifuatilia mada kwenye mafunzo hayo hii leo kabla ya mafunzo hayo kufungwa.
 
Washiriki wa mafunzo ya filamu mkoani Mwanza, wakifuatilia mada kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Joyce Fesso.
  
Washiriki wakiwa katika Picha ya pamoja

Wednesday, November 9, 2016

HOSPITALI YA TUMBI YAANZA KUZALISHA DRIP YENYEWE NA KUONDOA ADHA YA KUNUNUA SEHEMU NYINGINE.

tum
KAIMU mganga mkuu wa hospitali ya rufaa ya Tumbi ,mkoani Pwani, Dkt. Bryceson Kiwelu,akionyesha chupa ya drip ambazo wanazalisha katika kitengo cha hospitali  hiyo ambapo kwasasa wanaondokana na adha ya kununua drip nje ya hospital kwa asilimia 98 sasa.(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
 tubi

Na Mwamvua Mwinyi-Kibaha

HOSPITALI ya rufaa ya Tumbi mkoani Pwani,imeanza kuzalisha drip zake kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hali inayosababisha kuondokana na adha ya kununua drip nje ya hospitali hiyo kwa asilimia 98.

Aidha hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa kipimo cha CT Scan na kupelekea wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa kipimo hicho kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akizungumza kuhusiana na mafanikio na changamoto zinazozikabili hospitali hiyo ,kaimu mganga mkuu wa hospitali ya rufaa ya Tumbi,Bryceson Kiwelu,alisema kwasasa Tumbi ina kitengo cha kuzalisha drip yenyewe.

Alieleza kwamba drip hizo wanatengeneza katika ujazo wa mill’s 250 hadi 500 lakini wanatarajia kuzalisha katika ubora wa chupa za vioo ili waweze kuuza katika hospitali na vituo vya afya vingine kwa lengo la kujipatia kipato.

“Kuna wauguzi zaidi ya watatu ambao wana vyeti vinavyoruhusiwa kutengeneza drip hizo,ndio wataalamu kwenye kitengo hiki lakini lengo letu ni kupeleka wengine wawili masomoni ili wasomee utaalamu huu”alifafanua Dkt. Kiwelu.

Mafanikio mengine ni pamoja na hospitali kupata mtambo wa hewa ya oxygen,uliogharimu sh.mil.184 ambao unasaidia kuhudumia wagonjwa 75 kwa wakati mmoja ikiwemo wa ajali za barabarani.

Dk.Kiwelu alisema ipo changamoto ya kipimo cha CT Scan, endapo kingekuwepo kingesaidia kwa kiasi kikubwa hasa wahanga wa ajali za barabarani kwani Tumbi huhudumia wagonjwa hao kwa asilimia 8 ambao wengi wao huumia vichwa.

Nae mkurugenzi wa shirika la elimu Kibaha, Dk. Cyprian Mpemba alisema mafanikio hayo, yametokana na ubunifu wao kwa kuandika maandiko kwa wafadhili na ushirikiano.

Alisema pia wameweka mtambo mpya wa kisasa wa kufulia nguo za wagonjwa uliogharimu mil .119.

“Mtambo huo wa kufulia nguo unasaidia hospitali nyingine ikiwemo Bagamoyo na vituo vya afya kupeleka mashuka kufuliwa”alisema dk. Mpemba.

Dk.Mpemba alifafanua kwamba pia kumejengwa na maabara katika shule ya sekondari ya wasichana ambapo imeshakamilika kwa asilimia 75.

Alieleza licha ya hayo yote bado wanakabiliwa na ufinyu wa bajeti.

Dk.Mpemba alisema bajeti iliyoidhinishwa 2016/2017 katika 
mishahara,matumizi na miradi ya maendeleo ni zaidi ya sh.bil 19.324 ambapo mapato halisi ya Julai/Septemba 2016 ni sh.bil 3.210 pekee sawa na asilimia 16.6.