Wednesday, November 9, 2016

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

lic1
Katibu Msaidizi  toka Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Peleleja  Masesa akiwaeleza waandishi wa Habari(hawapo pichani) leo Jijini Dar es salaam kuhusu mikakati ya Serikali kuhakikisha kuwa watumishi wa Umma wanazingatia maadili ya Utumishi wa Umma ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
........................................


Serikali imewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma ili kuleta ustawi kwa wananchi kwa kutekeleza mipango  inayolenga kukuza uchumi na kutoa huduma bora.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Katibu Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Peleleja Masesa wakati wa mkutano na vyombo vya Habari.

Bw. Masesa amesema kuwa Matokeo ya Makosa ya watumishi wa Umma waliokata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma mwaka 2014/2015 yanaonyesha kuwa kati ya watumishi 135 walikata rufaa walipatikana na makosambalimbali ambapo 54 walipatikana na kosa la utoro kazini.

Bw. Masesa aliongeza kuwa watumishi wengine 16 walishindwa kutekeleza majukumu yao,10 kumdharau mwajiri,8 kughushi nyaraka mbalimbali,8 kufanya malipo kinyume na taratibu,aidha makosa mengine yalikuwa chini ya watumishi 7.

Aidha Masesa aliwataka watumishi wa Umma kujiepusha na vitendo vya rushwa,ulevi,utoro makazini na matendo yote yanayokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

“ Utendaji kazi katika utumishi wa Umma huongozwa na sheria,kanuni,taratibu na Miongozo mbalimbali ambayo ipo”Alisisitiza Masesa.

Pia  Masesa amesema kuwa watumishi watakaoshindwa kuzingatia taratibu zilizowekwa watachukuliwa hatua kali za kisheria na mamlaka za nidhamu katika taasisi husika.

Tume ya Utumishi wa Umma,inawataka waajiri,Mamlaka za ajira na nidhamu na Watumishi wote kuzingatia kanuni za maadili wakati wote wanapotekeleza majukumu yao ili kukuza uchumi,kutoa huduma bora kwa jamii na kulinda amani na utulivu wan chi.lic2

Katibu Msaidizi  toka Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Celina Maongezi akisisistiza jambo kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na vyombo vya habari. Kulia ni Katibu msaidizi wa Tume hiyo Bw. Peleleja Masele,kushoto ni Afisa Habari na Mawasiliano wa Tume hiyo Bi Jorlin Kagaruki.
 lic3

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma uliofanyika leo Jijini Dar es salaam.



KIFO CHA JOSEPH MUNGAI RAIS DKT. MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Tuesday, November 8, 2016

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWA WAWEKEZAJI

mr14 
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambapo alimpongeza muwekezaji wa kiwanda hicho na kutoa rai kwa wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya viwanda kama ilivyo katika mkoa wa Pwani.
  ..........................................................


Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini wametakiwa kuweka kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda nchini.

Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema kuwa tukiwa tunaelekea katika nchi ya viwanda serikali inajukumu la kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji nchini.

Dkt. Adelhelm amesema kuwa viongozi hao hawana budi kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika mkoa huo.

“Dhumuni la serikali kwa sasa ni kuhakikisha tunaifikia nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda,na hili tutalitekeleza pia kwa kushirikiana na sekta binafsi na ni jukumu la viongozi ikiwemo wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa nchini kote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda”. Alisema Dkt. Adelhelm

Dkt. Adelhelm aliongeza kuwa mpaka ifikapo mwaka 2020 Serikali imepanga kuhakikisha sekta ya viwanda nchini inachangia asilimia 15 kwenye pato la taifa kutoka asilimia 7.3 iliyopo hivi sasa.

Pia Dkt. Adelhelm alisema kuwa Serikali imepanga kuongeza idadi ya ajira za viwandani na ajira zitokanazo na sekta ya viwanda hadi kufikia asilimia 40 ifikapo mwaka 2020.

Naye Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) Bw. Mlingi Mkucha amesema kuwa shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza katika viwanda ikiwemo kupitia maandiko ya miradi yao na kuwasimamia ili kuhakikisha kwa pamoja wanatimiza lengo la serikali ya awamu ya tano ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

Bw. Mkucha aliongeza kuwa katika wilaya ya Kibaha kuna hekari 330 zilizotengwa kwa ajili ya viwanda vya aina mbalimbali ikiwamo viwanda vya kuunganisha magari, vuwanda vya madawa na viwanda vya nguo hivyo kama kuna muwekezaji mwenye nia ya kuwekeza katika sekta hizo aende katika ofisi za Shirika hilo ili kuweza kujadili namna ya kutekeleza suala hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho katika mkoa wa pwani ni mwendelezo wa jitihada za kumuunga mkono Rais Magufuli ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Bw. Joseph Wasonga alishukuru jitihada za serikali na taasisi zake kwa ushirikiano wanaoupata tangu wakiwa na wazo la kuanzisha kiwanda hicho hadi kufikia hatua hiyo ya uzinduzi.

Bw. Wasonga aliongeza kuwa dhumuni la kiwanda hicho ni kuzalisha vifungashio milioni 16 hadi milioni 20 kwa mwaka na kuongeza zaidi idadi ya ajira kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka kiwanda hicho na maeneo ya jirani.

Kiwanda cha hicho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) na kampuni ya Wande Printing and Packaging inayomilikiwa na mzawa.
mr12

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na kumshukuru muwekezaji wa kiwanda hicho kwa kuamua kuwekeza katika mkoa wa pwani kwani itaisaidia kuongeza mapato katika mkoa na kuongeza ajira kwa wakazi.mr16mr17

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru (katikati mwenye miwani), Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda cha vifungashio Bw. Joseph Wasonga (wanne kutoka kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kiwanda hicho na wafanyakazi wa NDC.