Monday, October 10, 2016

LHRC YAFUNGUA KESI DHIDI YA SERIKALI KUPINGA ADHABU YA KIFO

1
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo- Bisimba (katikati), Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio (kulia) na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga , wakionesha jarida la kupinga adhabu ya kifo wakati wa uzindi wake Dar es Salaam leo.
 

Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio (kulia), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo, kusho ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo- Bisimba.
 

Wanahabari wakifuatilia mkutano huo.
..............................


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimefungua kesi ya kikatiba kuhusiana na ulinzi wa haki ya kuishi na urekebishwaji wa sheria ya kanuni ya adhabu juu ya ulazima wa kutolewa kwa adhabu ya kifo katika makosa ya uhaini na mauaji.

Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali  wakitaka ufafanuzi zaidi juu ya adhabu ya kifo, wakibainisha kuwa adhabu hiyo haimpi nafasi mtuhumiwa kujirekebisha bali ni ya kulipiza kisasi.

Kituo hicho kimesema endapo Tanzania itatekeleza hukumu ya kifo  kwa sasa inamaanisha watu wapatao 228 na zaidi watapoteza maisha yao huku  wengine 244 wanasubiria maamuzi ya rufaa zao.

Akizungumza wakati akitoa tamko la kupinga adhabu ya kifo  Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen- Kijo Bisimba alisema hadi  mwaka 2015 jumla ya watu 472 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa.

Alisema kituo kinaiomba serikali kurekebisha sheria ya kanuni ya adhabu na sheria ya ugaidi yenye kutoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi.

Dk. Bisimba alisema kituo  kina sababu za kupinga adhabu hiyo ya kifo na  hawafurahii watu kuua wengine na ndio maana hawapendi pia hata muuaji auawe.

“Adhabu ya kifo ni vigumu kuhakikisha kuwainatekelezwa tu  kwa wale watu ambao huwezi kuirekebisha kwani mfumo wa utoaji haki huwa pia na mianya ya makosa na hivyo maisha ya mtu yanaweza kupotea bure,” alisema Dk. Bisimba na kuongeza kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa adhabu hiyo inaweza kuzuia watu wengine kutokutenda makosa  kama hayo.

Alisema licha ya adhabu  hiyo kutokutekelezwa nchini kwa takriban miaka 22 , taaarifa zinaonesha kuwa watu 72 ambao walishawahi kunyongwa kutokana na adhabu hiyo.

Hata hivyo aliiomba serikali kutengeneza utaratibu wa kuelimisha jamii juu ya kuheshimu haki za binadamu hususani haki zakuishi na kuweka mazingira ya kuiheshimu haki hiyo, pia ibadilishe sheria  kwa kuondoa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala kwenye makosa ya jinai na kwa wafungwa waliopo mfano vya muda mrefu  gerezani.




TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGONJWA WA SARATANI KULIPISHWA FEDHA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

capture
 Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili unapenda kuutarifu Umma kwamba haijamzuia Bi. Mwajuma Ramadhani Kimweri kutoka hospitalini kwa madai ya kushindwa kulipa pesa za matibabu kama ilivyoandikwa na Gazeti la Jambo Leo lenye namba ISSN 7826 No 2589, hivyo taarifa hizo si za kweli.

Katika ukurasa wa mbele, gazeti hilo limechapisha taarifa yenye kichwa cha habari kinachosema “Mgonjwa saratani azuiwa Muhimbili miezi miwili ni baada ya kushindwa kulipa deni la Sh. 330,000”.

Bi. Mwajuma Ramadhani Kimweri kwa mara ya kwanza alilazwa Muhimbili Agosti 29, 2016  akitokea mkoani Morogoro na kuruhusiwa Septemba 10, 2016  na  Septemba 23, 2016  alilazwa tena na kuruhusiwa Septemba 24, 2016.

Baada ya vipimo vya awali kufanyika Septemba 29, 2016 alilazwa tena na kufanyiwa  upasuaji Septemba 30, 2016 na kuruhusiwa Oktoba 04, 2016 baada ya taratibu za matibabu kukamilika.

 Mgonjwa  aliingizwa kwenye utaratibu wa msamaha na kuchangia Shilingi 70,000 tu, kati  ya Shilingi 400,142.33. Hivyo si kweli kwamba mgonjwa alilipa Shilinngi 380,000 kama ilivyoandikwa na gazeti hilo.

Kuhusu tiba ya mionzi, Bi. Mwajuma Ramadhani Kimweri amefanyiwa vipimo vingine hivyo atatakiwa kurejea baada ya wiki tatu kwa ajili ya majibu na si kweli kwamba Muhimbili imezuia uhamisho wake kwenda Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa ajili ya tiba hiyo.

Imetolewa na;
Uongozi wa  Hospitali ya Taifa Muhimbili
Oktoba  10, 2016.