Friday, August 12, 2016

WAZIRI JAFO, AWATAKA WAKUU WA IDARA KUTEMBELEA VIJIJINI.



Jafo akizungumza na wananchi na watumishi katika mradi wa maji kijijin cha Tinde Mkoani Shinyanga.
 

Naibu Waziri Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na usalama wa Wilaya ya Shinyanga.


..........................................................................................


NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amewataka wakuu wa idara kwenye Halmashauri nchini kuacha kufanya kazi kimazoea kwa kuishia kukaa maofisini bila kwenda maeneo ya vijijini ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Jafo ametoa kauli hiyo ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi katika Halmashauri za Singida, Shinyanga, Uyui na Sikonge mkoani Tabora. Akizungumza na watumishi katika halmashauri hizo, Jafo amesema imekuwa ni mazoea kwa wakuu wa idara kujifungia maofisini bila kufika vijijini kukutana na wananchi ili waweze kutatua kero zao.

Hata hivyo amewaonya baadhi ya wakuu wa idara wanaowanyanyasa watumishi wa kada za chini kwa kuwapendelea baadhi yao katika mchakato wa upandishaji wa madaraja. Amewaagiza wakurugenzi kupangiana malengo na wakuu wa idara kuwa ni kitu gani kila mmoja wao atakifanya ndani ya mwaka mmoja kwenye eneo lake la kazi.

Aidha amesema na wakuu wa idara wafanye hivyo hivyo kwa watu wao wa chini ili kila mtu apimwe kiutendaji ndani ya mwaka mmoja. Jafo amekemea tabia ya wakurugenzi wa Halmashauri kupitisha malipo ya miradi ambayo inakuwa imejengwa chini ya kiwango na kwamba ni ubadhirifu wa fedha za wananchi kwa kuwa haifikii malengo yaliyokusudiwa.

“Hali kama hii imejitokeza kule halmashauri ya kondoa mkoani Dodoma serikali imefanya uchunguzi na tayari hatua zimechukuliwa kwa watendaji 8 ambao wamesimamishwa kazi na wengine kufikishwa mahakamani kutokana na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo…Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa yeyote atakayefanya vitendo kama hivi,”amesema Jafo

Naibu Waziri huyo kwa takriban wiki mbili amefanikiwa kutembelea halmashauri 15 na kutembelea miradi 63 ikiwemo miradi ya hospitali, vituo cha afya na zahanati, miradi ya elimu, maji, na miundombinu ya barabara.

Miongoni mwa Halmashauri alizozitembelea ni pamoja na Halmashauri ya Kilolo, Mufindi, Mafinga, Iringa, Chemba, Kibaha, Korogwe mji, Halmashauri ya Korogwe, Jiji Arusha, Kisarawe, Singida, Manispaa ya Shinyanga, Halmashauri ya Shinyanga, Uyui, na Sikonge .

Waziri Jafo bado anaendelea na ziara yake katika mikoa ya Katavi na Rukwa kwa lengo kutimiza matakwa ya watanzania. 



MZEE YUSUF AACHANA NA MUZIKI, AVITAKA VITUO VYOTE VYA TELEVISHENI NA REDIO KUACHA KUPIGA NYIMBO ZAKE



Aliyekuwa Mfalme na gwiji wa muziki wa taarabu Afrika mashariki MZEE YUSUF ameamua kuachana na mziki na kumrudia Allah
 ..............................................................................


Mzee Yusuf aliyekuwa mwimbaji wa muziki taarabu leo ijumaa tarehe 12-08-2016 ametangaza kuachana na muziki Muda mfupi baada ya kumaliza kuswali swala ya ijumaa ktk msikiti wa ilala bungoni (Masjid Taqwa)

Alizungumza huku akibubujikwa na machozi mengi Mzee Yusuf amemuomba Allah amsamehe madhambi yake yote pamoja na kuwaomba waumini wote wamuombee msamaha kwa Allah. Kadhalika amewaomba wanamuziki wengine ambao ni waislamu kuachana na muziki na kuzitumia fani zao walizonazo ktk kutangaza na kusifia tabia za bwana mtume muhammad (s.a.w).

Gwiji huyo wa zamani wa taarabu amewaomba watu wote waliokuwa na Cd zake majumbani mwao kuacha kupiga nyimbo zake na wakikaidi wafahamu madhambi yote yatakuwa juu yao kwani yeye hivi sasa anafanya toba kwa Allah.

Pia amevitaka vituo vyote vya televisheni na redio kuacha kupiga nyimbo zake kwani yeye Hana dhimma hiyo Tena. Ikumbukwe hali kama hii ilishawahi kutokea kwa aliyekuwa msanii wa bongo fleva SUMA LEE kuamua kuachana na mziki na sasa ni mpenzi mkubwa wa mtume muhammad (s.a.w)

Yaa rabbi awape tawfiiq wanamuziki wote wa kiislamu waachane na muziki pamoja kutupa mwisho mwema wao pamoja nasi in shaa Allah.

Hakuweza kuendelea kuongea zaidi ya maneno hayo na kuangua kilio kilichomsababishia maneno kutoweza kutoka mdomoni mwake.



Thursday, August 11, 2016

RAIS MAGUFULI AAGIZA MALI ZA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA CHA NYANZA ZIRUDISHWE




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Ushirika cha Nyanza ambazo zilinunuliwa na kutwaliwa na watu binafsi kwa njia za ujanja ujanja.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Dkt. Magufuli amesema Serikali yake haipo tayari kuwafumbia macho watu wachache waliovifilisi vyama vya ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha mali za ushirika yakiwemo majengo, viwanda na mashamba na ametaka mali hizo zirudishwe mikononi mwa wananchi.

"Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe kwa umma" Amesema Rais Magufuli.

Katika Mkutano huo Rais Magufuli pia amesema Serikali itafanya oparesheni kubwa ya kuteketeza Makokoro katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji wa minofu ya samaki katika viwanda.

Amebainisha kuwa lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo la Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya kusindika minofu ya samaki lifanikiwe.

Kabla ya kuhutubia mkutano huo Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu la Furahisha linalokatiza barabara ya Uwanja wa Ndege kwenda katikati ya Jiji la Mwanza.

Daraja hilo litakuwa na urefu wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta 5.5 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.455

Akizungumzia ujenzi huo Rais Magufuli amemtaka Mkandalasi anayejenga Daraja la Furahisha kukamilisha kazi hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na pia ameagiza Mkandalasi aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuendelea na kazi hiyo ndani ya wiki moja kwa kuwa Serikali imejipanga kumlipa fedha za kazi hiyo.

Pia Dkt. Magufuli ameahidi kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Katikati ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili barabara hiyo ifike hadi uwanjani badala ya kuishia eneo la Pasiansi.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
11 Agosti, 2016

WIZARA YA AFYA YATOA TAMKO.