Thursday, July 14, 2016

JK. AFUNGUA MKUTANO WA TATU WA MABADILIKO YA TABIA NCHI JIJINI DAR ES SALAAM.



Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akifungua mkutano wa tatu wa Sera za Mabadiliko ya Tabia Nchi jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Climate Strategies. Mkutano huo ilijumuisha watafiti na watunga sera 80 kutoka nchi zaidi ya 10 nje na ndani ya Afrika chini ya kauli mbiu "Kutekeleza Makubaliano ya Paris - Suluhu Mpya za Utafiti kwa ajili ya Nchi zinazoendelea." Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa mkutano huo Bw. Chuks Okereke, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano Mhe. January Makamba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja. 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano Mhe. January Makamba akizungumza katika mkutano wa tatu wa Sera za Mabadiliko ya Tabia nchi unaoendelea jijini Dar es Salaam. Waziri Makamba amesema kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi 175 zilikubali na kutia saini Makubaliano ya Paris Aprili 22 mwaka katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York ili kuweza kupunguza na kudhibiti utoaji wa gesi ya kaboni duniani. 
 

Mwenyekiti wa Mkutano wa Sera za Mabadiliko ya Tabia Nchi Bw. Chuks Okereke kutoka Chuo Kikuu cha Reading, Uingereza akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo. Mkutano huu ni wa tatu kufanyika duniani na wa kwanza kufanyika barani Afrika baada ya London, Uingereza 2014 na New Delhi, India 2015.

WAZIRI MKUU ASEMA ATAKAEKWAMISHA UPATIKANAJI WA VIWANDA NCHINI ATASHUGHULIKIWA.

 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Goodwill Ceramic, Frank Yang (aliyeshika kipaza sauti) wakati akiangalia ramani ya kiwanda hicho katika kijiji cha Mkiu Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdalah Ulega 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mfano wa hundi ya Shilingi milioni 20, kutoka kwa Balozi wa China Nchini, Dkt. Lu Youqing (wa pili kulia) kusaidia ununuzi wa madawati katika Shule zilizopo katika wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, Kulia ni Mbunge wa Jimbo hilo, Abdallah Ulega na Kushoto ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. 




WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa viwanda unaotekelezwa kwa kasi hapa nchini utakuwa ndio mwarobaini wa kuondoa tatizo la ajira kwa vijana kwa wingi hapa nakudai kuwa atakayekwamisha mkakati huo wa Serikali hatovumiliwa.

Pia amesema kuwa maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Viwanda hivyo na yale ambayo tayari ujenzi wa viwanda umeshaaza lazima miundombinu ya umeme wa uhakika upatikane ili kuwezesha viwanda hivyo kuzalisha kwa wingi.

Majaliwa aliyasema hayo juzi Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ikiwa sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya kikazi,ambapo alitembelea utekelezaji wa Ujenzi wa Kiwanda cha Vigae cha Googwill,ambacho kinajengwa katika kijiji cha Kiu,kilichopo Kata ya Nyamato tarafa ya Mkamba wilayani humo.

WIZARA YA AFYA YAKANUSHA UVUMI.

 
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO   

         
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na Uvumi katika Mitandao ya Kijamii kuwa Serikali imeamua kushusha Mishahara ya Madaktari kwa asilimia 30% ili kuendana na dhana ya Hapa kazi tu na kuwa Serikali   imekusudia kufuta malipo ya Posho za Wataalamu wa Afya walio katika Mafunzo kwa Vitendo ufafanuzi kwa Umma wa Watanzania na Watumishi wa Sekta ya Afya kuwa taarifa hizo siyo za kweli.

Taarifa aliyoitoa Katibu Mkuu (Afya) alipokuwa anaongea na Watumishi wa  Hospitali ya Bugando  ililenga kutoa ufafanuzi kwa Watumishi wa Hospitali hiyo kuhusu kufutwa kwa kibali cha Msajili wa Hazina kilichowawezesha  watumishi wa Hospitali hiyo kulipwa Mishahara ya Taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina tangu mwaka 2012.

Uamuzi huo wa Msajili wa Hazina unatokana na ukweli kwamba Hospitali ya Bugando siyo Shirika la Umma na hivyo wanastahili kulipwa mishahara sawa na watumishi wengine wa Serikali Kuu kwa kuzingatia makubaliano yaliyopo kati ya Serikali na Baraza  la Maaskofu Tanzania  (TEC) ambao ndio wamiliki wa Hospitali ya Bugando.

Aidha, ieleweke kuwa mishahara ya Watumishi wa Sekta ya Afya haizingatii ngazi ya Vituo vya kutolea huduma kama vile Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali, au Hospitali za Rufaa bali huzingatia uzito wa kazi na majukumu ya kada husika. Hivyo, mshahara wa Daktari wa Hospitali ya Wilaya ni sawa na ule wa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda.

Kutokana na maelezo haya, uamuzi huo wa Msajili wa Hazina utaihusu Hospitali ya Bugando pekee na siyo Hospitali zote za Kanda kwa kuwa dosari hiyo haikutokea katika Hospitali nyingine za Kanda.

Kuhusu ajira mpya kwa mwaka 2015/2016 ufafanuzi ulitolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hakutakuwa na ajira mpya hadi hapo Zoezi la Uhakiki wa Watumishi Serikalini litakapokamilika.  Hivyo, vibali vya ajira vilivyokuwa vimetolewa vimefutwa hadi hapo itakapotamkwa vinginevyo.

Kadhalika, kumekuwa na Uvumi kuwa Serikali inakusudia kufuta posho ya ‘Interns' kuanzia mwaka huu wa fedha.  Taarifa hii pia siyo sahihi kwa kuwa hakuna chombo chochote cha Serikali ambacho kimetoa maamuzi hayo.

Wizara inasisitiza kuwa maamuzi ya Serikali hutolewa na Mamlaka husika  kwa nyaraka. Hivyo, watumishi wa Sekta ya Afya na wananchi kwa ujumla wanaaswa kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka za Serikali kuhusu Masuala yanayowahusu ambayo mara nyingi hutolewa kwa nyaraka badala ya Mitandao ya kijamii,

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Afya
14 Julai, 2016