Tuesday, August 12, 2025

TBN YAKEMEA 'MANABII' WA MITANDAONI, KWA UTABIRI WAO UNAOLETA TAHARUKI KWA JAMII.

 

Mkuu wa Mawasiliano Serikalini, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, (PDPC) Innocent Mungy, akizungumza katika mafunzo hayo.


Na Mwandishi wetu, Dar es salaam.


Mtandao wa Bloga Tanzania (TBN) umekemea vikali tabia inayoshamiri ya watu kujinadi kufanya utabiri kwa watu na taifa kupitia mitandao ya kijamii, ukisema vitendo hivyo vinakiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.


Kauli hiyo imetolewa kama azimio katika kikao kazi cha mafunzo ya mabloga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.


Mabloga hao wameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kushirikiana kuwasaka na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.


Katika kikao hicho, mabloga walibainisha kuwa kumeibuka kundi la watu wanaodai kuwa ni manabii na kutoa kauli zinazokiuka sheria za nchi na kuleta taharuki kuelekea uchaguzi mkuu.


Wakitolea mfano wa kauli hizo ni kama vile kusema kutatokea kifo cha kiongozi mkubwa siku za hivi karibuni, au kutatokea machafuko fulani, na kusema kuwa kauli hizo ni za kuleta taharuki kwa wananchi na kukiuka sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.


Walisisitiza kuwa baada ya kuchambua Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act), walibaini kwamba 'utabiri' wa namna hiyo unavuruga haki ya msingi ya faragha ya wahusika.


Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Mawasiliani Serikalini, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, (PDPC) Innocent Mungy, amesema sheria  inakataza kutoa Taarifa za mtu binafsi bila ya ridhaa yake.


Aliongeza kwa kusema kuwa, katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wapo watu watatoa taarifa za Afya ya mtu kwa lengo la kumharibia ili asichaguliwe jambo ambalo ni kosa kisheria.


Mungy alisisitiza kuwa sheria hiyo ina adhabu kali na lazima ifuatwe na kila mtu, si tu mabloga na waandishi wa habari.


Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na TCRA, yalilenga kuwaandaa mabloga kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi na uadilifu. 


Pamoja na mada ya ulinzi wa taarifa binafsi, mada nyingine muhimu zilizotolewa ni pamoja na Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uchaguzi na Matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika uandishi wa habari.


Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza uwezo wa mabloga kuhakikisha wanafuata sheria na maadili ya uandishi, jambo linalotazamiwa kuchangia mazingira ya uchaguzi yenye amani na utulivu.

Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, akiwasilisha mada katika mafunzo maalumu kuelekea uchaguzi mkuu mahususi kwa bloga yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Agosti 11, 2025 Jijini Dar es Salaam








No comments:

Post a Comment