Thursday, August 14, 2025

MARIAN SCHOOLS MARATHON NI KESHO

 



Na Albert Thomas Kawogo.

TAASISI ya Marian Schools Bagamoyo imeandaa mbio za marathon MARIAN SCHOOLS MARATHON 2025 zitakazofanyika Bagamoyo Ijumaa ya tarehe 15  Agosti.


Msemaji wa Marian Schools, Ohsana Mnalunde amesema mbio hizo zitaanzia kwenye kijiji cha Zinga Samakisamaki na kumalizikia kwenye hoteli ya Stella Maris Bagamoyo mjini.


Mnalunde amesema tayari zaidi ya washiriki 5,000 wamethibitisha ushiriki wao huku idadi kubwa ya watu wa Bagamoyo ikionyesha nia ya kushirki mbio hizo.



Msemaji huyo amesema mgawanyo wa mbio hizo ni wa km 21, km 10 na km 5 ambapo idadi ya washiriki watarajiwa ni wanafunzi, wazazi,  wafanyakazi, walimu na wakuu wa mashrika ya serikali na binafsi pamoja na wafanyakazi wao.


Naye Meneja wa Taasisi za Marian Schools Padre Valentine Bayo amewataka watu wengi kujitokeza kujisajili ili waweze kushiriki kwani kukimbia ni afya na  kunasaidia kupunguza kasi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama shinikizo la damu sukari na moyo ambayo huchangia zaidi ya asilimia 30 ya vifo vyote hapa nchini.


Padre Bayo ambaye pia ni mwanzilishi wa shule za Marian amesema watu wanaingia gharama kubwa kutibu magonjwa yatokanayo na uzito wa kupindukia lakini kama wangejenga utamaduni wa kufanya mazoezi hasa kukimbia wangeepuka magonjwa hayo.


Mbio hizo ambazo kwa mwaka huu zinatimiza miaka mitatu sasa zimedhaminiwa na Benki ya KCB.

No comments:

Post a Comment