Saturday, April 20, 2024

WAJASIRIAMALI WANAWAKE PWANI WATAKIWA KUZINGATIA UBORA WA BIDHAA ZAO.

 

Mwanasheria wa Halmashauri ya Bagamoyo, Hemedi Malogo (katikati) akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Shauri Selenda, katika kufunga mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake wafanyabiashara (TWCC) ambayo yamefanyika wilayani Bagamoyo.


Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa TWCC Bi Mwajuma Hamza, Mwenyekiti wa Bodi ya TWCC Taifa, na kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Tred Mark Afrika (TMA) Bi Ester Utamis, Mwenyekiti wa TWCC mkoa wa Pwani, Bi Stela Gwassa.

...........................................

Na Athumani Shomari

Bagamoyo

Wajasiriamali wanawake Mkoani Pwani  walio chini ya Chama cha Wanawake wafanyabiashara (TWCC) wametakiwa kuzingatia ubora wa bidhaa zao ili kuingia katika ushindani wa soko huru la Afrika (AFCFTA)


Akifunga mafunzo ya siku mbili ya Chama cha Wanawake wafanyabiashara (TWCC) yaliyofanyika wilayani Bagamoyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda amesema bidhaa zenye ubora huongeza thamani na kuweza kukabiliana na ushindani uliopo sokoni.


Katika hutuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mwanasheria wa Halmashauri ya Bagamoyo, Hemedi Malogo, Selenda amesema wajasiriamali wa Mkoa wa Pwani wanaweza kutumia mazao yanayopatikana mkoani humo ili kujiongezea kipato.


Alisema mkoa wa Pwani una bidhaa za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, pamoja na ufugaji ambapo vyote hivyo vikitumiwa vizuri vinaweza kukuza pato la mtu mmoja mmoja, familia na hatimae Taifa kwa ujumla.


Aliendelea kueleza kwa kusema kuwa, swala la uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ni sehemu ya kipaumbele chake.


Alisema kutokana na umuhimu huo, Tanzania imekuwa Mwanachama wa Jumuiya mbalimbali za maendeleo ya kikanada na kimataifa ikiwemo jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumuiya ya  Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na imeridhia utekelezaji Mktaba wa eneo la soko huru la Afrika (AFCFTA) ili kutoa fursa za masoko kwa watanzania.


Selenda alisema, ni matumaini ya Serikali kuona wajasiriamali wanazitumia vizuri fursa hizo ili waweze kunufaika nazo kwakuwa Tanzania inazalisha bidhaa nyingi zenye ubora hivyo wanawake wanatakiwa wawe mstari wa mbele katika kuchangamkia fursa.


Alimalizia kwa kuzitaka Taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zimeshiriki kwenye mafunzo hayo, kushirikiana na wafanyabiashara hao kuhakikisha bidhaa zao zinafuata taratibu na kanuni zote ili ziweze kukua, na kuwa endelevu.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya    Chama cha Wanawake wafanyabiashara Taifa (TWCC) Bi Mercy Emanuel Sila amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wafanyabiashara wanawake kuhusu taratibu, Sheria na kanuni za kufanya Biashara maeneo waliyopo na kwenye soko la Afrika (AFCFTA).


Alisema kupitia TWCC wanawake wanaweza kupiga hatua ya kimaendeleo kwenye biashara zao na kujua njia mbalimbali za kukuza mitaji,  kuboresha biashara na kutafuta masoko.


Alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Sukuhu Hassan kwa kutoa umuhimu juu ya wanawake na kutengea asilimia 10 ili kujiemdeleza kupitia vikundi vyao.


Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamesema wanaishukuru TWCC kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewajengea uelewa mkubwa katika maswala mbalimbali yahusuyo biashara.


Wamesema kupitia mafunzo hayo wamepata uelewa juu ya ulipaji kodi, uelewa juu ya kupata kusajili majina ya Kampuni, kupitia Taasisi na mashirika yaliyokuwepo kwenye mafunzo hayo.


Mashirika yaliyokuwepo kwenye mafunzo hayo kwa lengo ka kutoa elimu ni Mamlaka ya mapato nchini (TRA) Shirika la viwango nchini (TBS) Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA)


Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC) yamewashirikisha wafanyabiashara wanawake wa mkoa wa Pwani kutoka Halmashauri za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Mkuranga, Kibiti, na Mafia.




No comments:

Post a Comment