Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi amewahimiza Waumini wa Dini ya kiislamu kuendelea kuisoma kwa wingi Quran Tukufu katika kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika fainali za kwanza za Mashindano ya kuhifadhi Quran Tukufu Afrika Mashariki yanayosimamiwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ikiwemo washiriki tisa kutoka nchi za Afrika Mashariki katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 30 Machi 2024.
Aidha Rais Dk.Mwinyi ameiomba Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kuzidisha juhudi za malezi ya vijana na kuwaongoza katika maadili na tabia njema ili wawe raia wema na wenye hofu ya Mungu.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mashindano hayo kufanyika kila mwaka.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amezipongeza Taasisi za Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuandaa mashindano hayo makubwa ambayo yanaitangaza Zanzibar.
Mshindi wa kwanza wa Mashindano hayo ni Mahmoud Kassim Nassor wa Zanzibar aliyepata shilingi milioni 30 mshindi wa pili Abdourahamane Papa Said kutoka Comoro shilingi milioni 20 , na mshindi wa tatu Abdulrahman Mussa kutoka Kenya shilingi milioni 10.
No comments:
Post a Comment