Na Alodia Babara
Bukoba.
Jeshi la polisi mkoani Kagera limekamata silaha 11 zikiwemo bunduki 2 aina ya AK 47 zikiwa na magazine tatu, risasi 115, bastola aina ya glock 17 na bunduki aina ya gobore.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. Blasius Chatanda, akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 14, 2023, amesema kuwa, jeshi hilo linaendelea kufanya oparasheni mbalimbali na kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi katika mkoa huo ambapo katika oparasheni iliyofanyika kuanzia Septemba, 2023 hadi sasa silaha 11 zilikamatwa.
“Katika kudhibiti matukio ya utekaji nyara hasa kwa wafugaji katika mkoa wetu wa Kagera tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 14 wa utekaji, tumekamata silaha mbili aina ya AK 47 zikiwa na magazine tatu pamoja na risasi 115 na bastola aina ya grock 17” amesema Chatanda.
Aidha amesema katika kudhibiti matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ujagili jumla ya bunduki nane aina ya gobore zimekamatwa na kati ya hizo nne zilisalimishwa na watuhumiwa watano kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Amesema jeshi hilo limeendelea kudhibiti wimbi la wizi wa watoto na kufanikiwa kukamata watu wanne ambao walihusika na wizi wa watoto na watoto wanne walikamatwa wakiwa hai.
Ameongeza kuwa, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kwa hatua mbalimbali ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Wakati huo huo, amesems pikipiki za wizi ambazo hazikuwa na nyaraka zozote zipatazo 157 zimekamatwa mkoani Kagera pamoja na nchi jirani ya Burundi baada ya kufanyika oparashen.
Amesema pikipiki 157 zilizokamatwa kati ya hizo 92 zilikamatwa nchini Burundi zikiwa na usajili wa namba za Tanzania zikiwa zinatumika nchini humo, huku pikipiki 65 zikikamatwa mkoani Kagera.
“Kwa sasa pikipiki hizo bado ziko Burundi baada ya kukamilisha taratibu zote za kuzirejesha hapa nchini tutawatangazia wananchi ili waje kuzitambua, na pikipiki zilizopo mkoani hapa watu waje kuzitambua” amesema Chatanda.
Mmoja wa waendesha pikipiki maarufu boda boda manispaa ya Bukoba, Enock Novath, ameliomba jeshi la polisi kuimarisha ulinzi ili kudhibiti matukio ya wizi wa pikipiki ambayo yameshamiri katika mkoa wa Kagera.
Joanes Festo mkazi wa manispaa ya Bukoba amedai kuwa mwaka huu ameibiwa pikipiki mbili na kutoa taarifa kituo cha polisi na kuwa hakuna pikipiki yake ambayo imeishapatikana.
Ameliomba jeshi la polisi kuwa zinapotolewa taarifa za wizi wa pikipiki msako uanze mara moja na siyo kusubili oparasheni kwani kufanya hivyo zitakamatwa pikipiki kabla hazijasafirishwa kwenda nje ya mkoa
No comments:
Post a Comment