Tuesday, April 21, 2020

DC BAGAMOYO ATOA SOMO KUHUSU CORONA.

Image may contain: 2 people, people standing and outdoor 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Mheshimiwa Zainabu Rashidi Kawawa, akizungumza na wananchi katika Halmashauri ya Chalinze kuhusu kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya Corona.
......................................

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Mheshimiwa Zainabu Rashidi Kawawa, amewataka wananchi wilayani humo  kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wizara ya Afya dhidi ya Mapambano ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona yaani COVID-19.


Mheshimiwa Kawawa ametoa maagizo hayo jana katika ziara yake aliyoifanya na timu ya Mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu ya halmashauri ya Chalinze Katika Vijiji vya Lugoba, Msata, Kiwangwa na Mji Mdogo wa Chalinze.

Kawawa alitoa tahadhari kwa wananchi hao kwa kueleza hali halisi ya gonjwa hili la COVID-19 lilivyoikumba Dunia, ikiwemo Tanzania na mikoa yake.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaeleza wananchi hali halisi ya tatizo hili kwa kuwajuza kuwa hata Mkoa wa Pwani kuna wagonjwa wa Corona, hivyo tuna kila Sababu ya kuchukua tahadhari za kujikinga na huu ugonjwa.

Katika mazungumzo yake aliwataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na safari zisizo na ulazima ili kulinda Afya zetu na familia zetu.


Aidha aliwataka wananchi kutumia Balakoa kama kinga dhidi ya maambukizi ya Corona na kutumia vitakasa mikono na maji yanayotiririka kunawa mikono muda wote, pia alitumia muda kutoa onyo kwa wafanyabiashara watakaopandisha bei kwa vitendea vinavyotumika katika Mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu.

"Ole wao watakao pandisha holela bei ya vifaa vinavyotumika katika Mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu kama ndoo, sabuni, vitakasa mikono, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kufungiwa biashara zao." Kawawa alisema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya Dkt Kyungu, alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa mara moja endapo wataona mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Corona bila kuchelewa kwa hatua zaidi, na kuwataka wananchi kufuata kanuni na miongozo iliyotolewa na wizara ya Afya dhidi ya Mapambano ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka, alitoa maelekezo kwa watendaji wa halmashauri kuanzia ngazi ya Kijiji hadi wilaya kuelimisha wananchi namna ya kupambana na Corona sanjari na kuwataka wananchi wa Chalinze kula vyakula vya vitamini"C" ili kuimarisha kinga za miili kama njia mbadala ya kupambana na Corona.

"Tutumie vyakula vya vitamini C na mboga za majani, kwani hivi vyote vinapatikana Katika Mazingira yetu ili kupambana na janga hili. Mkurugenzi alisisitiza.

MAMA SALMA ATOA SARUJI MIFUKO 50 SHULE YA MSINGI KIDONGO CHEKUNDU BAGAMOYO.

 Mbunge wa kuteuliwa ambae pia ni mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Mama Salma Kikwete ametoa msaada wa saruji mifuko hamsini kwa shule ya msingi kidongo chekundu iliyopo kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo.


Alisema hatua hiyo ya kukabidhi saruji mifuko hamsini ni hatua ya mwanzo ya kutekeleza ahadi yake aliyoiweka kwenye mahafali ya darasa la saba ya kutoa mifuko mia moja ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

       
"Nimeahidi kutoa mifuko ya saruji mia moja lakini kwa sasa nimeanza na hii hamsini na baada ya muda nitamalizia iliyobaki" alisema mama Salima.



Aidha, mama Salma amewataka viongozi na wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona ambao umekua ukienea kwa kasi nchini na kuuwa watu wengi duniani kote.


Mama Salma Kikwete aliwasisistiza viongozi hao kufikisha ujumbe kwa familia zao na   wananchi katika maeneo yao juu ya umuhimu wa kuwa makini na ugonjwa huo wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19)


Naye Diwani wa kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo, Abdul Pyallah ameelezea furaha yake wakati wa kupokea mifuko hiyo kwani kwa kiasi kikubwa itainua maendeleo ya elimu shuleni hapo kwakuwa shule hiyo ina changamoto kubwa hasa za
madarasa hali inayoepelekea adha katika suala la kujifunza


Pyalla alisema yeye kama Diwani anapambana kutatua baadhi ya changamoto hivyo anapata faraja anapoona watu wenye moyo wa kujitolea kama mama Salma Kikwete wanapoingiza nguvu zao katika maendeleo ya kata hiyo.


Aidha viongozi wengine pamoja na kamati ya shule hiyo wametoa shukrani zao za dhati juu ya kutekelezwa kwa ahadi hiyo na moyo wa mama huyo wa kutoa na kumuomba asiwachoke kuwasaidia.
 
Sehemu ya Saruji hiyo iliyotolewa na mama Salma Kikwete katika shule ya msingi Kidongo Chekungu wilayani Bagamoyo.

 
Diwani wa kata ya Nianjema Halmashauri ya Bagamoyo, Abdul Pyallah, akiwapanga watu kwa umbali wakati wa kumpokea mgeni rasmi mama Salma Kikwete, ikiwa ni tahadhari ya kujinga na maambukizi ya Virusi vay Corona.
 


Wednesday, April 8, 2020

KAWAMBWA AKABIDHI PIKIPIIKI TATU KWA KIKUNDI CHA BODABODA (UMABOS G4)

 
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) akikabidhi pikipiki tatu kwa kikundi cha waendesha bodaboda kilichopo kitongoji cha Benki kata ya Dunda jimboni humo, pembeni yake ni Diwani wa Dunda, Dickson Makamba.

 Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) akizungumza na wanakikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4). 
....................................


Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa amekabidhi pikipiki tatu kwa kikundi cha waendesha bodaboda kilichopo kitongoji cha Benki kata ya Dunda jimboni humo.


Pikipiki hizo ambazo zimenunuliwa kutokana na mkopo uliotolewa na halmashauri ya Bagamoyo kwa vijana, zimekabidhiwa kwa kikundi hicho kinachojulikana kwa jina la Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4).


Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Mbunge huyo wa jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa amewapongeza vijana hao kwa kuchangamkia fursa na kwamba wao ni mfano wa kuigwa.


Alisema Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli inawajali wananchi wa hali ya chini ndiomana kila halmashauri kuna mfuko kwaajili ya vijana, kinamama na walemavu ambapo makundi hayo hukopeshwa na kurejesha bila ya riba.


Kawambwa amefurahishwa na kikundi hicho kwa kitendo chao cha kuchangamkia fursa kwa kusajili kikundi haraka na kupata mkopo wa halmashauri.


Alisema amefurahishwa kwakuwa yeye alikuwa miongoni mwa washauri wa kikundi hicho toka kuanzishwa kwake jambo ambalo limepa faraja kuona kuna vijana wanaopenda kujituma kwa kujishughulisha na shughuli za halali.


Alisema serikali haiwezi kumpa fedha mtu mmoja mmoja lakini inatoa kwa vikundi ili iwe rahisi kuwahudumia watu wengi wenye uhitaji kwa wakati mmoja.


Aliongeza kuwa,  kikundi hicho kinavyokuwa na kuongeza pikipiki kitasaidia vijana wengine ambao wataendesha pikipiki za kikundi huku nao wakijipatia kipato cha kujikimu na familia zao.


Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Dunda, Dickson Makamba amewapongeza vijana hao na kusema kuwa hao ni vijana wa mfano katika kata yake.


Alisema kikundi hicho hakina muda mrefu toka kuanzishwa kwake lakini mafanikio yake ni makubwa katika kipindi kifupi ukilinganisha na vikundi vingine ambavyo vina muda mrefu.


Aihda, Makamba alisema iko haja ya kuendelea kukisimamia kikundi hicho ili kiweze kufikia malengo yake waliyojiwekea.


Makamba alimueleza Mbunge kuwa, iko haja ya kuwaongezea nguvu vijana hao kwa kuangalia uwezekano wa kuwatafutia bajaji ili waendelee na kazi ya kusafirisha abiria wao hata katika kipindi cha mvua.


Awali akisoma taarifa ya kikundi Katibu wa kikundi hicho Abdalla Shabani Jongo alisema malengo yao ni kupata pikipiki tano na kwamba mpaka sasa wamefanikiwa kupata pikipiki tatu tu.


Alisema pikipiki hizo tatu walizopkoe ambazo zimetokana na mkopo wa shilingi milioni nane kutoka Halmashauri ya Bagamoyo zinawawezesha kupata fedha ya marejesho ili waendelee kujenga uaminifu kwa halmashauri na baadae waweze kukopa fedha nyingi zaidi kwaajili ya kujiendeleza kiuchumi.
 
Diwani wa kata ya Dunda wilayani Bagamoyo, Dickson Makamba, akizungumza na wana kikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4). 
 
 Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, alipowasili katika ofisi ya kikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4).
 
 Vijana wa kikundi cha waendesha bodaboda cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4). wakifurahia mara baada ya makabidhiano hayo yalihudhuriwa na Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.