Wednesday, November 15, 2023

TMDA YANG'ARA MASHINDANO YA SHIMMUTA, YAICHAPA LGTI MABAO 4 KWA 2.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.


TIMU ya soka ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) maarufu kama TMDA FC imeicharaza timu yaChuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo ya LGTI FC kwa jumla ya mabao 4 dhidi ya 2 katika mashindano ya SHIMMUTA yanayoendelea Jijini Dodoma.


Mchezo huo umechezwa leo saa 2:00 asubuhi katika uwanja wa Humanity-1 uliopo Chuo Kikuu cha Dodoma.


Akizungumza mara baada ya mchezo huo kocha wa TMDA Bw. Brian Kyando ameeleza kuwa timu yake ilijiandaa vyema kupata matokeo katika mchezo huo.


"Tunamshukuru Mungu kwa kupata matokeo mechi ya leo. 

Tulijipanga kushambulia kuanzia dakika ya kwanza ili tuweze kupata magoli mengi lakini wapinzani wetu nao walijitahidi kutuzuia tukaishia magoli hayo manne. Mchezo huo umeshapita na sasa tunaangalia michezo iliyo mbele yetu ili nayo tufanye vizuri.


Mashindano ya SHIMMUTA yameanza kuanzia tarehe 12 Novemba, 2023 na yanatarajiwa kuendelea hadi tarehe 25 Novemba, 2023.





Thursday, November 9, 2023

MAKONDA ATOA MAAGIZO KWA MAWAZIRI, KAGERA

 

Na Alodia Babara 


Bukoba. 



Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda,  ametoa maagizo mbalimbali kwa Mawaziri wa wizara nne hapa nchini ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuwapigia simu mawaziri hao na kutoa majibu ya changamoto na kutatua changamoto hizo.


Mawaziri waliopigiwa simu ni pamoja na waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, Waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun, waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa.


Makonda ametoa maagizo hayo leo Novemba 9, 2023 wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara akiongea na wananchi mkoani Kagera uliofanyika uwanja wa mashujaa Mayunga.


Moja ya changamoyo zilizotajwa ni pamoja na ujenzi wa soko kuu, kingo za mto Kanoni, ujenzi wa stend kuu, uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Bukoba, tatizo la nida maeneo ya mipakani na ujenzi wa barabara za lami.


Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akijibu kuhusu changamoto za ujenzi wa soko kuu, stend kuu na kingo za mto Kanoni amesema kuwa maagizo ya katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Makonda ameyapokea na kufanyia utekelezaji haraka, mwezi Desemba 2023 atafika mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua maeneo itakapotekelezwa miradi hiyo


Akijibia changamoto ya vitambulisho vya NIDA kwa upande wa wananchi waishio mipakani waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun amesema kuwa, swala la vitambukisho vya NIDA katika maeneo hayo wizara inalifanyia kazi ili kuharakisha zoezi na wale wenye haki ya kupata kadi za NIDA waweze kuzipata. 


Amesema wameanza mkakati wa kutembelea mikoa iliyopo maeneo ya mpakani kwa kuanza na mkoa wa Mara na baadaye watakwenda Kagera.


Makonda amewataka Askari wa usalama barabarani wote nchini kutowaonea waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na badala yake watumie sheria wanapowakamata na kuwakuta na makosa.

 



HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAVUKA MALENGO UKUSANYAJI WA MAPATO

 

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imevunja rekodi ya kukusanya kiwango katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuaniza Julai mpaka Septemba 2023


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Bagamoyo Mhe. Halima Okashi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo tarehe 09 Novemba 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.



Akizungumza katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani Mkuu huyo wa Wilaya aliwapongeza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuanzia Julai mpaka Septemba 2023. 



Katika kipindi hicho Halmashauri imekusanya zaidi ya shiling bilioni 1 sawa na asilimia 27.7 ambapo ni asilimia 2.7 zaidi ya malengo waliyojiwekea ya asilimia 25.



"Niwapongeze Madiwani wa Kata zote pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato kwenye taarifa yenu inaonyesha mapato yaliyopatikana ni asilimia 27.7 ambapo malengo yalikuwa ni asilimia 25 hivyo hongereni sana kwa ongezeko hilo la asilimia 2.7" alisema Bi Halima Okashi


Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliwataka Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kuongeza ubunifu zaidi ili kuweza kupata wigo wa kuongeza mapato utakaopelekea uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo akipokea pongezi hizo kwa niaba ya Baraza la Madiwani Mhe. Mohamedi Usinga aliahidi kuendelea kuboresha vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuboresha mapato kwenye Halmashauri hiyo.





MAGAZETI YA LEO TAREHE 09 NOVEMBA 2023.