Friday, October 27, 2023

DKT. TULIA ACKSON ACHAGULIWA KUWA RAIS WA MABUNGE DUNIANI.

 

Spika wa Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika leo Oktoba 27, jijini Luanda nchini Angola.


Dkt. Ackson amechaguliwa kwa kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa na anarithi mikoba ya rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka Ureno aliyekuwa rais wa IPU kwa mihula mitatu.


Tulia alipata ubunge nchini Tanzania mwaka 2015, na baadae kuchaguliwa kuwa Naibu Spika na hatimae Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo, Dk Tulia Ackson amesema, “Asanteni kwa kuniamini kwa kunichagua, naipokea nafasi hii kwa unyenyekevu huku nikitambua majukumu yote yanayoambatana na nafasi hii, napenda kuwathibitishi tena kuwa,  jitihada zangu za kufanya kazi mkono kwa mkono na wote ili kuifanya IPU iwe na ufanisi zaidi, yenye kuwajibika na uwazi.”

Wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) walipiga kura ya siri, huku kukiwa na wagombea wanne, ambapo rais mpya Dkt. Tulia Ackson, alipata kura 172 sawa na asilimia 57 ya kura zote zilizopigwa, huku wagombea wengine ni Catherine Gotani Hara kutoka Malawi, aliyepata kura 61, Adji Diarra Mergane Kanouté, kutoka Senegal, aliyepata kura 59, na Marwa Abdibashir Hagi kutoka Somalia aliyeambulia  kura 11. Wote wakiweka historia ya kuwa wabunge wanawake kutoka Afrika, waliogombea nafasi hiyo.

Dkt. Tulia Ackson anakuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na anakuwa mwanamke wa tatu kushika nafasi hiyo baada ya Najma Heptulla kutoka India (1999–2002) na Gabriela Cuevas kutoka Mexico (2017–2020), pia Dkt. Dulia Ackson anakuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushika nafasi hiyo.



Umoja wa Mabunge Duniani IPU inachagua Rais baada ya kila miaka mitatu na lazima anaechaguliwa awe mbunge katika kipindi atakachokuwa Rais.
Rais mpya wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson akihutubua mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa IPU.
Dkt. Tulia Ackson akipongezwa mara baada ya kutangazwa mshindi.
Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) wakimpongeza Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja huo.







MSIGWA AZINDUA RASMI TAMASHA LA SANAA BAGAMOYO.

 



KATIBU Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amefungua rasmi Tamasha la 42 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lililohudhuriwa na wananchi na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambapo alisema kuwa Utamaduni na Sanaa ni Sekta zenye umuhimu mkubwa katika kuleta maendeleo na kukuza ajira hapa nchini.

Katibu Mkuu Bw. Msigwa amesema hayo usiku wa Oktoba 26, 2023 wakati akifungua rasmi tamasha hilo linaloendelea katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kwamba eneo la Sanaa katika nchi yetu ni la kimkakati, ni lazima tulitumie kimkakati, naomba sana vijana wenye vipaji wasizuiliwe kufanya Sanaa, huku nako kuna ajira" amesisitiza Katibu Mkuu Bw. Msigwa.

Hafla ya ufunguzi wa Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 26 - 28, 2023 katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo Bw. George Yambesi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Dkt. Emmanuel Ishengoma, viongozi na wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo.

Baadhi ya Wasanii na vikundi vilivyofungua tamasha hilo ni pamoja na:
Wamwiduka Band, Worrious from the East, msanii Vitalis Maembe, na wengine wengi.


Wednesday, October 25, 2023

WAJASIRIAMALI WAHIMIZWA KURASIMISHA BIASHARA BRELA

 


Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Hashim Komba amewataka wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) na wadau wake kutumia fursa hiyo kurasimisha biashara zao ili biashara zao ziweze kukua.

Mhe. Komba ametoa rai hiyo  Oktoba 24, 2023 wakati akifungua Maonesho ya kwanza ya BRELA na wadau wake, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam. 

“Wito wangu kwenu BRELA na wadau wengine wa maonesho haya ni kwamba tuhakikishe hawa wajasiriamali mbalimbali wanakua, hivyo wasaidiwe kwa kupatiwa elimu ili waweze kurasimisha biashara zao,” amesema Mhe. Komba.

Amesema ili kuboresha zaidi maonesho haya BRELA iendelee kuandaa maonesho kama haya katika maeneo mengine yatakayowezesha wadau wengi zaidi kufikiwa. Ameyataja maeneo ambayo yana idadi kubwa ya wajasiriamali katika Wilaya ya Ubungo kuwa ni Mbezi na Manzese, hivyo BRELA itoe kipaumbele kwa kuwapatia elimu kupitia maonesho kama haya. 

Pia ameitaka BRELA kuimarisha mahusiano na mazuri na taasisi zingine za Serikali hususan Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Serikali za Mitaa ambazo ndizo zinazowakutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa. 

Mhe. Komba amesema Maonesho haya pia yatumike kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa sambamba na kuwa na madawati yanayowakutanisha wadau ili kupunguza watu wa kati (Vishoka) ambao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara. 

“BRELA, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania(TBS) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) shirikianeni katika utoaji wa elimu ili kudhibiti na kupambana na Bidhaa bandia, kuthibitisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali na kuhakikisha wanafanya sajili mbalimbali na kupata leseni," amesema Mhe. Komba.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA itaendelea kuwahamasisha wadau wake kurasimisha biashara zao kupitia majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika maonesho. 

Maonesho ya BRELA na wadau wake ambayo yatahitimishwa na mkutano wa Wadau tarehe 27 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Da es Salaam, kauli mbiu yake ni "Urasimishaji Bashara katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda." 

Tuesday, October 24, 2023

BODI MPYA YA USHAURI YA WIZARA YA AFYA (MAB) KWA TMDA YAZINDULIWA

 

Na. WAF - Dodoma 


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu Oktoba 23, 2023 amezindua rasmi bodi mpya ya ushauri ya Wizara ya Afya (MAB) kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ambayo inawajumbe Saba. 


Waziri Ummy wakati akizindua bodi hiyo mpya amewataka wajumbe hao kuimarisha usimamizi wa TMDA katika upande wa dawa, vifaa na vifaa tiba ili kusiwepo na upotevu wa aina yoyote wa vifaa tiba hivyo. 


“Kazi kubwa mnayotakiwa kufanya ni ufuatiliaji wa mara kwa mara wa bidhaa duni na bandia zinazoingia kwenye soko ili zisiwafikie wananchi wakazitumia”. Amesema Waziri Ummy 


Lakini pia wakati akifungua bodi hiyo Waziri Ummy amewataka wajumbe hao kuharakisha utoaji wa vibali na leseni mbalimbali ili kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wa dawa, Vifaa na Vifaa Tiba. 


“Kwakweli niwapongeze kwa hili bodi iliyomaliza muda wake, sikusikia malalamiko ya mtu kucheleweshewa leseni au kibali cha kufanya biashara hivyo bodi hii mpya mkaliendeleze hili”. Amesema Waziri Ummy 


Aidha, Waziri Ummy amepongeza bodi iliyopita kwa kufanya kazi zake kwa weledi ambalo TMDA imepiga hatua kubwa kwenye masuala mbalimbali ndani na nje ya chi na mafanikio ambayo Wizara pia inajivunia kuyafikia na kuitaka bodi mpya kuendeleza mazuri hayo. 


“Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kwa bodi iliyopita ni pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi ikiwemo mifumo ya TEHAMA kwenye kutoa vibali vya uingizaji bidhaa nchini ambapo sasa vibali vinatolewa ndani ya masaa 24”. Amesema Waziri Ummy


Bodi hiyo iliyoundwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ina wajumbe Saba ambayo inaongozwa na Mwenyekiti aliyeongezewa muda kwa kipindi kingine Bw. Erick Shitindi, Prof. Appolinary Kamuhabwa (Mjumbe) ambae ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).


Pia, Bi. Mariam Mwanilwa (Mkurugenzi wa Mishahara na Maslahi ya Watumishi wa Umma-Ofisi ya Rais Utumishi), CPA Chiku Thabit Yusuf (Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu Shirika la Hifadhi ya Jami (NSSF), Wakili Patricia Maganga (Mwanasheria Mbobezi).


Vile vile yupo Bw. Daudi Msasi (Mfamasia Mkuu wa Serikali) na Bw. Adam M. Fimbo ambae ni Katibu lakini pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TMDA. 





MAGAZETI YA LEO TAREHE 24 OKTOBA 2023

 KURASA ZA MBELE















KURASA ZA NYUMA


















Monday, October 23, 2023

ULEGA, PROF. KITILA WAKUTANA KUJADILI MAENDELEO SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo na kufanya mazungumzo yaliyolenga kufahamu vipaumbele muhimu vya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambavyo vitajumuishwa katika mapendekezo yatakayosaidia kuandaliwa kwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2024/2025. 


Katika kikao hicho ambacho kimefanyika Oktoba 23, 2023 katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, jijini Dodoma, Prof. Kitila aliongeza kuwa, kikao hicho kimelenga kuleta ushirikishwaji wa sekta katika maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/2025.


Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameahidi kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ili sekta za mifugo na uvuvi ziweze kutekeleza majukumu yake sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.


Aidha, Mhe. Ulega ameomba masuala yanayohusu uanzishwaji wa Mamlaka inayosimamia Uvuvi, Chanjo ya Mifugo , Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo na Uchumi wa buluu na Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT-LIFE) kujumuishwa katika mapendekezo hayo.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida ametoa rai kwa Wizara hiyo kuzingatia uzalishaji wenye tija na upatikanaji wa masoko wa bidhaa zinazozalishwa huku akigusia matumizi ya teknolojia katika uzalishaji akitolea mfano ufugaji wa Samaki.