Sunday, December 24, 2017

NAIBU WAZIRI NISHATI ASHANGAZWA NA TATIZO LA UMEME BAGAMOYO.



Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema ameshangazwa na tabia ya kukatika umeme mara kwa mara katika wilaya ya Bagamoyo hali ya kuwa Serikali imeshaweka mikakati ya kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika.

Naibu waziri huyo aliyasema hayo mjini Bagamoyo alipokuwa akifunga maonesho ya wajasiliamali katika viwanja vya shule ya msingi Mbaruku.

Alisema Serikali imeshaweka mikakati ya kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika nchi nzima ili kuenda sambamba na mahitaji katika kuelekea kuwa nch ya viwanda.

Aliongeza kuwa katika mikakati iliyowekwa na serikali iliwahusisha mameneja nchi nzima ili nao waeleze changamoto zinazowakabili na hatimae kuzipatia ufumbuzi ili kuondokana na tatizo la kukatika umeme mara kwa mara.

Aliongeza kwa kusema kuwa, ujenzi wa viwanda, wajasiliamali kujikwamua kiuchumi na maendeleo kwa ujumla vyote hivyo vinategemea upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kufikia malengo.

Alisema kutokana na mikakati hiyo anashangaa kuona mapaka sasa bado kuna tatizo la kukatika umeme Bagamoyo jambo ambalo lilipaswa kuisha.
Alimuagiza meneja wa TANESCO wilaya ya bagamoyo kuhakikisha

anashughulikia changamoto zinazomkabili ili kuondoa tatizo hilo ili kuepuka kuwapa hasara wananchi ambao wanategemea umeme katika kuzalisha na kuhifadhi bidhaa mbalimbali.

Naibu waziri huyo alikuwa na ziara katika wilaya ya Bagamoyo ambapo alipata nafasi ya kuongea na wananchi katika kitongoji cha sanzale kata ya Magomeni na baadae kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo katika Uwanja wa shule ya msingi Mbaruku. 

Aidha, aliwasikiliza wananchi wa kitongoji cha Sanzale ambao hawajafikiwa na huduma ya umeme na kuwahakikishia kuwa Mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu utawafikia ili nao wapate huduma hiyo ya umeme.

Naibu waziri huyo ameridhishwa na hali ya ujenzi wa nyumba za kuishi zilizojengwa katika kitongonji cha Sanzale na kuahidi kutatua tatizo la umeme.

SUBIRA MGALU APONGEZA WANAWAKE BAGAMOYO.


Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu ambae pia ni naibu waziri wa Nishati, (katikati) akiangalia bidhaa ya unga wa viazi vitamu unaotengenezwa na wajasilimali wanawake Bagamoyo wakati wa kufunga maonesho hayo yaliyofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Mbaruku, wa kwanza kulia ni katibu tawala wa wilaya ya Bagamoyo,Erica Yegela , wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, fatuma Latu na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis.
...........................................

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu amepongeza jukwaa la Uwezeshaji Wanawake wilayani Bagamoyo kwa hatua waliyopiga katika kujikwamua kiuchumi.

Subira Mgalu aliyasema hayo leo jumapili Desemba 24 2017 wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali yaliyoandaliwa na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo katika viwanja vya shule ya msingi Mbaruku.

Alisema Jukwaa hilo limepiga hatua hivyo ni jukumu la serikali kuunga mkono juhudi hizo ili wanawake waweze kujikwamua kupitia fursa mbalimbali zilizoandaliwa na serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Mbunge huyo wa viti maalum Mkoa wa Pwani ambae pia ni naibu waziri wa Nishati alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo kuhakikisha anaunga anashirikiana na wanawake hao ili waweze kufikia malengo yao.
Alisema kwa sasa Bagamoyo kuna fursa nyingi za kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kuanza mwezi januari ambapo mahitaji ya vitu mbalimbali yataongezeka.

Aidha, alitoa wito kwa wajasiliamali hao wanawake kujiwekea malengo ya kuzalisha bidhaa malighafi ambazo zitahitajika kwenye viwanda vinavyojengwa wilayani Bagamoyo ili wanawake wajasiliamali wafaidike kupitia maendeleo ya viwanda.

Alisema vipo viwanda kadhaa ambavyo vinahitaji malghafi kutoka kwa wajasiliamali hivyo ni vyema wanawake wakatumia fursa hiyo kujua ni aina gani ya bidhaa zinazohitajika, ubora wake na namna ya kuzalisha.
Aliongeza kwa kusema kuwa dhamira ya Rais John Magufuli ni kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa hali ya chini na badala yake kuwasogezea fursa ili waweze kuzitumia kubadilisha maisha yao.

Alisema kwa Bagamoyo fursa nyingi zimeshandaliwa na utekelezaji wake tayari umeshaanza ikiwemo ujenzi wa viwanda vya aina mbalimbali.

Subira Mgalu alimtaka Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi bagamoyo kutafuta namna ya kupata wafadhili watakaowezsha katika utekelezaji wa miradi ya wanawake haku yeye akiahidi kushirikiana nao.

Nae mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa alisema wananchi wa Bagamoyo kwa sasa wanapaswa kutumia fursa zilizopo ili kujiongezea kipato.

Alisema ni vyema wakaunganisha nguvu kwenye vikundi ili wafaidike na asilimia tano zinazotolewa na Halmashauri kwaajili ya kinamama na vijana.

Akizungumza mbele ya mgeni rasmi mwenyekiti wa Jukwaa la uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Devis alisema anaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuonesha kuthamini kwa wananchi wa hali ya chini na kufanya juhudi za kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Teddy alitoa shukrani kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na Mbunge wa jimbo la Bagamoyo kwa namna walivyotoa ushirikiano ili kufanikisha maonesho hayo ambayo ni njia ya kuwakomboa wanawake kiuchumi.

Alisema kupitia maonesho hayo wajasiliamali wengi wamefaidika kwa kujua fursa mbali mbali ambazo wakizitumia wanaweza kupiga hatua.
  Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis akimkaribisha mgeni rasmi  katika kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo yaliyoandaliwa na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo.
  Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis (kushoto) akimkabidhi zawadi Mgeni rasmi Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu, (Kulia).

Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu ambae pia ni naibu waziri wa Nishati, akiwa ameshika kikaango cha asili cha kupikia Mboga katika moja ya banda la wajasiliamali wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali mjini Bagamoyo leo Tarehe 24 Desemba 2017.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Omari Latu, akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo yaliyofanyika uwanja wa shule ya msingi Mbaruku. 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo yaliyofanyika uwanja wa shule ya msingi Mbaruku.