Friday, December 22, 2017

WALIOLIPIA UMEME WAUNGANISHIWE UMEME KABLA YA 30 DESEMBA 2017.



Serikali imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha wateja wote walioomba na kulipia huduma hiyo mwaka 2017 wanaunganishiwa kabla ya Desemba 30 mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Singida na Dodoma.

“Agizo hili ni kwa nchi nzima. Hakikisheni wateja waliowasilisha maombi yao na kulipia ndani ya mwaka huu wa 2017 wawe wameunganishiwa umeme siyo zaidi ya Desemba 30 mwaka huu.”
 
Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa shirika hilo kutoa elimu kwa umma, hasa wananchi walioko vijijini kuhusu umuhimu wa kutumia umeme ili kuwahamasisha kuunganisha nishati hiyo katika makazi yao.
 
Akifafanua, Waziri alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawajaunganisha umeme katika makazi yao japokuwa tayari Serikali imekwishawafikishia nishati hiyo katika maeneo yao.
 
“Inawezekana baadhi ya wananchi hawajatambua umuhimu wa kutumia umeme, hivyo ni vema wapatiwe elimu husika. Tuwatembelee mahali waliko, hususan vijijini na tuwapatie elimu hiyo,” alisisitiza.
 
Akizungumzia faida za umeme, Waziri Kalemani alisema umeme ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinahitaji nishati hiyo.
 
Aliongeza kuwa, ili dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda ifanikiwe, ni lazima kuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika. “Ndiyo maana tumedhamiria kufikisha umeme hadi vijjijini kwa kasi kubwa, hivyo wananchi tafadhali tumieni umeme ili kukuza pato lenu na uchumi wa nchi kwa ujumla.”
 
Waziri aliwapongeza viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge na Watendaji wa Halmashauri na Vijiji, kwa jitihada zao za kufuatilia utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wananchi ikiwemo upelekaji wa umeme vijijini.
 
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutunza miundombinu ya umeme katika maeneo yao ili isihujumiwe na hivyo kuwakosesha huduma hiyo muhimu na pia kuleta hasara kwa serikali.
 
Ziara hiyo ya Waziri Kalemani ni muendelezo wa ziara mbalimbali ambazo amekuwa akifanya nchi nzima kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupokea kero na changamoto mbalimbali za wananchi kuhusu sekta ya nishati ili zifanyiwe kazi.
 
Katika ziara hii, Waziri ametembelea Wilaya za Mkalama na Singida Vijijini mkoani Singida pamoja na Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Saturday, December 16, 2017

SUBIRA MGALU ATAKA KASI YA REA IONGEZEKE



Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Pangani  mapema jana tarehe 15 Desemba, 2017
 ......................


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaojenga miundombinu ya  usambazaji wa umeme vijijini chini ya  Wakala wa Nishati  Vijijini Awamu ya  Tatu (REA III) kuongeza kasi  ili miradi yote iweze kukamilika ifikapo mwaka 2019.

Mgalu aliyasema hayo mapema jana  tarehe 15 Desemba, 2017 katika ziara yake aliyoifanya katika kijiji cha Bwitini wilayani Korogwe mkoani Tanga, lengo likiwa ni kukagua hatua  ya utekelezaji wa miradi ya  umeme vijijini iliyopo chini ya REA Awamu ya Tatu na kutorishishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mgalu aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema kuwa, Serikali ilikwishawalipa wakandarasi wote malipo  ya awali na kuwataka kuanza kazi mara moja lakini wamekuwa wakifanya katika kasi ndogo hususan katika hatua ya upembuzi  yakinifu.

“ Wakandarasi wengi wamekuwa wakichukua muda mrefu kutekeleza miradi kwa kisingizio cha kufanya upembuzi yakinifu wakati fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi  zimekwishatolewa, nichukue fursa hii kuwatangazia wakandarasi wote nchini kuanza  kazi mara moja,” alisema Mgalu

Aliendelea kusema kuwa mkandarasi yeyote atakayefanya kazi kwa kiwango kisichoridhisha atanyang’anywa kazi na kupewa mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi kulingana na kasi inayotakiwa na Serikali.

Alisema kuwa wananchi wengi kwa sasa hususan walipo katika maeneo ya  vijijini wanahitaji nishati ya umeme kwa gharama nafuu, hivyo wamechoka na masuala ya michakato.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliwataka wakandarasi wote nchini kununua  vifaa kutoka ndani ya nchi  hususan transfoma na nguzo  badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi  kama ilivyoagizwa awali.

Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu ya Tatu  inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo  ifikapo mwaka 2019 karibia vijiji vote vitakuwa na umeme wa uhakika.

Aliendelea kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati  jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa  mradi  wa kuzalisha umeme  kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto  Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa kuzalisha  umeme kwa kutumia  gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi II.

Alisisitiza kuwa serikali imeweka mkakati wa kufufua mkoa wa Tanga kiuchumi hivyo kuwataka wawekezaji ndani  ya nchi kuwekeza kwenye viwanda katika mkoa huo.

Alieleza kuwa kutokana na uwepo wa mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi  Tanga nchini Tanzania katika mkoa wa Tanga,  mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa hivyo Wizara ya Nishati imejipanga katika kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika inapatikana.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mgalu aliwataka wananchi wa  Tanga kutoharibu vyanzo vya maji  katika Bonde la Mto Pangani yanayotumiwa katika uzalishaji wa umeme katika kituo cha kufua umeme cha Hale ili kutoathiri uzalishaji wa umeme katika mkoa huo.

Alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua hali za kisheria wananchi watakaobainika wanaharibu mazingira.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika ziara hiyo.