Tuesday, September 19, 2017

MAJALIWA ATEMBELEA KIWANDA CHA VIGAE CHALINZE WILAYANI BAGAMOYO.

PMO_8650
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ufungaji mitambo ya kiwanda cha vigae cha TWYFORD kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani leo jumanne Septemba 19, 2017. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Ndikilo na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Jack Fen, na mwenye miwani kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid Mwanga.
 PMO_8697
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na viongozi wa serikali na Chama Tawala CCM baada ya kutembelea kiwanda  cha vigae cha TWYFORD kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani leo jumanne Septemba 19, 2017. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete na kulia mwa Waziri Mkuu ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga, (Mwenye suti nyeusi na miwani.)


Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

DC. KIBAHA- WAMILIKI WA VIWANJA 943 KUFUTIWA HATI ZAO.

SAM_5568
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama amesema Serikli wilayani Kibaha ,mkoani Pwani inatarajia kufuta umiliki wa viwanja vya watu binafsi pamoja na taasisi 943 baada ya kushindwa kutekeleza agizo la kwenda kujisalimisha ndani ya mwezi mmoja wilayani humo ili kueleza mpango kazi kwa kila mmiliki .

Aidha inawaomba wawekezaji kujitokeza kwenda kuwekeza wilayani hapo kwani bado kuna maeneo ya kutosha yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda .

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ,mkuu huyo wa Wilaya ya kibaha, alisema ,hatua inayofuata sasa ni kupeleka majina yao kwa waziri wa ardhi na maendeleo ya makazi kwa ajili ya kuwafutia umiliki.

Assumpter alisema kuwa tayari ameshaandaa orodha ya wamiliki hao , na wiki hii anaipeleka ili kufanyiwa kazi.

“Wapo baadhi yao wameshindwa kuendeleza kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano na wengine miaka 15 wakati sheria inataka mmiliki kuendeleza eneo ndani ya miaka mitatu na endapo atashindwa kuendeleza unaweza kunyanganywa eneo husika,” alisema Assumpter .

Alieleza viwanja ambavyo havikuendelezwa kabla ya agizo hilo vilikuwa 1,000 ambapo waliojitokeza ni 246 kuelezea mipango yao .

Viwanja vya taasisi ni 189 ambavyo wahusika nao hawajajitokeza.
“Hatuwezi kuwavumilia,mji wetu wa Kibaha ndiyo makao makuu ya mkoa wa Pwani kwa kushindwa kuendeleza maeneo yao hawa tunawafutia umiliki ili wapewe watu wengine,” alisema .

Hata hivyo ,Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya hiyo imedhamiria kuendeleza mji huo hivyo hataki kuona vichaka ambavyo vimekuwa ni moja ya sehemu ambazo watu wanafanyiwa uhalifu.

“Watu wamekuwa wakifanyiwa vitendo mbalimbali ikiwemo wanawake kubakwa, madereva bodaboda kuporwa pikipiki na kuuwawa kutokana na mashamba na viwanja kushindwa kuendelezwa,” alifafanua Assumpter .

Akizungumzia kuhusiana na taasisi za serikali na umma ambazo zilipewa maeneo na kushindwa kuyaendeleza na kuwa hatarini kunyanganywa maeneo hayo alisema yote yamefika na kueleza jinsi gani watakavyoendeleza maeneo hayo.

Agost 10 mwaka huu ,Assumpter alitoa mwezi mmoja kwa kwa taasisi ,makampuni mbalimbali na wananchi waliokumbatia viwanja vyenye hati zaidi ya 1,000 pasipo kuviendeleza kuhakikisha wanafanya hivyo ndani ya muda huo

WAZIRI MKUU AUTAKA MKOA WA PWANI KUBORESHA MAENEO YA UWEKEZAJI

PMO_8540
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha sabuni cha KEDS wilayani Kibaha, Bw. Jack Feni (Kushoto  kwake) kuhushu  mitambo ya  kiwanda hicho   hicho  wakati alipokitembela September 19, 2017.  Kulia kwake ni. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mahandisi Evarest Ndikilo na kulia ni Mbunge wa Kibaha Mjini, Silyvestry Koka.

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
........................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mkoa wa Pwani waboreshe miundombinu ya maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili waweze kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani.

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Septemba 19, 2017) wakati akizungumza na kwa nyakati tofauti na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni ya unga cha Keds kilichopo Kibaha na kiwanda cha kutengeneza vigae cha Twyford kilichopo Chalinze.

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa viwanda mkoani Pwani na amewaagiza viongozi wahakikishe maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yanakuwa na miundombinu muhimu kama maji, umeme na barabara.

“Nimefarijika kuona miradi hii mikubwa ya ujenzi wa viwanda ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika, nawashukuru kwa kuunga mkono mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.”

Amesema mbali na viwanda hivyo kutoa ajira nyingi kwa Watanzania, pia vitakapoanza uzalishaji vitawawezesha wananchi kupata bidhaa mbalimbali kama vigae kwa bei nafuu kwa kuwa vitakuwa vinazalishwa nchini.

Pia Waziri Mkuu amewataka wananchi wanaofanyakazi kwenye viwanda hivyo wawe mabalozi wazuri wa Taifa kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kuwathibitishia wawekezaji kwamba wao wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi na hakuna haja ya kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa viwanda hivyo Bw. Jack Feng amesema ujenzi wa huo umekamilika kwa asilimia 90 na sasa wako katika hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na ufungaji wa mitambo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji Oktoba mwaka huu.

Amesema vigae watavyovizalisha wanatarajia kuviuza kwa gharama nafuu kwa sababu asilimia 95 ya malighafi inapatikana ndani ya nchi. Pia ameahidi kutoa ajira nyingi kwa wananchi waishio kwenye maeneo yanayozunguka viwanda hivyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo amemuomba Waziri Mkuu awasaidie upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha kuweza kuendesha viwanda katika mkoa huo.

Mhandisi Ndikilo amesema mahitaji waliyonayo ya nishati ya umeme ni megawati 92, ambapo kwa sasa wanasambaziwa megawati 40, hivyo ameomba suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa haraka ili lisije kuathiri uzalishaji.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMANNE, SEPTEMBA 19, 2017.