Tuesday, July 12, 2016

RAIS, DKT. JOHN MAGUFULI AWATAKA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI, WAKAONDOE KERO ZA WANANCHI.


 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na kuwataka kuwatumikia wananchi ikiwemo kuondoa kero zinazowakili wananchi katika maeneo yao ikiwemo utitiri wa kodi hasa kwenye bidhaa wanazozalisha.Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan. wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. 




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya hapa nchini kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi na kuondoa kero zinazowakabili kwa kujiamini, uadilifu na uaminifu.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 12 Julai, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam muda mfupi kabla ya wakurugenzi hao wa halmashauri kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeendeshwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kutekeleza jukumu hilo la kuwaletea wananchi maendeleo na kuondoa kero zinazowakabili, wakurugenzi hao hawana budi kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo ahadi ambazo serikali ya awamu ya tano imezitoa, wakiongozwa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020.

Aidha, amesema wakurugenzi wote wa halmashauri wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na amewataka kutosita kuchukua hatua dhidi ya watendaji ambao wamejigeuza kuwa miungu watu na wanawanyanyasa wananchi.

"Wapo watendaji wa kata ambao ni miungu watu, wanachonganisha wananchi na serikali, katumieni madaraka mliyonayo kuwaondoa kazini" Amesema Rais Magufuli

Mhe. Rais Magufuli pia amewataka wakurugenzi hao kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya serikali na ametumia nafasi hiyo kuagiza wizara zote kuanza kutumia mashine za kielektroniki (EFD) katika ukusanyaji wa mapato kwenye taasisi zote ambazo zinakusanya maduhuli.

Dkt. Magufuli amewasisitiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ambapo kila mwezi serikali hutoa shilingi bilioni 18.777 na ametaka tabia ya wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na wafanyabiashara ama wanasiasa kujinufaisha kupitia zabuni za serikali ikome.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambao walikuwepo wamewataka wakurugenzi hao wa halmashauri kuwa watumishi bora, kusimamia vizuri rasilimali za halmashauri na kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya katika halmashauri zao.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Julai, 2016

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya (Hawapo pichani) walioteuliwa hivi karibuni na kusisitiza kwenye matumizi ya Kanuni, Sheria na Taratibu katika kutimiza majukumu yao. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku. wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.

 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim akiongea na Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa dhumuni la kuwaletea wananchi maendeleo.Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angella Kairuku akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.

 

Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni wakila kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma. Wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni, iliyofanyika Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

MAAFISA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO, WASHIRIKISHWE ILI KUBORESHA SEKTA ZAO.


Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura (Katikati) akizungumza wadau wa kisekta (hawapo pichani) leo Jijini Tanga katika ziara ya kikazi iliyokuwa na lengo la kujua utekelezaji wa shughuli za kisekta katika Mkoa huo,(Kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga Bw.Thobias Mwilapwa na (kulia) Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Mustapha Selemani. 

 
 
 Serikali imeagiza Maafisa Habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo Mikoani kuanza kushirikishwa katika vikao vya maamuzi ili wapate kujua mikakati ya maendeleo kwa sekta zao.

Agizo hilo limetolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Annastazia Wambura alipokuwa katika ziara ya kikazi Jijini Tanga ambapo lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kufuatilia utekelezaji wa shughuli za kisekta kwa Wizara yake katika Mkoa huo.

Naibu Waziri Wambura alisema kushirikishwa katika vikao vya maamuzi kwa watendaji wa Kada hizo kutasaidia kuongeza chachu ya ukuaji wa sekta hizo katika mikoa pamoja na kutoa maoni ya kitaalum kwa sekta hizo kutoka kwao.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 mtenge bajeti ya Kitengo cha Habari na pia mfanye utaratibu wa kupata Maafisa Habari kwa kuanzia ngazi ya Mkoa,Wilaya ,Halmashauri,pamoja na Jiji kwani kada hii ni muhimu kuwepo kwa lengo lakusaidia kutangaza maendeleo na fursa zilizopo katika Mkoa wenu”,alisema Mhe .Wambura.

Pamoja na hayo Mhe. Naibu Waziri Wambura aliendelea kusema Serikali inataka wananchi wapate kujua shughuli zote za maendeleo katika Mkoa wao zinafanyika vipi na mikakati ya maendeleo iko vipo,hivyo ni muhimu kupata Maafisa Habari watakao wasaidia kufanikisha hilo kazi ya kutoa habari hizo kwa umma.

Aidha, Naibu Waziri huyo alisisitiza kuwa Wizara kwa sasa ipo katika mazungumzo na TAMISEMI kwa jili ya kubadili mfumo na kuanzisha Kurugenzi za kisekta kwa Maafisa Habari,Maafisa Utamaduni,Maafisa Sanaa na Maafisa Michezo katika ngazi za Mikoa lengo ikiwa ni kuimarisha sekta hizo.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martin Shigela alisema Mkoa huo unakabiliwa pia na uhaba wa Maafisa Michezo ,Maafisa Utamaduni na Maafisa Sanaa katika Mkoa na Halmashauri lakini suala hilo tayari wameanza kulifanyia kazi kwa kufanya utaratibu wa kupata Maafisa hao.

Halikadhalika naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini Bw. Thobias Mwilapwa alimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ziara yake kwa kuwa ametoa somo zuri la utendaji na pia anaamini atafanyia kazi kilio cha wadau wa michezo wa mkoa huo kwani ni mmoja wapo katika historia ya Michezo ,pamoja na Muziki wa Mwambao (Taarabu) pamoja na Mchezo wa Mbio za Baiskeli.

Pamoja na hayo naibu waziri huyo alitoa wito kwa wakazi wa Tanga katika kipindi wanapokuwa wakifanya shughuli za kimila na desturi kama za Jando na Unyago basi wawashirikishe wataalam wa Afya pamoja na wa Elimu kwa lengo la kutoa elimu ya afya ya uzazi halikadhalika kuelezewa umuhimu wa elimu katika maisha ya vijana wanaofanyiwa shughuli hizo.

Hata hivyo wakazi wote wa mkoa wa Tanga wametakiwa kuongeza juhudi za kusimamia muenendo mzuri wa maadili ya kitanzania ikiwa ni jukumu la kila mtu pamoja na kufanya kazi kwa kujituma zaidi kama kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya HAPAKAZI TU! a


WAKURUGENZIN WAPYA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU, UWAJIBIKAJI NA UAMINIFU.





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya waende wakafanye kazi kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Julai 12, 2016) wakati akizungumza na wateule hao kabla hawajatoa viapo ya maadili katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Jukumu mlilopewa na Mheshimiwa Rais ni nyeti na linahitaji utulivu na kujituma. Kila mmoja wenu anatakiwa akafanye kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na uaminifu,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:

“Ninyi ndiyo injini ya maendeleo katika Halmashauri zote hapa nchini na pia mna dhamana ya kusimamia fedha za maendeleo katika halmashauri zenu. Mtajikuta mna jukumu la kusimamia fedha za ndani pamoja na fedha zinazotoka Serikali Kuu. Hakikisheni mnasimamia matumizi ya fedha hizi ili kupata value for money.”

Waziri Mkuu aliwataka wawe makini wasije wakajikuta wanaingia kwenye migogoro ya kifedha dhidi ya watendaji wengine, migogoro ya kikazi na pia migogoro na wananchi wanaoenda kuwaongoza.

“Mkifika huko ninawasihi mshirikiane na wadau wengine ambao ni wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa idara, watumishi wa idara mbalimbali zilizo chini yenu na watendaji wa kata na vijiji”, alisema.

Alisema wanatakiwa wakasome taarifa mbalimbali ili waelewe majukumu yao pamoja na mipaka yao, waelewe maeneo yao ya utawala ni yapi lakini pia wajipange kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwani imebeba ahadi zilizotolewa na Rais pamoja na Makamu wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi.

Aliwaasa pia wasiache kutafuta hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, aliyoitoa Novemba 20, mwaka jana na kuwataka waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwa vile inatoa dira ya utendaji katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan aliwataka wateule hao watambue dhamana waliyopewa kuwa viongozi wa halmashauri na kwamba wanakwenda huko kuwa watumishi wa umma na siyo watawala.
“Wewe ni mtumishi wa watu, na watu hao pia wana wawakilishi wao ambao ni madiwani. Kwa hiyo fanyeni kazi kwa karibu na madiwani, sikilizeni shida za wananchi na pangeni vipaumbele vya kazi na pia msiache kujifunza. Soma wajibu wako kisheria na kikatiba ni upi lakini pia jipe muda wa kujifunza,” alisisitiza.

“Wewe ni kiongozi kwa hiyo tengeneza watu wako ili wakusaidie kutekeleza kile ulichotumwa kufanya. Fanyeni kazi kwa bidii kwa sababu Tanzania inaenda kwa spidi sana lakini pia mjihadhari na kashfa za matumizi mabaya ya fedha. Msisahau kuwa fedha ni fedheha, ukiitumia fedha vibaya utapata fedheha…” aliongeza.

Akiwahutubia wateule hao, Rais Dkt John Pombe Magufuli aliwataka wawe ni watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwa watengeneza kero na akasisitiza wawe mitume wazuri kwa wananchi.

“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko wanatozwa kodi ndogondogo hata za kuuza mchicha tu. Mtu akivuna mpunga wa kula nyumbani kwake pia anatozwa kodi, ni lazima kodi hizi mkazizuie kwa sababu tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” alisema.

Alisema ana imani nao kwamba wataenda kutekeleza ilani ya CCM na akawataka waandae mipango yao ya maendeleo kila mmoja kulingana na eneo alilopo, waitekeleze hiyo mipango, na wafanye kazi kwa kushirikiana na viongozi walio juu yao na walio chini yao.

Alisema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Serikali imedhamiria kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda na kuwataka wasimamie kilimo ili mazao yatakayozalishwa yaweze kusindikwa hapa nchini. “Nendeni mkajipange tuwe na viwanda vidogo vidogo katika maeneo yenu”, alisisitiza.

“Nataka watu wafanye kazi. Bila kazi hakuna hela. Nataka mkahimizie tabia ya kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yetu. Watanzania wote bila kujali dini zetu, vyama au makabila ni lazima tufanye kwa sababu nataka Tanzania iingie haraka kwenye mataifa ya uchumi wa kati, na hili linawezekana,” alisema huku akishangiliwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM

JUMANNE, JULAI 12, 2016.