Sunday, July 10, 2016

MWISHO WA TIKETI ZA KAWAIDA KATIKA MABASI YA UDART NI JLY 30.





SHIRIKA la Mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (UDART), limetangaza kaunzia Julai 30 mwaka huu kuwa ni mwisho wa matumizi ya tiketi za kawaida kwa abiria badala yake zitatumika kadi.

Hayo yalibainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, David Mgwassa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya kadi badala ya tiketi.

" Tiketi zitaendelea kutumiwa na wanafunzi lakini watu wengine wote watatumia kadi maalumu za kupandia mabasi yetu" alisema Mgwassa.

Alisema Udart imepunguza bei ya kadi hizo kutoka sh.4500 ya awali hadi kufikia sh.2000 ili kutoa fursa kwa kila mwananchi wa kuweza kuipata kadi hizo na kuzitumia.

Mgwassa alisema kadi ziliuzwa ni 55,000 na zilizobaki ni 150,000.

Mkuu wa idara ya Fedha wa Kampuni ya MaxMalipo walioingia ubia ma Udart katika mpango huo, Deogratius Lazari alisema wateja wataweza kulipia kadi hizo kupitia kwa mawakala wao waliopo katika vituo vyote vya udart na kwa njia ya mitandao yote ya simu. 



Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART), David Mgwassa (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu matumizi ya kadi badala ya tiketi. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Fedha wa Kampuni ya MaxMalipo walioingia ubia ma Udart katika mpango huo, Deogratius Lazari.


 Mkuu wa Idara ya Fedha wa Kampuni ya MaxMalipo walioingia ubia ma Udart katika mpango huo, Deogratius Lazari (kulia), akizungumza katika mkutano huo. 

 
Meneja wa Uhusiano wa Udart, Deus Bugaywa (kushoto), akichangia jambo kwenye mkutano huo



TAARIFA YA MSIBA WA MWANDISHI ELIZABETH MAYEMBA.





Uongozi wa Kampuni ya Business Times Limited (BTL), inayozalisha Magazeti ya Business Times, Majira na Spoti Starehe, inasikitika kutangaza kifo cha mfanyakazi wake Elizabeth Mayemba.

Elizabeth Mayemba ambaye ni Kaimu Mhariri wa Michezo Gazeti la Majira alikutwa na mauti Jumamosi ya Julai 9, 2016 saa 2 usiku, akiwa nyumbani kwake Tabata Kisukulu, Dar es Salaam.

Kabla ya kukutwa na mauti, marehemu alifanya kazi zake na majukumu yote ya kila siku bila kuonesha dalili za kuumwa.Akiwa nyumbani kwake saa 2 usiku, alijisikia vibaya na kukimbizwa hospitali ya Amana, akiwa njiani alikutwa na mauti.

Kwa mujibu wa familia ya marehemu, Elizabeth Mayemba atazikwa siku ya Jumanne ya Julai 12, 2016, mkoani Morogoro kwenye Makaburi ya Kola.

Elizabeth Mayemba ataagwa Jumatatu ya Julai 11, 2016 saa 5.00 asubuhi nyumbani kwake Tabata Kisukulu. Baada ya Misa mwili utasifirishwa kwenda Morogoro kwa mazishi.

Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kila mara ili kuwapa nafasi watu wengi wajue ratiba zote zilivyopangwa.

Kampuni imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Elizabeth Mayemba, ambaye mchango wake ulikuwa mkubwa zaidi na ulioonekana kwa kila mtu. Marehemu ameacha mume na watoto watatu wa kiume.

Mungu Ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina

Meneja Mkuu
Business Times Limited

LINDI SEKONDARI YATEKETEA KWA MOTO USIKU WA KUAMKIA LEO.



Moto ukiendelea kuwaka katika moja ya majengo ya Shule hiyo.

Mpaka moto huu ulipodhibitiwa mali zifuatazo zilikuwa tayari zimeshaungua:-

• Madarasa tisa yameungua, ambapo matano yameungua pamoja na samani zilizokuwa ndani na mengine manne ni majengo peke yake Vifaa viliwahi kuokolewa na wananchi.
• Ofisi nne za walimu.
• Maabara mbili za kemia na fizikia zimeungua kwenye paa tu, hivyo samani za ndani hazijaungua.
• Takribani madawati zaidi ya 300 yameteketea kwa moto.

Majengo mengine ya shule yapo salama yakiwemo mabweni. 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewaomba wananchi na uongozi wa shule kuwa watulivu wakati Uongozi wa Mkoa Ukitafuta namna ya Kusaidia Wanafunzi Kuendelea na Mafunzo baada ya kufunguliwa kwa Shule hiyo kesho Julai 11, 2016
 

Aidha, Mkuu wa Mkoa amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kuuzima moto huo kwani haikuwa kazi rahisi, pia amewashukuru Polisi na Jeshi la zimamoto kwa jitihada walizochukua katika kuudhibiti moto huo.

Kwa sasa inafanyika tathmini ya mali zilizoteketea kutokana na moto huo sambamba na uchunguzi wa chanzo cha moto. Taarifa kamili ya uchunguzi na tathmini itatolewa pindi itakapokamilika.

Katika hatua nyingine mtu mmoja alietaka kuiba Komputa mpakato katika tukio hilo amekamtwa na Polisi Baada ya Wananchi kuanza kumpa adhabu.

WAZIRI MKUU WA INDIA APOKELEWA NA RAIS WA TZ. DKT. JOHN MAGUFULI.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wakati wakiwasili kwenye lango kuu la Ikulu jijini Dar es Salaam.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea Waziri Mkuu wa India Narendra Modi katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimtambulisha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Waziri Mkuu wa India Narendra Modi Ikulu jijini Dar es Salaam.



BREAKING NEWS: MTU MMOJA AKUTWA AMEKUFA GUEST BAGAMOYO.
















Mtu mmoja ambae hakufahamika mara moja jina lake amekutwa amekufa katika nyumba moja ya kulala wageni mjini Bagamoyo leo tarehe 10/07/2016, chanzo cha kifo chake hakijafahamika.




Tutawaletea habari kamili mara uchunguzi wa kipolisi utakapokamilika.