Monday, October 13, 2025

BASUTA YATOA TAMKO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 

Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya za Ansaar Sunna Tanzania (BASUTA) Sheikh Ally Zubeir.

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, akiongea kwenye Mkutano huo ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.
...............................

Baraza Kuu la Jumuiya za Ansaar Sunna Tanzania (BASUTA) limetoa tamko kuelekea uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu 2025.


Tamko hilo la BASUTA limetolewa katika Mkutano wake Mkuu uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Juliasi Nyerere jijini Dar es salaam siku ya tarehe 11 Oktoba 2025.






Sunday, October 12, 2025

KAMBAYA ATAHADHARISHA SIASA ZA FUJO

 


Na Rashid Mtagaluka, Dar es Salaam


Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kada maarufu wa chama hicho, Abdul Kambaya, amewatahadharisha Watanzania na wanasiasa wa upinzani wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa siasa ni mashindano ya hoja, siyo matusi wala fujo.


Kambaya alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Makurumla, manispaa ya Ubungo, ambapo aliwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaopotosha jamii kupitia mitandao.


“Siasa sio kushindanisha ukubwa wa sauti, hapana. Siasa ni kushindana kwa hoja. Kama wenzetu wana hoja, basi wazilete mezani, siyo kukaa mitandaoni na kuhamasisha watu kufanya maandamano wakati wao wenyewe hawaonekani na hatujui kama bado wako hai au la,” alisema Kambaya huku akishangiliwa na umati wa wananchi.


Kambaya aliongeza kuwa baadhi ya watu wanaomchukia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hawafanyi hivyo kwa sababu ya mavazi yake au jinsia yake, bali kutokana na uimara wake katika kushughulikia changamoto za wananchi na kasi ya maendeleo ambayo wengi hawakutarajia.


“Wanaomchukia Dkt. Samia wanachukia mafanikio yake. Wamezoea kuona wanawake wakinyamaza, lakini huyu mama ni jasiri, anajituma, anatatua matatizo ya wananchi kwa vitendo,” alisema.


Aidha, Kambaya aliwataka wananchi wa Makurumla kutoingia kwenye mtego wa watu wanaohubiri mambo yasiyotekelezeka, akisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana katika kata hiyo ni matokeo ya uongozi makini wa CCM na Rais Samia.


“Makurumla ya leo sio ile ya mwaka 2020. Dkt. Samia na serikali yake wamefanya kazi kubwa. Tazameni huduma za afya, maji, na elimu mabadiliko ni makubwa. Hata watoto wa shule leo wangeruhusiwa kupiga kura, wangechagua Dkt. Samia kwa sababu wanajua amani yao inayowafanya wasome itaendelea,” aliongeza Kambaya.


Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumpigia kura Dkt. Samia akisema ndiye kiongozi mwenye uzoefu na uwezo wa kusimamia amani, umoja na maendeleo ya taifa.


“Dkt. Samia ni kiongozi mwenye maono. Anatoka katika chama imara chenye historia ya kujenga nchi. Tumuunge mkono kwa kura zetu ili aendelee kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi,” alisema Profesa Mkumbo.


Mkumbo pia aliwaomba wananchi kumpa nafasi ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kusimamia miradi ya maendeleo na kupunguza kero za michango mashuleni.


“Serikali ya Dkt. Samia ilishafuta ada zote, lakini bado kuna wazazi wanalalamika kuchangishwa hovyo. Nikichaguliwa tena, nitahakikisha tatizo hilo linaisha kabisa,” aliahidi Profesa Mkumbo.

Naye Mgombea udiwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga, alisema akichaguliwa ataendelea kushirikiana na Mbunge na serikali kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo miundombinu ya maji na ujenzi wa kingo za Mto China.


“Tutahakikisha mradi wa maji unakamilika kwa wakati na kingo za Mto China zinajengwa ili kuzuia mafuriko. Tayari tumeona mafanikio kwenye mradi wa jengo la kujifungulia kina mama katika zahanati ya kata hii. Huo ndio mwelekeo wa CCM – vitendo, si maneno,” alisema Kimwanga.


Kampeni hizo zimeendelea kuvutia mamia ya wananchi, ambapo viongozi mbalimbali wa CCM katika ngazi ya mkoa na wilaya wamekuwa wakitoa wito wa kudumisha amani na kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Rais Samia.


KIKWETE ASHIRIKI MAPOKEZI TUZO YA SHUKRANI KWA DKT. SAMIA.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameshiriki mapokezo ya Tuzo ya Shukrani kwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa alizozifanya akiongoza mapambano kuwatetea na kuwahudumia Watu wenye Ulemavu , zilizopokelewa na Ndg. Kassim Majaliwa Majaliwa , Waziri Mkuu wa JMT kwa niaba yake Jana tarehe 11 Oktoba Dar- Es Salaam. 


Tuzo hii ambayo inabeba mrejesho wa shukrani kwa kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais. Dkt Samia ameifanya kwa watu wenye Ulemavu katika kipindi cha miaka yake minne ya uongozi wake, ni alama ya shukrani toka kwa watu wenye Ulemavu. Kwa upande wake waziri Kikwete, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mh. Rais kwa jinsi anavyoleta heshima kwenye nchi  na  matunda yake yanaonekana.


Naye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kasim Majaliwa, amewashukuru watu wenye ulemavu kwa kutambua mchango huo wa Mh. Rais na kuwapa salamu pia za Mh. Rais kuwa ataendelea kushirikiana nao.



DC BAGAMOYO, AWATAKA WANANCHI WAMILIKI ARDHI KISHERIA KUEPUKA UTAPELI.

 


MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amewataka wananchi kurasimisha ardhi ili wapate umiliki kisheria waepukane na utapeli na migogoro ya ardhi.


Ndemanga ameyasema hayo Chalinze wakati akizindua Mradi wa Kuboresha Usalama wa Miliki za Ardhi katika Halmashauri ya Chalinze.


Amesema kuwa mfumo wa hati za kisasa hauwezeshi mtu kutumia ujanja ujanja kupata hati na kumiliki ardhi kinyume cha utaratibu hivyo kupunguza utapeli na migogoro ya ardhi ambayo ilikithiri.


Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Rugambwa Banyikila amesema kuwa hadi sasa jumla ya wananchi 515 wamekwisha hudumiwa kupitia kliniki ya ardhi ya wiki ya huduma kwa wateja. 


Banyikila amesema kuwa zoezi la kliniki ya ardhi kwa wananchi wa wilaya ya chalinze lilianza tarehe Oktoba 7 mwaka huu na linafanyika ikiwa ni kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, ambapo limerahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma za kisekta kwa wananchi katika maeneo yao.


Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Chalinze Deo Msilu  akisoma taarifa ya kamishna wa ardhi Mkoa wa Pwani amesema kuwa vipande vya ardhi 24,730 vimetambuliwa na viwanja 23,936 vimepimwa kwenye Kata tatu za Bwilingu na Vigwaza.


Msilu amesema kuwa viwanja 22,022 vya matumizi mbalimbali vimesanifiwa kwenye mfumo wa e–Ardhi na viwanja 20,257 vimepimwa na kuidhinishwa kwenye mfumo huo na zoezi la umilikishaji na viwanja 3,135 vimesajiliwa kwa ajili ya hatua ya umilikishaji.


Thursday, October 2, 2025

SERIKALI YAHIMIZA TAASISI ZA KULEA YATIMA KULINDA IMANI YA WAHISANI

 

Na Albert Kawogo,

Bagamoyo 


SERIKALI imezitaka taasisi zinazosimamia malezi ya watoto yatima na wale wanaoshi katika mazingira magumu kusimamia miongozo,taratibu na sheria katika matumizi ya misaada mbalimbali wanayopewa ili kujenga imani ya wahisani wanaotoa misaada hiyo


    Wito huo umetolewa hivi karibuni  na Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Bagamoyo Abuu Yasin wakati wa sherehe ya miaka 25 ya kuadhimisha kituo cha kuelelea watoto yatima cha Moyo Mmoja kilichoko mjini hapo


   Yasin amesema kumekuwa na matatizo ya baadhi ya vituo vya watoto yatima kutumia vibaya misaada ya wahisani hasa fedha jambo ambalo linawakatisha tamaa watoa misaada na madhara yake yanakwenda moja kwa moja kwa walengwa wakuu wa misaada hiyo ambayo ni yatima.


   "Sisi kama serikali taratibu na sheria zetu ziko wazi na kazi yetu sisi ni kuwahimiza kufuata miongozo hiyo ili kulinda imani ya wafadhili" Amesema


  Aidha Yasin alikisifu kituo cha Moyo Mmoja Trust kuwa kama mfano wa vituo vingine katika kuendesha shughuli zake kwa usahihi jambo ambalo limevutia wahisani kukisaidia kwa muda wa miaka 25 sasa.


  Kwa upande wake Meneja wa Moyo Mmoja Trust Shilinde Masangu amesema kwa zaidi ya miaka 25 Taasisi hiyo imeweza kusaidia kwa ufanisi mkubwa watoto waliopoteza wazazi kutokana ajali magonjwa na hali ngumu za maisha.


   Shilinde amesema wamelea watoto wengi zaidi ambao wamepata elimu ya Chuo Kikuu na ile ya ujuzi wengine wakiajiriwa na wengine wakijiajiri.


  Meneja amesema pamoja na changamoto mbalimbali za malezi ya kielinu lakini kubwa ni Ile ya watoto wanaolelewa hapo kukosa mikopo ya elimu ya juu pindi wakiwa vyuo vikuu.


  "Ugumu wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa watoto wetu walioko vyuo vikuu limekuwa ni tatizo licha ya kujaribu mara kwa mara".Amesema Shilinde


  Naye Meneja wa Taasisi ya Ushirikia wa Tanzania na Norway TANO Olav Holten amesema Norway kupitia TANO kwa muda wa miaka 25 imekuwa mstari wa mbele kusaidia Moyo Mmoja kwenye misaada ya kufanya kituo hicho kiweze kuendelea kutoa huduma zaidi 


  Holten amesema TANO inaamini kuwa kila mtoto anahitaji kupata huduma zote muhimu za makuzi ikiwemo upendo elimu afya na uhifadhi hata kama amepoteza wazazi au walezi.


  Amesema amefurahi sana kuona watoto wakiwa na sehemu wanayoweza kuita hapa ni nyumbani kwao.


  Pia Holten amesema TANO itaendelea kudumisha ushirikiano na kituo hicho kwenye jitihada zote kuimarisha malezi ya watoto ili kulinda ustawi wa utu.

MARUFUKU YA WATAWA, MAPADRE KANISA KATOLIKI HAKI AU KIZUIZI ?

 


ANAANDIKA  RASHID MTAGALUKA


Kauli iliyotolewa Septemba 25, 2025 na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa wa Jimbo Katoliki Lindi, ikiwakataza watawa na waseminari kujihusisha na siasa kwa namna yoyote ile, imeibua mjadala mpana unaohitaji tafakuri ya kina kwa maslahi ya mshikamano wa Taifa letu.



Kwa mujibu wa Askofu Pisa, watawa na waseminari hawataruhusiwa hata kufahamika au kutambulishwa kama washiriki wa chama chochote cha kisiasa, wala kuhusishwa na jambo lolote lenye sura ya kisiasa.



Kauli hiyo imekuja siku moja tu baada ya Masista wa Ndanda kuonekana wakimuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wake wa kampeni.



1. *Haki* *za* *Kikatiba* 


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 20(1), inatamka wazi kuwa:



"Kila mtu anao uhuru wa kukusanyika kwa hiari na kushirikiana na watu wengine, na kwa hiari kuanzisha na kushirikiana na vyama na mashirika mengine kwa madhumuni ya kulinda na kuendeleza maslahi yake".


Vilevile, Ibara ya 21(1) inasema:



" Kila raia ana haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa".



Kwa mantiki hiyo, marufuku ya jumla ya Askofu wetu mpendwa Wolfgang Pisa kwa watawa na waseminari kujihusisha na siasa inaweza kuonekana kama kupunguza haki zao za kikatiba kama raia wa Tanzania.



2. *Mafundisho* *ya* *Kanisa* (Catholic Social Teaching)



Kanisa Katoliki, kupitia nyaraka zake kuu, mara kwa mara limekuwa likisisitiza wajibu wa waumini kushiriki katika maisha ya kijamii na kisiasa:


Gaudium et Spes (1965), waraka wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, unasema:


"Kanisa linaona ni wajibu wa waumini kushiriki katika ujenzi wa jamii ya kidemokrasia, yenye haki na mshikamano".



Compendium of the Social Doctrine of the Church (2004) linabainisha kuwa:


"Shughuli za kisiasa ni sehemu ya wito wa Kikristo wa upendo na mshikamano; kwa hiyo waumini hawawezi kujitenga nazo".



Hii inamaanisha Kanisa linapaswa kuhimiza uwiano: kulinda heshima ya wito wa kitawa, lakini pia kutambua nafasi yao kama raia wanaoshiriki kwenye maisha ya kijamii.



3. *Data* *za* *Kisiasa* *na* *kijamii* 



Tanzania ina zaidi ya Wakatoliki milioni 12 (takribani 30% ya idadi ya watu  Pew Research Center, 2019).


Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, asilimia 80 ya wapiga kura walihusiana moja kwa moja na taasisi za dini (tafiti za Twaweza 2021).


Utafiti wa Baraza la Maaskofu (AMECEA, 2018) ulionesha kwamba asilimia 65 ya wananchi wa Afrika Mashariki wanaamini taasisi za dini zina mchango mkubwa zaidi katika kudumisha amani kuliko vyama vya siasa.



Kwa data hizi, tukubaliane kwamba, kuwatenga watawa na waseminari kabisa kwenye maisha ya kisiasa kunaweza kudhoofisha nafasi ya Kanisa katika mshikamano wa kitaifa.



4. *Mifano* *ya* *Kimataifa* 


Kenya: Wakati wa uchaguzi wa 2007 na 2013, viongozi wa Kanisa Katoliki na makanisa mengine walihusiana sana na wanasiasa,  mara nyingine kwa kuombewa au kuzungumzia masuala ya uchaguzi.



 Badala ya marufuku ya jumla, Kanisa Katoliki Kenya lilitoa _Pastoral_ _Letters_ likiwataka watawa na mapadre kuwa waangalifu ili kuepuka kuonekana kushabikia chama fulani, huku likiwataka washiriki kwenye majukwaa ya kuhubiri amani na mshikamano.



Poland: Nchini Poland, historia ya Kanisa Katoliki haiwezi kutenganishwa na siasa. Wakati wa utawala wa kikomunisti, Kanisa lilikuwa nguzo ya mapambano ya kisiasa kupitia harakati za Solidarity Movement chini ya uongozi wa Papa Yohane Paulo II. 



Hii ilionyesha kuwa pale ambapo haki na demokrasia zinahusiana, Kanisa linakuwa mstari wa mbele.



Amerika ya Kusini (Brazil, El Salvador): 


Hapa, Kanisa Katoliki limekuwa na utamaduni wa Theology of Liberation (Teolojia ya Ukombozi), likihusisha moja kwa moja mafundisho ya dini na mapambano ya kijamii na kisiasa ya wananchi.



 Viongozi wa Kanisa kama Askofu Oscar Romero (El Salvador) waliuawa wakiwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi dhidi ya ukandamizaji wa kisiasa.



Mifano hii michache inaonesha kuwa kuhusika kwa viongozi wa dini katika masuala ya kisiasa si jambo jipya, na linaweza kufanyika kwa namna yenye kulinda mshikamano badala ya kuupunguza.



5. *Uhalisia* *wa* *jamii* *yetu* 


Mfano wa Masista kumwombea Rais Samia haupaswi kuonekana kama ushabiki wa kisiasa, bali ni tendo la mshikamano na kitamaduni cha kuombea viongozi.



 Viongozi wote wa kitaifa, kuanzia Mwalimu Julius K. Nyerere hadi sasa, wamekuwa wakipokea baraka na sala kutoka kwa taasisi za dini. (Rejea hotuba ya Mwalimu 1985)



6. *Hitimisho* 

Kwa mtazamo wa Katiba, mafundisho ya Kanisa, takwimu za kijamii, na mifano ya kimataifa, kauli ya *TEC* inahitaji kupitiwa upya. 



Marufuku ya jumla inaweza kudhuru mshikamano wa kijamii na kuwapokonya raia haki zao za msingi.


Suluhisho bora ni kuweka mwongozo unaozuia ushabiki wa moja kwa moja, lakini kuheshimu nafasi ya watawa na waseminari kama raia wa Tanzania wanaoshiriki katika maisha ya Taifa.



Kwa maslahi mapana ya Taifa letu, taasisi za dini zinapaswa kuendelea kuwa daraja la mshikamano na mshiriki wa kweli katika ujenzi wa demokrasia na maendeleo ya kijamii.


 Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii 

 Simu 0718 406 242