Saturday, December 21, 2024

WANAFUNZI KIDOGOZERO WAISHUKURU LION.

 







Na Omary Mngindo, Kidogozero.



WANAFUNZI wanaioishi katika mazingira hatarishi wakilelewa kwenye kituo cha Faraja, Kijiji cha Kidogozero Kata ya Vigwaza Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameishukuru Lion Club (Host) ya jijini Dar esa Salaam kwa kuwapatia misaada.


Shukrani hizo zimetolewa na wanafunzi Enjo Frank na Faraji Ramadhani baada ya kupokea vifaa vya shule na vyakula vyenye shilingi milioni 1.6, vikikabidhiwa na Rais Mahmood Rajvan, Mountazir Barwani na viongozi wenzao walipofika kijijini hapo kuwafariji watoto hao 41.


"Namshukuru Mwenyeezimungu kwani sikutegemea kupata msaada kama huu, utakaonisaidia katika masomo yangu wakati shule ikifunguliwa, mungu awasaidie na awaongezee pale mlipopunguza," alisema Enjo.


Nae Ramadhani alieleza kwamba kwa msaada huo wa begi, madaftari  pamoja na peni vimempatia chachu ya kuendelea na masomo, huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika elimu yake ya Sekondari.


Kwa upande wao wazazi Mohamed Ally aliishukuru Lion huku akiwahimiza wanafunzi kuongeza bidii katika kusoma, na kwamba zawadi hizo ziwe chachu ya kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.


Evat Mapunda alielezea shukrani zake kwa uongozi huo kwa msaada mkubwa ambao wamewapatia watoto hao, na kuwa kijana wake amepoteza wazazi wote wawili hivyo yupo mikononi mwake hivyo msaada huo umekuwa faraja kubwa kwake.


"Kijana wangu hana baba hana mama mimi ndio anayenitegemea hivyo vifaa hivi vimenigomboa, muendelee na moyo huo wa kusaidia watoto kama hawa hasanteni sana," alimalizia Evat.


Katibu wa kikundi hicho Zena Mindu mbali ya kuwashukuru Lion, pia ameuomba uongozi huo kuendelea kukisaidia kikundi hicho kinacholea watoto hao hao, huku wakiwa hawana msaada wowote.


"Nawashukuru sana mlikuja Ruvu Darajani kukabidhi Matenki ya maji pamoja na vifaa vya shule, nami mlinikabidhi msaada, leo mmekuja hukuhuku Kidogozero ambako ndio tunakosihi na kutusaidia vifaa vya shule pamoja na vyakula, tunawashukuru sana," alisema Mindu.


Akizungumza kwa niaba ya Diwani Mussa Gama, Katibu wake Amos Mwakamale alitoa shukrani kwa Lion huku akiwataka wazazi waaoishi na watoto hao kuhakikisha shule ziapofunguliwa wote wanakwenda kusoma.


Mwenyekiti wa Kijiji Said Sango alimshukuru Barwani na viongozi wote, kwa kuendeleza kazi aliyoianza kijana wake Mouhsin Barwani aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo miaka mitano iliyopita.


"Nimefurahi kuona mnaendelea kutusaidia Kata ya Vigwaza, tunaona kama bado tupo na Mohsin Barwani aliyekuwa diwani wetu miaka mitano iliyopita, hapa Kidogozero kuna tenki alilolitoa  shuleni mpaka leo linatumika, tunawashukuru sana," alisema Sango.


Akitoa neno kwa wanafunzi hao, Barwani aliwataka wanfunzi hao kukazania masomo, na kwamba taifa linawategemea katika kulitumikia miaka ijayo panapouhai, hivyo wakazanie elimu.


Tuesday, December 17, 2024

WAZIRI KIKWETE AHUDHURIA MASHINDANO YA QUR ANI KWA WENYE ULEMAVU.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Ridhiwani Kikwete  ameshiriki mashindano ya Usomaji wa Quraan Takatifu kwa Wenye Ulemavu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Riziki Lulida yaliyofanyika jijini Dodoma.


Katika mashindano hayo ambayo yalikutanisha Wenye Ulemavu kutoka makundi mbalimbali, Waziri Kikwete alitoa  salamu za serikali na kuwakumbusha kazi nzuri anayoifanya Mh. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri Ya Muungano ya Tanzania ikiwemo Mkakati wa kusimamia Haki na Ustawi wa Wenye Ualbino, Sera ya Usimamizi wa Teknolojia saidizi na mapitizo ya sera mbalimbali zinazosimamia maslahi ya Wenye Ulemavu ikiwemo sera ambazo haziendani na mazingira ya sasa. 


Aidha alisema Wizara kwa upande wao walieleza walipofikia katika kila maelekezo ya Mh. Rais, Ilani ya uchaguzi na miongozo mingi imetolewa. 

Wameendelea kumpongeza Muandaaji wa mashindano hayo Bi. Riziki Lulida, na taasisi yake na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na washiriki na kwa upekee Mh. Rais kwa kuunga mkono jambo hilo kwa kuchangia Shilingi Milioni 15. kwa vijana washiriki 30 walioshiriki usomaji wa Qur ani tukufu.



Tuesday, December 3, 2024

WATU 7 WAFARIKI AJALI YA GARI KARAGWE.

 

Na Alodia Dominick,  Karagwe.


Watu saba wamepoteza maisha huku wengine tisa wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu ya haice, kosta pamoja na Lori aina ya scania katika kizuizi cha barabarani kilichopo kijiji cha Kihanga kata ya Kihanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera na chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva.


Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea Desemba 03, 2024 saa 5:00 asubuhi  na kuhusisha lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ lenye Tela namba T472 EAQ likiwa linatokea Kayanga wilaya ya Karagwe kwenda Kyaka lilipofika Kihanga katika kizuizi cha barabarani yalikuwepo magari mawili.


Ameongeza kuwa, moja lilikuwa kosta namba T367 ECP pamoja na toyota  haice yenye namba za usajili T973 DGD yakiwa yamesimama yanaendelea kukaguliwa na maafisa uhamiaji mita kama kumi kutoka kwenye kizuizi ndipo Scania iliyagonga kutokea nyuma na kusababisha ajali hiyo.


"Gari hilo limetokea Mbeya likiwa limebeba mchele kuupeleka Mtukula na baada ya kushusha mchele lilipata mzigo mwingine Karagwe wa kurudi nao Mbeya ambao ni parachichi, huyu dereva ni mgeni katika eneo hilo kwa uzembe na kutokuchukua tahadhari alikuja katika mwendo ambao ni mkali akaigonga toyota haice pamoja na kosta" amesema Chatanda.


Aidha, katika ajali hiyo vimetokea vifo saba wanawake wanne, mwanaume mmoja na watoto wawili huku majeruhi wakiwa tisa wanaume wanne na wanawake watano.


Amesema uzembe wa dereva umesababisha ajali kwani inaonekana alikuja katika mwende mkali lakini ajali haikusababishwa na kufeli breki kwani huko nyuma alikotoka alipita katika mlima wa Kishoju na kwenye kona hivyo ingekuwa breki ule mteremko asingeumaliza.


"Ni wazi kwamba tahadhari za alama barabarani hakuzichukua kwani barabara hiyo inazo alama za barabara na hata kabla ya kizuizi kuna alama pia" amesema Chatanda.


Mmoja wa mashuhuda Adamu Alon mtengeneza majokofu kutoka Kayanga amesema kuwa, ameitwa na mteja Kyaka wilaya ya Misenyi na kupanda Kosta ambayo imehusika kwenye ajali walivyofika Mgakorongo walikuta hilo lori likiwa limesimama dereva anaongea na askari wa usalama barabarani wakapita.


Amesema, wakati gari hilo limefika Kihanga katika kizuizi cha barabarani ndipo Scania hiyo imegonga gari lao likiwa linakaguliwa na maafisa uhamiaji yeye alikuwa amekaa kiti cha mbele na dereva huku akitakiwa kuonyesha kitambulisho na afisa uhamiaji ndipo amesikia kishindo kikubwa na gari alilokuwemo likahama na kwenda mbele.


Ameeleza kuwa, yeye na afisa uhamiaji wamedondoka chini baadaye alipopata fahamu alikuta scania waliyoipita Mgakorongo ndiyo iliwagonga.


Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Karagwe iliyopo Nyakanongo pamoja na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.







Friday, November 29, 2024

VIONGOZI WATEULE WA VITONGOJI NA VIJIJI WAAPA BAGAMOYO.

 







Viongozi wa Vitongoji na Vijiji pamoja na Wajumbe wao walioshinda katika uchaguzi uliofanyika tarehe 27 Novemba 2024. Leo tarehe 29 Novemba 2024 wameapishwa rasmi kushika nyadhifa zao katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. 

Akifungua kikao cha kuwaapisha Viongozi hao, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bagamoyo Bw Shauri Selenda aliwakaribisha na kuwashukuru kwa kuchaguliwa  na kuaminiwa na wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 27 mwezi huu .

"Nichukue nafasi kwa niaba yangu mimi mwenyewe na kwa niaba ya Halmashsuri kwa kuteuliwa kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa,  "Mchakato haukuwa rahisi lakini mmefanikiwa niwapongeze". Alisema Bw Shauri Selenda.

 Katika Uchaguzi huo ulifanyika tarehe 27 Novembe, 2024 vyama mbalimbali vya kisiasa vilishiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwenye vitongoji vyote   167 vya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. 

     Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Shaibu Ndemanga aliwaasa wenyeviti  hao kushirikiana ili kuwahudumia wananchi kama walivyoapa katika viapo vyao.

CCM YASHINDA KWA ASILIMIA 98.82 LINDI

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.


Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Lindi Mkoani Humo bwana Juma Mnwele Leo tarehe 29 November 2024 ametangaza matokeo ya Jumla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa vijiji na vitongoji Katika Manispaa hiyo uliofanyika November 27 mwaka huu 2024


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake msimamizi huyo wa uchaguzi Manispaa ya Lindi amesema Kati ya nafasi za uongozi 1954 zilizoshindaniwa na Vyama vya siasa chama cha mapinduzi kimeshinda nafasi 1931 sawa na asilimia 98.82, chama cha ACT wazalendo wameshinda nafasi 21 sawa na asilimia 1.07


Alitaja chama chama kingine ni chadema ambacho kilishinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.1 kikifuatiwa na chama cha wananchi cuf ambacho kimeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.05 huku chama cha CHAUMA, NCCR MAGEUZI na TLP vikikosa ushindi kabisa

Monday, November 25, 2024

RAIS SAMIA KUSHIRIKIANA NA THE ISLAMIC FOUNDATION KUANZISHA CHUO CHA UALIMU NA MAADILI.

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia kushirikiana na Taasisi ya The Islamic Foundation kuanzisha Chuo cha Ualimu na Maadili katika eneo la Kitungwa wilayani Morogoro.


Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo tarehe 25 Novemba 2024 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Msikiti wa Al Ghaith uliopo maeneo ya Kilakala Flats/old Dar es Salaam Road mjini Morogoro unaomilikiwa na Taasisi ya The Islamic Foundation Chini ya Mwenyekiti wake Aref Nahdi


Aidha, Rais Dkt. Samia amesema katika kipindi hiki dunia imekumbwa na mmomonyoko wa maadili kuna haja kubwa ya kuongeza ujenzi wa Madrasa ili ziwe vituo vya kuwalea watoto kiimani na maadili.


Aliwahimiza wazazi kusimamia malezi bora ya watoto ili jamii iwe na kizazi chenye hofu ya Mungu, na maadili mema.


Akizungumzia mmomonyoko wa maadili, Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref Nahdi, amesema jamii ya sasa imecha ushirikiano katika malezi jamno linalopelekea watoto kupoteza heshima katika jamii na kuharibikiwa kimaadili.


Alisema zamani ilikuwa mtoto akikosea anapewa onyo na mtu yeyote aliyemzidi umri na kwamba taarifa zikifika nyumba kwa mtoto huyo mzazi wa mtoto anaongeza kumpa adhabu ili iwe fundisho kwa mtoto huyo


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akifungua kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi Msikiti wa Al Ghaith uliopo maeneo ya Kilakala Flats/old Dar es Salaam Road mjini Morogoro unaomilikiwa na Taasisi ya The Islamic Foundation Chini ya Mwenyekiti wake Aref Nahdi (kushoto)









Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref Nahdi akizungumza na waandiaji wa habari katika tukio la uwekaji wa jiwe la msingi Msikiti wa Al Ghaith uliopo maeneo ya Kilakala Flats/old Dar es Salaam Road mjini Morogoro, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 25 Novemba 2024.





Saturday, November 16, 2024

HEART TO HEART YASAIDIA MRADI WA MAJI ZAHANATI YA NAMUPA

 






NA HADIJA OMARY,   LINDI.


Hatua ya Taasisi ya heart to heart Foundation kwa ufadhili wa KOICA kuchimba kisima cha maji Katika Zahanati ya namupa iliyopo Katika Kata ya nyangao halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi  inaelezwa kuwa ni msaada kwa wanawake wajawazito wanaokwenda kujifungua Katika Zahanati hiyo kutobeba maji kutoka majumbani kwao



Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga Mfawidi wa Zahanati hiyo Dr. Paul Dominic alisema mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bi victoria Mwanziva Jana November 15, 2024 wakati wa makabidhiano ya kisima hicho ni kwamba kutokana na  tatizo hilo la  ukosefu wa maji  Katika Zahanati hiyo inawalazimu kina mama wanaofika kwa ajili ya kujifungua  kubeba maji kutoka majumbani 


" Katika kipindi ambacho kina mama walikuwa wanakuja kupatiwa huduma ya kujifungua Katika Zahanati yetu  walikuwa wanalazimika kubeba maji kutoka majumbani kwao na wengine wanabeba kutoka mtoni kwa ajili ya kuweza kusaidia kukabiliana na upungufu wa maji ulikuwepo na kuweza kukamilisha zoezi la mama kujifungua ambalo linahitaji maji mengi".


Hata hivyo Dkt Dominic alisema kuwa kapatikana kwa maji hayo pia kutaweza kusaidia kupunguza magonjwa yote yanayotokana na maji.


Nae Melina Simon Amesema tatizo hilo lilikuwa likiwafanya wamama wajawazito kutoka kijijini wakiwa na maji na pengina yasitosheleze mahitaji na kulazimika kurudi tena nyumbani kwa mara ya pili ili kufuata maji mengine ili kumalizia kupata huduma hiyo.


Mratibu wa Mradi kutoka heart to heart Foundation Innocent Deus Amesema Utekelezaji wa mradi huo ni moja ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwenye jamii husika ambapo  kupitia Mradi huo wa miaka mitatu Taasisi hiyo inalenga kufikisha huduma ya maji Safi na salama Katika vituo vya Afya na Zahanati 15 ndani ya halmashauri hiyo ya Mtama .


Amesema Katika kijiji hicho cha Namupa ujenzi huo umehusisha huduma Kwenye Zahanati hiyo pamoja na kusogeza huduma hiyo kwa wananchi .


"Kingine tumeona kulikuwa na changamoto Katika chumba cha kujifungulia ambapo kwenye hicho chumba kulikuwa hakuna huduma ya maji hivyo Katika hii Zahanati ya namupa kwa sababu tumetaka iwe ya mfano tumeunganisha pia huduma hiyo kwenye hicho chumba cha kujifungulia".


Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bi victoria Mwanziva akimuwakilisha Mkuu wa mkoa huo amesema kama serikali ya wilaya  itaendelea kuthamini mchango unaotolewa na taasisi mbalimbali ikiwemo heart to heart katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kutatua changamoto za wananchi ambapo aliwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ya maji ili idumu kwa muda mrefu.


"Mheshimiwa Rais Samia suluhu Hassan amewekeza Sana Katika sekta mbalimbali, amewekeza Katika sekta ya maji, Elimu,  sekta ya Afya lakini tunapowapata Wadau wetu kama hawa heart to heart Foundation wanakuja kuongezea nguvu Sisi hatuna budi  kuwashukuru Sana Sana" 


GHOROFA LAPOROMOKA KARIAKOO

 


Jengo la ghorofa Kariakoo mtaa wa Kongo na Mchikichi Jijini Dar es aalaam limeporomoka leo asubui Novemba 16, 2024. huku watu kadhaa wakiwa chini ya kifusi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Charamila amefika eneo la tukio na kuwataka walio hai ndani ya jengo hilo wawe watulivu ili kuona namna ya kuwaokoa 

Vikosi vya jeshi la ukoaji na zimamoto tayati vimewasili eneo la tukio, Vikosi vya jeshi la polisi vimefika eneo la tukio 

Juhudi za kuokoa watu zinaendelea kwa kushirikiana vikosi vya jeshi la uokoaji na zimamoto, jeshi la polisi na wananchi wote waliopo eneo la tukio wakitoa ushirikiano

Sunday, November 10, 2024

MUFTI NA SHEIK MKUU WA TANZANIA APONGEZA MRADI WA KUTAFSIRI QUR’AN TUKUFU NENO-KWA-NENO KWA LUGHA YA KISWAHILI

 


Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakary Zubeiry bin Ally, amempongeza Dkt. Shehnaz Shaikh kwa kazi yake ya kujitolea katika kuandaa tafsiri ya Qur’an neno-kwa-neno kwa lugha ya Kiswahili.
 
Katika mkutano uliofanyika leo ofisini kwake Kinondoni, Dar es Salaam, mara baada ya swala ya Ijumaa, Dkt. Abubakary aliutambua mradi huo kama rasilimali nzuri kwa Waislamu wanaozungumza Kiswahili, na kwamba utawasaidia kuelewa Qur’an kwa undani wa kipekee.
 
Dkt. Shaikh, mzaliwa wa Gujarat, India, na kwa sasa akiishi Dallas, Marekani, aliandamana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu, Bi Shamim Khan, na Alhaj Albert Marwa, ambaye aliratibu ziara yake. 
 
Dkt. Abubakary alitoa shukrani zake kwa kujitolea kwa Dkt. Shaikh, akibainisha kwamba ingawa wengi wanaweza kuelewa maana pana ya Qur’an, ni wachache wanaoweza kuifahamu kwa kina neno kwa neno. 
 
Uelewa huu, alieleza, huleta muunganiko wa kiroho na uwazi zaidi wa mafundisho ya Qur’an, jambo ambalo tafsiri yake inaleta ufahamu mkubwaa zaidi kwa wasomaji wa Kiswahili.
 
Dkt. Abubakary alisisitiza umuhimu wa lugha sahihi katika kutafsiri Qur’an, akisema kuwa Kiswahili kinahitaji umakini mkubwa wakati wa kufikisha maandiko ya Kiarabu. 
 
Alionyesha imani kwamba wasomi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), ambao watasaidia kukamilisha tafsiri hiyo, wana ujuzi wa kutosha kwa kazi hii nyeti.
 
Mufti pia alielezea umuhimu wa tafsiri hii ya neno kwa neno katika dunia ya sasa inayounganishwa zaidi, kwani Waislamu wengi, hasa vijana na wale wanaoishi katika maeneo yasiyozungumza Kiarabu, hukutana na changamoto ya kufikia lugha asilia ya Kiarabu ya Qur’an. 
 
Alisema ingawa tafsiri za jumla huleta uelewa wa kawaida, mara nyingi hukosa muundo na maana halisi ya Qur’an. Hivyo Tafsiri ya Dkt. Shaikh, kwa kutoa ufafanuzi sahihi wa neno kwa neno, inakuwa ni zana muhimu ya kujifunza na kutafakari, ikiwaruhusu wasio na ujuzi wa Kiarabu cha zamani kuelewa kwa undani Maandiko Matakatifu.
 
Dkt. Abubakary alimshukuru Alhaj Marwa kwa kuratibu ziara ya Dkt. Shaikh na kumsifu kwa kujitolea kwake kuendeleza elimu ya Kiislamu. Alielezea mradi wa tafsiri ya Dkt. Shaikh kama mfano bora wa wajibu wa kusambaza ujumbe wa Mwenyezi Mungu.
 
Kwa upande wake, Dkt. Shaikh alieleza shukrani zake kwa Mufti kwa kubariki mradi huo. Akihitimisha ziara yake ya siku tano, alishiriki kuwa tafsiri yake imekubaliwa na kutumiwa katika nchi kadhaa duniani. 
 
Amesema mradi huo haubadilishi hata nukta moja ya Qur’anbali kila neno katika Kitabu hicho Kitukufu kinatafsiriwa neno kwa neno kama lilivyo na kulitafsiri kwa Kiswahili.
 
Tangu mwaka 2010, Dkt. Shaikh ametoa matoleo matatu ya tafsiri ya Qur’an kwa Kiingereza na Kiurdu, pamoja na vitabu vya watoto, vinavyopatikana kwenye Amazon. Pia hutoa rasilimali za bure mtandaoni, ikiwemo mihadhara ya YouTube na PDF zinazoweza kupakuliwa.
 
Akiwa katika chuo cha MUM Morogoro, Dkt. Shaikh alishuhudia kuundwa kwa timu ya wahadhiri kumi ambao wataendeleza mradi wake, wakiwezeshwa kwa zana za teknolojia na maelekezo. 
 
Juhudi hii mpya inafuata kazi yake ya miaka kumi ya kutafsiri, ambayo sasa inasimama kama rasilimali muhimu kwa Waislamu wanaozungumza Kiingereza na Kiurdu duniani kote.

Thursday, October 24, 2024

DAKTARI KIZIMBANI KWA KUBAKA MTOTO WA MIAKA 12 BUKOBA.

 

Na Alodia Dominick, Bukoba


Daktari wa viungo Haruna Ayubu maarufu kama Rubai (63) mkazi wa kata ya Rwamishenyi manispaa ya  Bukoba amepandishwa kizimbani kwa shitaka la ubakaji wa mtoto wa miaka 12.


Rubai amefikishwa katika mahakama ya wilaya Bukoba Oktoba 23 mwaka huu na kusomewa kesi ya jinai namba 30251/2024.


Upande wa mashtaka unaongozwa na mawakili wawili ambao ni Matilda Assey pamoja na Alice Mutungi.


Akisoma maelezo ya awali wakili upande wa mashtaka amesema kuwa, kati ya Desemba 2023 na Oktoba 19, mwaka huu  mshitakiwa amekuwa akimuingiza mhanga katika moja ya chumba katika ofisi yake iliyopo mtaa wa Pwani, kata ya Miembeni manispaa ya Bukoba.


Assey ameeleza kuwa, alipoingia katika chumba hicho alimvua mhanga nguo zake za ndani kisha na mshitakiwa kuvua nguo zake na kuchukua uume wake na kuuingiza kwenye uke wa mhanga baada ya mshitakiwa kumwingilia au kumbaka mhanga amekuwa akimpatia sh. 10,000 au 5,000 kwa ajili ya kuwapelekea wazazi wake.


Aidha amesema, Oktoba 19, mwaka huu mhanga alikwenda tena katika ofisi ya mshitakiwa kwa lengo la kuchukua fedha ambayo amekuwa akimpatia kama msaada na baada ya mhanga kufika mshitakiwa alimpeleka katika chumba kisha kumbaka na baada ya hapo alimpatia sh.1,000 akanunue soda.


Vilevile, mhanga alipotoka katika chumba hicho ndipo alitokea askari polisi na kumuhoji mhanga ndipo mshitakiwa aliweza kukamatwa na kisha kupelekwa kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano.


Mhanga alipelekwa hospitali na daktari alithibitisha kuwa ni kweli aliingiliwa kutokana na michubuko sehemu ya uke wake akimaanisha kuwa mhanga alikuwa ameingiliwa.


Upelelezi wa shauri hilo umekamilika wapo tayari kuendelea na kesi na upande wa mashtaka wana mashahidi 10, vielelezo vya maandishi vitatu na ripoti ya daktari.


Wakili wa upande wa utetezi  Frank  John, ameeleza mahakama hiyo kuwa hawako tayari  kuendelea na kesi  jana na kudai kuwa ili mshtakiwa aweze kusikilizwa kikamilifu lazima awe amepewa maelezo ya mlalamikaji.


Wakili John, amesema pamoja na kusomewa shitaka bado mshitakiwa hajapewa hati ya mashtaka na hoja ya tatu  apate muda wa kuongea na mteja wake ili aone ni jinsi gani ya kuweza kumtetea vizuri katika shtaka linalomkabili na ndiyo msingi muhimu wa haki ya kuwakilishwa na wakili.


Pia ameiomba mahakama kuahairisha shauri hilo kwa tarehe nyingine  ambayo watakubaliana pande zote mbili upande wa utetezi na upande wa mashtaka kwa sababu siku moja kabla ya kesi hiyo alipata msiba wa kufiwa na kaka yake.



Akijibu hoja za wakili wa upande wa utetezi wakili wa Serikali  Alice Mutungi,amesema mshitakiwa alifikishwa mahakamani tangu asubuhi hadi saa kumi jioni kama alitaka kuongea na mteja wake wangekuwa wameshaongea na kuiomba mahakama kuangalia maslahi  ya mtoto ambaye ni mhanga katika shauri hilo ambaye pia amekuwepo mahakamani hapo tangu asubuhi kwa ajili ya kusikilizwa.


"Tukisema shauri hili liahirishwe mtoto aondoke na kurudi tena tunaona kwa mazingira haya sio salama kwa mtoto, tunaiomba mahakama yako tukufu kwa maslahi ya mtoto shauri hili lisikilizwe kwa haraka ili mtoto asiwe anakuja mahakamani na kurudi"amesema wakili Alice.



Amesema  hati ya mashtaka amepewa wakili wa mshitakiwa na wakili hajakana amekiri kupokea hati hiyo kisheria, wakili ni muwakilishi wa mshitakiwa na yupo kwa ajili ya kumsemea.


Hakimu wa mahakama ya wilaya Endrew Kahabuka baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, upande wa wakili wa utetezi na upande wa mawakili wa mashitaka amewataka upande wa utetezi kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni wadhamini wawili wakazi wa manispaa ya Bukoba wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya sh.milioni nne kila mmoja na mtuhumiwa kutakiwa kutotoka ndani ya manispaa ya Bukoba labda kwa kibali maalum cha mahakama.


 Vilevile upande wa utetezi wametimiza masharti hayo na mshitakiwa amedhaminiwa kesi yake itatajwa Oktoba 29, mwaka huu.


Hata hivyo, baada ya kudhaminiwa mshitakiwa amekamatwa tena akiwa amefika nyumbani kwake.


Tuesday, October 22, 2024

TAMASHA LA SANAA BAGAMOYO KUZINDULIWA TAREHE 23 OKTOBA 2024

 

Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Tamasha la sanaa Bagamoyo, leo tarehe 22 Oktoba 2024. katika ukumbi wa TaSUBa mjini Bagamoyo.

.................................

Na Athumani Shomari Mkwama.

Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linatarajiwa kufunguliwa rasmi Tarehe 23 Oktoba 2024 katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)


Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa TaSUBa mjini Bagamoyo, Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, amesema wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) wamejipanga kupokea wageni na kuwaburudisha kutokana na burudani za sanaa na utamaduni zitakazowasilishwa kwenye Tamasha hilo.


Amesema TaSUBa imekuwa ikifanya tamasha kama hilo kila mwaka na kwamba kila mwaka linakuwa bora zaidi kuliko mwaka uliopita na mwaka huu pia litakuwa bora zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita.


Ameongeza kwa kusema kuwa, lengo la Tamasha hilo ni kutangaza kazi za wasanii kimataifa, kukuza vipaji na kutoa fursa kwa wasanii wa ndani kuweza kufanya kazi zao nje ya nchi kutokana na wageni kutoka nchi mbalimbali wanaohudhuria katika Tamasha hilo.


Alisema Serikali imejipanga kuinua kazi za  wasanii na kuimarisha utamaduni wa Mtanzania ili asili ya furaha isiyoharibu maadili ya utamaduni wa mtanzania ibakie kama ilivyopokelewa kutoka kwa wazee waasisi wa Taifa hili lakini pia ndio malengo ya serikali katika awamu zote ikiwemo awamu hii ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Aliongeza kwa kusema kuwa wapo vijana wadogo wameanza kuonesha vipaji vyao vya sanaa na utamaduni hivyo ni wajibu wa serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kuwalea vijana hao ili kutimiza ndoto zao na kukuza vipaji vyao kwa kuzingatia maadili na utamadani wa kitanzania.


Naibu waziri huyo wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametumia nafasi hiyo kuwaalika watanzania wote kuhudhuria katika Tamasha hilo litakalodumu kwa muda wa siku nne ndani ya mji wa kihistoria Bagamoyo.


Akizungumza wakati wa kumkaribisha  Naibu waziri, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema wamejipanga kuimarisha ulinzi wakati wote wa Tamasha na kuwahakikishia wageni wote watakaowasili Bagamoyo kuwa wapo katika eneo salama.


Amesema maandilizi yameenda vizuri ya kuhakikisha kila mgeni atakaewasili Bagamoyo kwaajili ya Tamasha la Sanaa na Utamaduni atapata sehemu ya kulala iliyokuwa bora na salama.


Awali akitoa Taarifa ya Tamasha hilo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye, amesema Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo,  litahusisha shughuli mbalimbali za kisanii, kiuchumi na kijamii lengo likiwa ni kuvutia wadau na watazamaji kutoka ndani na nje ya nchi.


Amesema Tamasha hilo litahusisha jumla ya vikundi 74 ambapo vikundi 61 ni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar 2, na vikundi 11 vya kimataifa kutoka nchi za Afrika ya kusini, Zambia, India, Ujerumani, Brazil, Uhispania, Botswana na visiwa vya Mayote.



Ameeleza kuwa, vikundi hivyo vitafanya maonesho ya Sanaa za jukwaani ikiwemo ngoma, za asili na za kisasa muziki wa asili na wakisasa maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho na mazingaumbwe.


Alifafanua kuwa, Tamasha la 43 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo litafunguliwa rasmi tarehe 23 Oktoba 2024 na mgeni rasmi anatarjiwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Dkt. Damas Ndumbaro na kilele chake kitakuwa tarehe 26 Oktoba 2024 ambapo mgeni rasmi wa kufunga Tamasha hilo anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Tulia Ackson.








Sunday, October 20, 2024

MTAALAMU BINGWA WA NYONGA NA MAGOTI KUTOKA UINGEREZA AWASILI DAR.





Atashirikiana na wataalamu wa Mloganzila

Na Mwandishi Wetu


MTAALAMU bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti  kutoka hospitali ya Queen Elizabeth ya Uingereza Profesa Mamoun AbdelGadir, amewasili jijini Dar es Salaam kwaajili ya kambi ya matibabu ya siku tano kwa watanzania.

Daktari huyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani atafanya upasuaji huo kwenye kambi itakayofanyika katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila  kuanzia Jumatatu 21,Oktoba 2024.

Aliwasili leo  katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo alipokelewa na wafanyakazi wa Global Medicare ambao wameratibu kambi hiyo kwa kushirikiana na Muhimbili Mloganzila.

 Akizungumza kwenye mapokezi hayo, Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro,  alisema wamefurahi kuona amefika salama nchini Tanzania na kwamba ujio wake utakuwa wa manufaa makubwa kwa watanzania wenye matatizo ya nyonga na magoti.

“Tumefurahi kuona umefika salama na tunatarajia watanzania wengi watanufaika na ujio wako kwenye kambi hii ya siku tano itakayoanza katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila kuanzia Jumatatu,” alisema

Naye Profesa Gadir aliishukuru serikali ya Tanzania na taasisi ya Global Medicare kwa kuratibu vyema safari yake ya kuja nchini Tanzania na aliahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa watakaojitokeza kwenye kambi hiyo.

 

“Natarajia tunashirikiana vizuri sana na wataalamu wenzangu wa hapa nchini kwenye kambi hii ya siku tano na kwa huduma hii natarajia tutaongeza chachu ya ushirikiano wa nchi zetu na tutabadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji wa aina hii kwa wataalamu wetu,” alisema

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali ya Mloganzila, Goodlove   Mfuko, alisema hivi karibuni kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kwenye kambi hiyo watashirikiana na mtaalamu huyo.

“Mtaalamu huyu atashirikiana na madaktari bingwa ambao ni wataalamu wa mifupa na ajali hapa Mloganzila, hii itakuwa mara ya pili kutoa huduma  kama hii kwani mara ya kwanza tuliwafanyia upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti wagonjwa 170 kwa mafanikio makubwa,” alisema

“Kwa hiyo kwenye kambi hii ambayo ni ya pili  tutashirikiana na daktari huyu mbobezi kutoka Uingereza kupata uzoefu ili tuweze kuboresha zaidi huduma zetu hapa Muhimbili Mloganzila,” alisema

Aliwashauri watu wenye matatizo ya nyonga na magoti wafike Mloganzila kwaajili ya kupewa hiyo huduma ya kubadilisha nyonga na magoti kutoka kwa mtaalamu huyo wa Uingereza .

Aron Mwamyanda ambaye alifanyiwa upasuaji wa goti kwenye kambi iliyopita Mloganzila alisema aliugua magoti kwa miaka mitatu na alizunguka hospitali nyingi bila mafanikio.

“Nilienda hadi kwa waganga wa jadi lakini sikufanikiwa lakini mtoto wangu mmoja aliposikia kuna wataalamu wa magoti na nyonga hapa Mloganzila alinileta. Nilikuja wakanipiga wakasema hali yangu ni mbaya wakanipa gharama wakanitibia,” alisema

“Baada ya kunifanyia upasuaji hali yangu imekuwa tofauti kabisa kwasababu naweza kufanya mambo mengi ambayo awali sikuwa na uwezo wa kuyafanya na natarajia nitarejea kwenye hali yangu ya kawaida,” alisema

TRA KAGERA YAWAPA ELIMU YA KODI WAANDISHI WA HABARI.

 

Afisa uhusiano mkuu kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Hudson Kamoga, akizungumza katika mafunzo hayo.

..............................................

Na Alodia Dominick, Bukoba


Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) nchini imeendelea kusisitiza wananchi wanaponunua bidhaa yoyote kudai risit na wanapouza kutoa risit kwa kufanya hivyo pande zote zitakuwa zimechangia ulipaji kodi inayosaidia katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.


Afisa uhusiano mkuu kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Hudson Kamoga ameyasema hayo Oktoba 19,2024 wakati akizumgumza na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo.


Kamoga amesema, waandishi wa habari ni sehemu ya kuchochea maendeleo ya nchi yao na wanao wajibu wa kuelimisha jamii juu ya faida zinazopatikana kutokana na ulipaji kodi kwani asilimia 70 ya mapato ya serikali inatokana na kodi huku asilimia inayosalia ikitokana na wahisani mbalimbali.


"Unaponunua bidhaa ukadai risit unatimiza wajibu wako, risit ni ulinzi kwa bidhaa uliyoinunua unaweza kununua bidhaa ikiwa na changamoto usipokuwa na risit huwezi kurudishiwa bidhaa hiyo, inapotokea ulinunua simu bila risit ikatokea kuna mtu mwingine aliibiwa simu inayofanana na ya kwako mtu akasema hii ni simu yangu unajiteteaje kwamba hiyo simu ni ya kwako na siyo ya mtu yule anayedai" amesema Kamoga 


Kamoga ameongeza kuwa, unaponunua bidhaa ukadai risit unaisaidia serikali kukusanya mapato yake na kuwa yule aliyekuuzia bidhaa kama hajakupa risit unamsaidia kukwepa kulipa kodi hivyo wananchi waone umuhimu wa kudai risit ili kuisaidia serikali kusonga mbele.


"Unaweza kununua kitu dukani bila kudai risit alafu ukafika nje wakasema kuna kibaka ameiba kama huna risit wewe ukikamatwa kama mwizi hautaweza kujitetea, wananchi waone kudai risit ni wajibu wa kisheria lakini ni wajibu wao wa kizalendo kwa nchi yao na ni ulinzi wa bidhaa anayoinunua" ameeleza Kamoga 


Kwa upande wake, meneja msaidizi huduma kwa mlipa kodi mkoa wa Kagera Estomih Mossi ameeleza kwamba, elimu ya kodi imekuwa endelevu na walipa kodi inabidi waipate kutoka kwa waandishi wa habari kupitia vyombo vyao vya habari kwani wao ni kiunganishi kwa TRA na wananchi.


Amesema mamlaka hiyo kwa mwaka 2023/2024 walikusanya mapato zaidi ya trioni 28  na mwaka 2024/2025 wanapaswa kukusanya trioni 30.4


Akitoa mada ya elimu kwa waandishi wa habari afisa elimu na mahusiano TRA Kagera Rwekaza Rwegoshora amesisitiza utunzaji wa kumbukumbu kwa wafanyabiashara kwani itawaondolea kulipa kodi kubwa tofauti na mitaji yao ikiwemo kupata adhabu ya faini au kifungo.


Aidha alisisitiza kila mwananchi mwenye miaka 18 na kuendelea kuwa na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN namba) awe anafanya biashara au hafanyi na kuwa sheria hiyo ilifanyiwa maboresho mwaka 2023 ya mtanzania yeyote kuanzia umri huo anapaswa kuwa na namba ya tin 

kwani itamsaidia kupata huduma mbalimbali.


Alitolea mfano mtu anaponunua chombo cha moto kutumia namba hiyo ya utambulisho kupata leseni ya udereva au anaponunua chombo cha moto kutoka nje ya nchi ili ukifanyie usajili lazima uwe na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN)


Ashura Jumapili mwandishi wa habari gazeti la majira alishauri mamlaka hiyo kufuatilia hata wafanyabiashara waliopo nje ya mji ili nao waweze kulipa kodi kwani unakuta baadhi ya wafanyabiashara hao wanazo biashara kubwa hadi bidhaa nyingine ipo stoo lakini hawalipi kodi.


Ikumbukwe kuwa, TRA Kagera imekuwa ikikaa mara kwa mara na waandishi wa habari kwa lengo la kuwapa elimu ili nao wakaelimishe jamii inayowazunguka juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi hii.

Afisa elimu na mahusiano TRA Kagera Rwekaza Rwegoshora akitoa mada ya elimu kwa waandishi wa habari
Meneja msaidizi huduma kwa mlipa kodi mkoa wa Kagera Estomih Mossi akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na mamlaka hiyo

Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Kagera waliohudhuria mafunzo yaliyotolewa na mamlaka ya mapato Tanzania TRA

Sunday, October 13, 2024

HOSPITALI YA SHIFAA YAZINDUA KITUO CHA TIBA NA UTAFITI WA SARATANI DAR

 






Picha mbalimbali wakati Waziri wa Afya,  Jenista Mhagama alipozindua kituo cha tiba na utafiti wa saratani katika hospitali ya Shifaa iliyoko Kinondoni barabara ya Msese jijini Dar es Salaam Ijumaaa Tarehe 11 Oktoba 2024.
.......................................
Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amezindua Kituo cha Tiba na Utafiti wa Saratani cha Shifaa na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuongeza bajeti ya dawa za saratani kila mwaka kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani.


Waziri Mhagama aliyasema hayo Ijumaa jioni jijini Dar es Salaam wakati akizindua kituo hicho kilichopo kwenye hospitali ya Shifaa barabara ya Msese Kinondoni jijini Dar es Salaam.


Alisema wakati idadi ya wagonjwa ikiongezeka wagonjwa wengi wanaougua ugonjwa huo hawana uwezo wa kugharamia matibabu hivyo wanahitaji kusaidiwa.


Alisema kwa mwaka huu wa fedha pekee serikali imetenga shilingi bilioni 10 kwaajili ya kununua dawa za saratani na kwamba kila bajeti mpya kiasi hicho kitakuwa kikiongezeka.


Alisema uwepo wa kituo hicho utaongeza upatikanaji wa huduma muhimu sana za kiuchunguzi na kitabibu kwa matatizo yanayohusu ugonjwa wa saratani nchini.


Alisema saratani imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na takwimu za kila mwaka zinaonyesha kuwa na ongezeko na mwaka 2022 wagonjwa wapya wa saratani walikuwa 45,000.


“Wagonjwa wa saratani wasipowahi kupata matibabu inawasababishia vifo kwa hiyo unapokuwa na wagonjwa 45,000 nchi lazima iweke mipango ili kuokoa uhai wa wananchi hao kwa kupata tiba mapema,” alisema.


Alitaja saratani zinazoongoza kuwa ni saratani ya mlango wa kizazi inayochukua asilimia 24.2, saratani ya tezi dume inachukua asilimia 10.7, saratani ya matiti inayochukua asilimia 10, saratani ya koo inayochukua asilimia 7.9, saratani ya utumbo mpana inayochukua asilimia 4.9 ya aina zote  za saratani nchini.


Waziri Mhagama alisema saratani zote hizo zinachukua asilimia 42 ya idadi ya wagonjwa wote wanaougua saratani nchini na saratani zinazoathiri zaidi wanawake nchini ni ile ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.


“Ndiyo maana serikali imeamua kuchukua jitihada za kukinga wananchi wake dhidi ya saratani na pale ambapo mtu anapata saratani apate matibabu na leo Shifaa wanapounga mkono juhudi za serikali kuokoa wagonjwa wa saratani na kuwarejeshea furaha tunawashukuru sana,” alisema Mhagama.


 Alisema serikali imeendelea kutoa elimu na kufanya kampeni maalum za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa maradhi ya saratani na kupanua huduma za uchunguzi kwenye mikoa mbalimbali nchini.


Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na vituo vingi vya utoaji wa huduma hizo na hasa kwa wanawake na serikali imeimarisha huduma za uchunguzi a kimaabara na huduma za radiolojia kwa kuhakikisha inakuwa na mashine 85 za  CT SCAN za kutosha  na MRI.


Mkurugenzi Mtendaji wa  hospitali ya Shifaa, Bashir Haroon aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa inaofanya kwenye sekta ya afya.


Alisema hospitali ya Shifaa ni uwekezaji ambao umegharimu dola za Marekani milioni 60 kama jitihada za kuwawezesha wananchi kupata matibabu bora yanayokwenda na wakati.


“Ujenzi wa hospitali hii umefanywa kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika sekta ya afya na tunafurahi kuona maboresho makubwa yakiendelea kwenye sekta ya afya na navipongeza vituo binafsi vya afya kwa kazi kubwa wanayofanya,” alisema


Haroon alisema ugonjwa wa saratani umekuwa tatizo kubwa sana duniani na hapa Tanzania na ndiyo sababu yeye aliona umuhimu wa kuanzisha kituo cha tiba ya saratani ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wagonjwa wa Tanzania wanaokwenda India kutibiwa.