Na Omary Mngindo, Kidogozero.
WANAFUNZI wanaioishi katika mazingira hatarishi wakilelewa kwenye kituo cha Faraja, Kijiji cha Kidogozero Kata ya Vigwaza Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameishukuru Lion Club (Host) ya jijini Dar esa Salaam kwa kuwapatia misaada.
Shukrani hizo zimetolewa na wanafunzi Enjo Frank na Faraji Ramadhani baada ya kupokea vifaa vya shule na vyakula vyenye shilingi milioni 1.6, vikikabidhiwa na Rais Mahmood Rajvan, Mountazir Barwani na viongozi wenzao walipofika kijijini hapo kuwafariji watoto hao 41.
"Namshukuru Mwenyeezimungu kwani sikutegemea kupata msaada kama huu, utakaonisaidia katika masomo yangu wakati shule ikifunguliwa, mungu awasaidie na awaongezee pale mlipopunguza," alisema Enjo.
Nae Ramadhani alieleza kwamba kwa msaada huo wa begi, madaftari pamoja na peni vimempatia chachu ya kuendelea na masomo, huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika elimu yake ya Sekondari.
Kwa upande wao wazazi Mohamed Ally aliishukuru Lion huku akiwahimiza wanafunzi kuongeza bidii katika kusoma, na kwamba zawadi hizo ziwe chachu ya kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Evat Mapunda alielezea shukrani zake kwa uongozi huo kwa msaada mkubwa ambao wamewapatia watoto hao, na kuwa kijana wake amepoteza wazazi wote wawili hivyo yupo mikononi mwake hivyo msaada huo umekuwa faraja kubwa kwake.
"Kijana wangu hana baba hana mama mimi ndio anayenitegemea hivyo vifaa hivi vimenigomboa, muendelee na moyo huo wa kusaidia watoto kama hawa hasanteni sana," alimalizia Evat.
Katibu wa kikundi hicho Zena Mindu mbali ya kuwashukuru Lion, pia ameuomba uongozi huo kuendelea kukisaidia kikundi hicho kinacholea watoto hao hao, huku wakiwa hawana msaada wowote.
"Nawashukuru sana mlikuja Ruvu Darajani kukabidhi Matenki ya maji pamoja na vifaa vya shule, nami mlinikabidhi msaada, leo mmekuja hukuhuku Kidogozero ambako ndio tunakosihi na kutusaidia vifaa vya shule pamoja na vyakula, tunawashukuru sana," alisema Mindu.
Akizungumza kwa niaba ya Diwani Mussa Gama, Katibu wake Amos Mwakamale alitoa shukrani kwa Lion huku akiwataka wazazi waaoishi na watoto hao kuhakikisha shule ziapofunguliwa wote wanakwenda kusoma.
Mwenyekiti wa Kijiji Said Sango alimshukuru Barwani na viongozi wote, kwa kuendeleza kazi aliyoianza kijana wake Mouhsin Barwani aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo miaka mitano iliyopita.
"Nimefurahi kuona mnaendelea kutusaidia Kata ya Vigwaza, tunaona kama bado tupo na Mohsin Barwani aliyekuwa diwani wetu miaka mitano iliyopita, hapa Kidogozero kuna tenki alilolitoa shuleni mpaka leo linatumika, tunawashukuru sana," alisema Sango.
Akitoa neno kwa wanafunzi hao, Barwani aliwataka wanfunzi hao kukazania masomo, na kwamba taifa linawategemea katika kulitumikia miaka ijayo panapouhai, hivyo wakazanie elimu.
No comments:
Post a Comment