Na
WAF- DOM
MGANGA
Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amebainisha kuwa asilimia 26 ya watu
wazima wenye umri wa miaka kati ya 25 hadi 64 wana shinikizo la juu la damu, hali inayosababishwa na
mtindo wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula vya mafuta mengi, matumizi ya pombe
kupita kiasi na kutofanya mazoezi.
Dkt.
Sichalwe amebainisha hayo leo Aprili 13, 2022 wakati akifungua Mradi wa Healthy
Heart Africa tukio lililofanyika katika zahanati ya Makole Jijini Dodoma.
“Tumefanya
utafiti mwaka 2012 na kukagundua kwamba asilimia 26 ya watu wazima kati ya
miaka 25 na 64 wana shinikizo la juu la damu na tatizo hili linatarajia
kuongezeka kwa kiasi kikubwa endapo hatutachukua hatua.” Amesema Dkt. Sichalwe.
Aliendelea
kusema kuwa, tafiti zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 75% ya Wagonjwa hao
wenye shinikizo la juu la damu hawatumii tiba yoyote, huku akiweka wazi kuwa
zaidi ya robo tatu kati yao hawajui kama wana shinikizo la juu la damu.
Aidha,
Dkt. Sichalwe amesema kuwa, taarifa za utafiti zilizofanywa katika baadhi ya
hospitali za Rufaa zimebaini kuwa, wastani wa watu 19 katika kila watu 100
wanaolazwa kwa tatizo la shinikizo la juu la damu hufariki Dunia.
Sambamba
na hilo, ameweka wazi kuwa, hali ni mbaya zaidi kwa wagonjwa wa kiharusi,
ambapo katika kila watu 100 wanaolazwa, watu 39 wanafariki kwa tatizo hilo la
shinikizo la juu la damu, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea
kutoa elimu na kuhamasisha jamii ili kuongeza nguvu za kupambano dhidi ya
ugonjwa huo.
Mbali
na hayo Dkt. Sichalwe ameendelea kusisitiza juu ya kuzingatia utoaji huduma za
afya kwa kufuata miongozo, huku akisisitiza weledi na umahiri wakati wa kutoa
huduma ili kuepusha malalamiko yanayoweza kuzuilika kutoka kwa wananchi.
Naye,
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amewashukuru Wadau wa
PATH kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa
yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu.
Amesema,
Ukuaji wa miji, Maendeleo ya Sayansi na teknolojia na mabadiliko ya mtindo wa
maisha kwa kiasi kikubwa yanaendana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza
ikiwemo ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, hivyo kuwaomba Wadau kuendelea
kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo hasa katika
miji inayoendelea kwa kasi ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na
Mbeya.
Mpango
wa Healthy Heart Africa (HHA) ni mpango wa miaka miwili unaoratibiwa na
AstraZeneca katika Mkoa wa Dodoma (HF 13) na Dar es salaam (HF 22), na
unajumuisha jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 35 (zahanati 25 na
hospitali 10). Mradi huu unashughulikia magonjwa ya moyo na mishipa, haswa
Shinikizo la damu (HTN).