Thursday, October 5, 2023

MAKAMU WA RAIS AZITAKA NGO's KUCHUNGA MAADILI NA TAMADUNI ZA KITANZANIA.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NGO’s) kuwajibika kutunza na kulinda maadili kwa kuheshimu mila, desturi na tamaduni za kitanzania wakati wa utekelezaji wa programu mbalimbali.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifunga Jukwaa la Tatu la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) llililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Aidha amewataka kuzingatia sheria za nchi na kufuata miongozo mbalimbali inayoratibu shughuli za mashirika hayo.

 

Makamu wa Rais ametoa rai kwa NGO’s kuhakikisha hazitumiki kuharibu maadili ya Tanzania kwa kutekeleza ajenda binafsi zisizofaa. Ametoa wito kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii kufanya uchambuzi makini wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuishauri serikali ipasavyo juu mwenendo na ufanisi wa mashirika hayo.

 

Pia Makamu wa Rais amesema suala la mabadiliko ya tabianchi linapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika. 



Amesema serikali Serikali ingependa kuona ushiriki zaidi wa NGOs katika utoaji elimu na hamasa kuhusu uhifadhi wa mazingira, udhibiti wa majanga na maisha endelevu, utunzaji wa misitu na uoto wa asili na kuchangia katika utengenezaji au uboreshaji wa sera mbalimbali. 



Aidha amesema mashirika hayo yana nafasi ya kubuni programu muhimu kama ukusanyaji na urejelezaji taka, biashara ya kaboni, uanzishwaji na utunzaji wa vitalu vya miti na usambazaji wa miche pamoja na usafi wa mazingira katika maeneo maalum.

 

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu zaidi. 



Ametaja miongoni mwa hatua ambazo Serikali imechukua katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ni pamoja na kuandaliwa kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara (2020), Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020), Kitabu cha Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa (2020/2021/2022), pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2022/23 – 2026/27). 



Hatua nyingine ni uanzishwaji wa madawati ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika Wizara za Kisekta na Mfumo wa Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambao imezinduliwa.



Kwa Upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima amesema NGO’s zimekuwa zikiunga mkono jitihada za serikali kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali ikiwemo miradi ya afya, elimu, mazingira, kilimo , maji, utawala bora, nishati na uwezaji wa jamii.



Ameongeza kwamba utekelezaji wa miradi hiyo umechangia kuboresha utoaji huduma, kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya serikali na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Dkt. Gwajima amesema Wizara itaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa NGO’s ili ziweze kuisadia jamii kwa kuzingatia mipango, mikakati na vipaumbele vya taifa.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Dkt. Liliani Badi ameiomba serikali kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo upatikanaji wa vibali kwaajili ya utekelezaji wamiradi na afua mbalimbali katika mikoa na halmashauri mbalimbali, vigezo vya upatikanaji wa misamaha ya kodi pamoja changamoto ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa kutozingatia utekelezaji wa takwa la kisheria la kuyajengea uwezo mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani ya nchi.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

05 Oktoba 2023

Dodoma. 

CHONGOLO: MAWAZIRI 3 KUHUSIKA FIDIA MRADI WA UMEME TABORA - KATAVI

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema atakutana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kutatua changamoto ya malipo ya fidia ya wananchi ambao ardhi yao imechukuliwa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Msongo wa Umeme kutoka Tabora hadi Katavi. 


Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amesema hayo leo Oktoba 5, 2023, wakati akizungumza na wananchi wa Inyonga, wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi, kuhusu mradi huo wa msongo wa umeme ambao utauwezesha mkoa huo sasa kuunganishwa katika gridi ya taifa, hivyo kumaliza kabisa changamoto ya nishati hiyo katika maeneo hayo. 


“Nikirudi Dar es Salaam nitakaa na pande zote zinazohusiana na ulipaji fidia wakiwemo Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi pamoja na wadau wengine ili watuambie wanaendaje na nini kifanyike kusukuma suala la fidia ili walipwe haraka.


Ndugu Chongolo amewahikishia wananchi wa Mkoa wa Katavi kuwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, kuunganisha Mkoa wa Katavi kwenye gridi ya taifa, ni mojawapo ya vipaumbele vya muhimu kwa Serikali. 


Chongolo ambaye yupo katika mkoa huo kwa ziara ya kuhamaisha uhai wa Chama, kukagua utekelezaji wa Ilani pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia majawabu, amesema Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.


“Na huu mradi sio mradi tu bali ni mradi wenye lengo mahususi la kutafuta majawabu kwa wananchi wa Katavi lakini pia kuinua shughuli za uchumi wao na wakazi wa jirani kama Sikonge na maeneo mengine.


“Mmeeleza vizuri uwezo wa kituo hapa ni megawati 1.4  na mahitaji sasa hivi yaweza kuwa yamefika megawati mbili lakini ukipeleka Majimoto kuna viwanda zaidi ya 20 au 30 vya mpunga vile viwanda vyote vinahitaji umeme.


“Ukipiga hesabu utakuta Majimoto nao wanahitaji megawati mbili mpaka tatu, kwa hiyo zinahitajika karibia megawati tano kwa wilaya  ya Mlele. Ukienda Mpanda shughuli zao zinaunganisha mpaka Kalema na kalema tuna bandari." Amesema.


Ameongeza ili kubadilisha kwenda kwenye uhalisia ni kutekeleza huo mradi huku akitumia nafasi hiyo kuzungumzia suala la fidia kwa watakaopitisha mradi huo.


“Nikirudi Dar es Salaam nitakaa na pande zote zinazohusiana na ulipaji fidia wakiwemo Wizara ya Nishati,Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi pamoja na wadau wengine ili watuambie wanaendaje na nini kifanyike kusukuma suala la fidia ili walipwe haraka.


Ameongeza fidia ikishalipwa itabaki kusubiri ujenzi wa laini ya umeme na kushauri watekelezaji wa mradi huo kuanzia shughuli za za awali za utekelezaji wa mradi huo kwa kuandaa mazingira.


“Wakati huu ungekuwa wakati muafaka wa kuanza kujenga nguzo kwenye maeneo yale yenye majimaji ili wakati wa masika ujenzi usimame maeneo hayo.Tunaomba mradi huu uangaliwe kwa uzito wake.


“Tukifungua na kuleta umeme kwa wananchi wa Katavi naamini mchango wao katika kukuza uchumi wa nchi hii utakwenda juu kwani kwa sasa hata ujenzi wa viwanda vikiwemo vya kuchakata tumbaku na migodi ya madini, umesimama kwasababu ya changamoto ya umeme,” amesema Ndugu Chongolo.







RAIS SAMIA AMEIBEBA KWA DHATI AJENDA YA MATUMIZI NISHATI MBADALA – NAIBU WAZIRI KAPINGA

 

Lilian Lundo, Veronica Simba na Zuena Msuya - Songea


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameibeba kwa dhati ajenda ya matumizi ya nishati mbadala kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.


Mhe. Kapinga amesema hayo leo Oktoba 5, 2023 wakati wa Baraza Maalum la Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma, sanjari na ugawaji wa majiko/mitungi ya gesi yaliyotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).


“Ninyi nyote mnafahamu ajenda ya Mhe. Rais kuhusiana na umuhimu wa nishati mbadala, tunafahamu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mazingira kwa ujumla. Hii ni ajenda ambayo Mhe. Rais ameibeba kwa dhati kabisa kuhakikisha tunaanza mchakato wa kuelimisha Watanzania ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira, na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira,” amesema Mhe. Kapinga.


Naibu Waziri Kapinga ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma amewataka vijana kushirikiana na wanawake, wazee na makundi mengine katika kuhakikisha wanapunguza changamoto za kimazingira kwa matumizi ya nishati mbadala.


“Wengi wanadhani ajenda hii ya nishati mbadala ni kwa ajili ya akina mama tu, lakini wote tunafahamu nguvu na mchango wa vijana kwenye masuala ya mabadiliko chanya. Kwa hiyo ajenda hii ni lazima twende nayo pamoja wanawake, vijana, wazee na kila kundi kwenye jamii. Ndiyo maana nikaona busara kushirikisha Baraza la Mkoa kwa sababu ninyi ndio viongozi kwenye Wilaya zenu,” amesema Mhe. Kapinga.


Akifafanua, amesema kuwa ajenda ya matumizi ya nishati mbadala ni ya Serikali ya Awamu ya Sita na inatakiwa kuungwa mkono na wananchi wote ili kuweza kuboresha mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea hivi sasa duniani kote.


Kapinga amesema ni wakati wa vijana kusaidia katika anjenda mbalimbali zenye manufaa ya taifa na kwamba ajenda ya nishati mbadala ikibebwa na vijana inaweza kwenda kwa kasi katika kusaidia kupunguza changamoto za uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii.


Aidha, ameongeza kuwa wakati huu ambapo REA wanaendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati mbadala, Mhe. Rais ametoa mitungi ya gesi kwa Wabunge wote ili iende kwenye maeneo yote, na majimbo yote ili kuhamasisha umuhimu wa nishati mbadala. 


Awali, akiwasilisha Mada kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA amesema Wakala hiyo inaendeshwa kwa Mipango Mikuu mitatu ambayo ni Mpango wa Sera ya Taifa wa Upelekaji Nishati Vijijini (Rural Energy Master Plan), Mpango wa usambazaji wa huduma ya umeme vijijini (Rural Electrification Master Plan) pamoja na Mpango wa Nishati safi za kupikia.


Kuhusu Mpango wa nishati safi ya kupikia, Mhandisi Tarimo amesema umelenga kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo salama kwa mtumiaji na kwa mazingira, ubora, upatikanaji wake, gharama nafuu, rafiki kwa mazingira na iliyo endelevu.


Akizungumzia aina za nishati za kupikia na kiwango cha matumizi yake kwa hapa nchini, Mhandisi Tarimo amebainisha kuwa kuni inaongoza kwa asilimia 63. 5 ikifuatiwa na mkaa asilimia 26.2, gesi oevu asilimia 5.1, umeme asilimia 3 na asilimia 2.2 vyanzo vinginevyo.


Amesema, kutokana na matumizi makubwa ya mkaa na kuni, imechangia uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji miti. Pia, amesema athari nyingine ni za kiafya kwa watumiaji wa nishati hizo ambapo vifo zaidi ya 33,000 hutokea kwa mwaka kutokana na kuvuta hewa ya ukaa. Vilevile, kiuchumi amesema matumizi ya nishati zisizo salama yanachelewesha maendeleo ya shughuli za kiuchumi.


Kufuatia hali hiyo, amesema Serikali imeweka mikakati ya makusudi katika kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala hivyo akatoa wito kwa wananchi wanaopata elimu hiyo kuifikisha kwa wengine.


Amewasihi wananchi kubadili mitazamo hasi dhidi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo imani kwa baadhi ya watu kwamba chakula huwa kitamu zaidi kikipikwa kwa kutumia mkaa au kuni kuliko kikipikwa katika jiko la gesi au umeme.


Mhandisi Tarimo ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.


Naibu Waziri Kapinga yuko katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati pamoja na kuzungumza na wananchi. 


NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUSHIRIKIANA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA ONGEZEKO LA IDADI YA WATU

 

Mkurugenzi wa Milki wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi Upendo Matotola(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Fedha wa NHC Bw. Adolph Kasegenya(kulia) na Meneja Habari na Ubusiano wa NHC Bw. Muungano Saguya Jijini Algiers wanaposhiriki mkutano wa Taasisi ya Makazi Barani Afrika.
..................................

Na Mwandishi Wetu, Algiers 

Wakuu wa nchi za kiafrika wametakiwa kuweka msukumo wa pamoja ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu Barani Afrika.


Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Algeria Mhe. Aymen Ben Abdirrahmane alipofungua Mkutano wa dharula wa Taasisi inayoshughulikia makazi Barani Afrika ya Shelter Afrique unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa CIC Abdelatif Rahal Jijini Algiers.


Amesema kuwa hivi sasa Bara la Afrika lina idadi ya watu inayofikia bilioni 1.4 na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi hiyo itafikia watu bilioni 2.5 na hii itakuwa ni asilimia 25 ya idadi ya watu wa dunia.

Alisema kuwa hii inaleta mahitaji makubwa ya makazi bora na huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na miundombinu hivyo alisema kuwa viongozi wa Bara la Afrika wanahitaji kushirikiana vilivyo ili kukabili changamoto za ongezeko hili ikiwemo kukosekana kwa makazi bora. 

Alibainisha kuwa inatarajiwa kuwa mabadiliko ya tabianchi katika nchi nyingi za bara la Afrika yatasababisha mafuriko na ukame wa kupindukia na kuathiri maisha ya wananchi wa bara hili. 

Alitumia nafasi hiyo kuuelekeza Mkutano huo unaohudhuriwa na nchi 44 za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, namna pekee ya kukabiliana na hali hiyo ni kila nchi kuwekeza katika upatikanaji wa makazi bora, kuwa na miundombinu ya uhakika na kusaidia upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu kwa watu wa kipato cha chini. 

Alizitahadharisha nchi za kiafrika kuwa kama hazitafanyika jitihada za kuondoa makazi holela na kuwezesha upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu barani Afrika, maisha ya watu yatakuwa mabaya na kuongeza umaskini. 

Alisema kuwa jitihada zinazohitajika kufanyika ni pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha na gharama nafuu za ujenzi na ununuzi wa nyumba, kwa kutumia malighafi za ujenzi zinazopatikana Barani Afrika, kuwa na teknolojia inayosaidia ujenzi wa nyumba nyingi za gharama nafuu na kupunguza riba ya mikopo katika benki. 

Aliendelea kwa kusema kuwa, ni lazima nchi za Afrika kuwekeza katika ujenzi wa nyumba katika vijiji ili kupunguza idadi ya watu wanaohamia mijini ambao wanaongeza mahitaji makubwa ya huduma za kijamii na miundombinu imara. 

Katika Mkutano huo unaoendelea leo Jijini Algiers, Mtendaji Mkuu wa Shelter Afrique Bw. Thierno-Habib Hann amewasilisha mapendekezo ya Bodi ya Taasisi hiyo ya Makazi Barani Afrika iliyoleta mabadiliko makubwa ya kimfumo ambayo inaanzisha Benki ya Maendeleo ya Shelter Afrique itakayosaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa nchi wanachama na kuongeza uwekezaji zaidi katika teknolojia na miundombinu katika miji ili kuwa na miji bora, salama na kuboresha maisha ya wananchi wa bara la Afrika.


Nchi 15 za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania ndizo zitakazoridhia kwanza mabadiliko hayo kwa kuwa zina hisa na zinakubalika katika muundo wa sasa wa Taasisi hiyo yenye nchi wanachama 44 wa Afrika. 



Wajumbe kutoka Tanzania wakipitia ajenda mbalimbali  zilizowasilishwakwkwenye Mkutano wa Taasisi ya Makazi Afrika unaoendelea Jijini Algiers akiwemo Bw. Deogratious Kalimenzi, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji anayemuwakilisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

SOMA MAGAZETI YA LEO TAREHE 05 OKTOBA 2023.