Monday, February 24, 2025

WAZIRI KIKWETE KUFANYA ZIARA YA SIKU TATU MKOANI SONGWE.

 

Anatarajiwa kukagua na Kuzindua Miradi ya Maendeleo  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu -Mhe. Ridhiwani Kikwete Februari 23, 2025 amewasili mkoani Songwe kwa lengo la ziara ya  kukagua miradi ya Maendeleo ikiwemo ya sekta  ya Elimu, Afya na Miundombinu   kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya wananchi .


Mhe. Waziri Kikwete anatarajiwa kukagua na kuweka Mawe ya msingi katika miradi hiyo ambayo inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 700 katika Halmashauri zote za mkoa huo.


Mara baada ya kuwasili katika  mkoa huo , Waziri Kikwete alipokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Ndg. Daniel Chongolo ambaye alimpa hali ya maendeleo ya Mkoa huo na maandalizi ambayo yameshafikiwa kwa ajili ya ziara hiyo.


Vile vile Mhe.  Kikwete anatarajiwa pia kukagua Maendeleo ya Kituo cha Vijana cha Sasanda wilayani   Songwe ambapo atakagua  mradi wa Shamba la vijana lililopo kituo hicho.


 Mhe Waziri Kikwete ameambatana  na watendaji mbalimbali ambapo amemhakikishia Mkuu wa mkoa huo  kuwa timu yake ipo tayari kwa ajili ya kazi iliyowaleta.







Saturday, January 4, 2025

MRADI WA MAJIKO YA GESI YA RUZUKU WATUA LINDI

 







NA HADIJA OMARY,  LINDI.


Ili kufikia azma ya Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati kupikia wakala wa  umeme  vijijini (REA) imekuja na program ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku


Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya Leo January 3, 2025 alipokuwa akimtambulisha mtoa huduma hiyo Katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, 


Amesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited kwa ajili ya kutekeleza mradi wa shilingi milioni 317.3 wa kusambaza majiko ya gesi 16,275 (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% sawa na shilingi 19,500 kwa jiko katika maeneo ya vijijini ndani ya Mkoa huo


Amesema Katika program hiyo kwa Mkoa huo wa Lindi Jumla ya Kaya 16,275 Katika Maeneo tofauti ya vijijini linatarajiwa kunufaika huku akibainisha  kuwa lengo la mradi huo ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za Nishati Safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti. 


"Mradi huu unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya, pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza Mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi," alifafanua Mhandisi Yesaya.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa majiko ya ruzuku ambao  utaongeza matumizi ya nishati safi kupikia hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini. 


Pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujaza mitungi pale inapoishiwa gesi ili kuendelea kutumia huku akimuelekeza Mtoa huduma (Taifa Gas) kuhakikisha anakuwa na mawakala kwenye kila kata na vijiji ili kumrahishia mwananchi kubadilisha mtungi pale gesi inapomalizika.


"Ili kuwa na uendelevu wa matumizi ya gesi kupikia, natoa wito kwa Taifa Gas kuwa na mawakala ili kumrahishia mwananchi; tusikubali kumpoteza mtu kurudi kwenye kuni na mkaa kwa sababu ya kukosa mahala pa kubadili mtungi," alielekeza. 


Kwa upande wake, Meneja   mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Kusini, Hawa Omari amesema kuwa wanejipanga vyema kufika kwenye maeneo yote Mkoani hapo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi watakaonunua majiko hayo kabla ya kutumia.


Wednesday, January 1, 2025

NANI ATAKUWA MRITHI WA KINANA CCM?

 

Na Mwandishi Wetu.



NANI atakuwa makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara?


Ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na makada wa CCM na hata wafuatiliaji wa karibu wa siasa nchini, hasa mwaka huu ambao Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu Rais, Wabunge na Madiwani.


Jibu la swali hilo linatarajiwa kupatikana kupitia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwezi huu, lakini kitendawili cha nani atakuwa Makamu Mwenyekiti atakitegua Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Makamu mwenyekiti anayetakiwa kwa wakati huu ni yule ambaye atakuja kufanya kazi ya kuivusha salama CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Anahitajika Makamu Mwenyekiti mwenye uwezo wa kukabili jukwaa na hadhira yake. Makamu Mwenyekiti asiye bubu wala mbabe, asiye mwenye ‘makando kando’, asiyekuwa mbinafsi, mchoyo na ambaye akisema atasikilizwa na kuaminiwa na wanachama na viongozi wenzake wa chama hicho tawala.


Pamoja na majukumu mengine, makamu mwenyekiti atasimamia maadili ndani ya CCM. Ilivyokuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa dola, suala la wanachama kuzingatia maadili ni jambo la msingi kabisa maana ulegevu wowote katika hili ni kupata wagombea ambao hawana maadili. 


Kwa jinsi mambo yana vyokwenda CCM, inahitaji makamu mwenyekiti mwenye ushawishi kwa umma, mwenye nguvu na mvuto ambaye hatoyumbishwa kwa namna yoyote ile iwe Abdallah Bulembo ndani ya CCM au hata nje ya chama hicho.


Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, katika hotuba aliyotoa mwa ka 2005 Chimwaga mkoani Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuteua wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, alitaja sifa 13 anazostahili kuwa nazo mtu anayetaka kushika nafasi hiyo.


Pamoja na nyingine nyingi, Mkapa aliwataka wanaCCM wasichague mtu kwa kumpenda, bali achaguliwe kwa sifa. 


Mkapa akatoa mfano wa bangili akisema hata ikiwa nzuri kiasi gani, kama inabana kwenye mkono haifai.


Je, hao wanaotajwa au kujitaja kuwa wanaweza kushika wadhifa wa makamu mwenyekiti CCM Bara sifa yao ni kama bangili yenye kubana mkononi au isiyo bana? 


Kwa vyovyote vile, mtu anayefaa kwa nafasi hiyo asiwe mgeni ndani ya CCM, bali awe mwenye kuvifahamu vikao vya chama, katiba, kanuni na miongozo huku akizingatia sera na hali ya kisiasa.


Hadi sasa kuna watu kadhaa wanatajwa na ku zungumzwa kuwa huenda wana sifa za kuwa makamu mwenyekiti wa CCM Bara kurithi ‘viatu’ vya Komredi Abdulrahman Kinana aliye jiuzulu wadhifa huo mwaka jana.


Miongoni mwa wanaota jwa ni William Lukuvi, Abdulrahman Juma, Mizengo Pinda, Abdallah Bulembo, Paul Kimiti, Dk Asha–Rose Migiro, Anne Makinda, na Stephen Wassira.


Makala haya yanaangazia wagombea hao ambao na wengine wanaotajwa kuwa na sifa za kumrithi Komredi Kinana aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.


Wa kwanza kumuangazia ni kada wa siku nyingi, Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo.

 

Kwa wasiomfahamu Bulembo ni kuwa, kada huyo ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM. Amewahi kuwa Mbunge, Mjumbe wa NEC, Kamati Kuu na kwa sasa ni Mshauri wa Rais Mambo ya Siasa na Jamii.


Mwaka 2015, Bulembo alizunguka nchi nzima kumnadi aliyekuwa Mgombea Urais wa wakati huo, Dk John Magufuli akiwa Meneja wa Kampeni. 

Bulembo ni kada wa CCM mwenye msimamo thabiti, asiyekubali kuburuzwa na hababaishwi na jambo. 


Ilihitaji moyo na ustahamilivu kuweza kuwa meneja wa kampeni wa mwanasiasa aina ya Magufuli, lakini kwa busara zake na uwezo wake wa kisiasa, Bulembo aliweza kumnadi vyema Rais Magufuli na kufanikisha ushindi wa kishindo wa CCM.


Mbali na uzoefu wa kisiasa na utumishi ndani ya CCM, Bulembo anaonekana kuwa na sifa nyingine ambayo pengine wengine hawana. 


Sifa kimsingi, ndiyo inayomfanya awe anatajwa na makada wa CCM kuweza kumrithi Komredi Kinana.


Sifa ya ziada ya Bulembo ni kuwa mwanasiasa anayewakilisha mawazo ya rika tofauti ya wazee, kizazi kipya, umri wa kati na mtu anayeweza kuwa kiungo cha wanasiasa wazee na vijana ndani ya CCM na hata katika vyama vingine vya siasa.


 Je, ni hulka yake ya kujichanganya na watu wa rika tofauti? Ni haiba yake ya utu uzima, busara mpenda watu na aliye tayari kujitolea ikibidi hata vitu vyake binafsi?


Ni upeo wake mkubwa wa kuona mambo? Ni hoja zake za kisasa? Ni uzalendo wake? Ni upungufu walionayo wanasiasa wengine wanaotajwa kufaa katika nafasi hiyo? Ni kitu gani hasa? Wana CCM wanapaswa kuyatafutia jawabu maswali haya.


Bulembo mwenye umri wa miaka 63, bado anabeba matumaini ya zama za sasa.


Hajapitwa na wakati. Ikiwa zama za leo ni za vijana na watu wa umri wa kati. Wapigakura wengi ni vijana na hadhira ya kisiasa imebadilika sana, hivyo anahitajika makamu mwenyekiti wa CCM anayeweza kuyanadi matarajio ya vijana katika ulingo wa kisiasa na zaidi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Bulembo ni muumini wa dhati kabisa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mapinduzi ya Zanzibar, ni mzalendo na ni mwanasiasa mwenye siasa za kati.


Anaonekana pia kuwa mwanafalsafa ambaye amegeuka kuwa tumaini la mabadiliko chanya ndani ya CCM. Anao uwezo wa kusaidia CCM kukabili changamoto za kisiasa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Changamoto kubwa inayomkabili Bulembo ni misimamo yake isiyoyumba kwani ni mtu ambaye habadiliki kama kinyonga katika jambo mlilokubaliana. 


Kwa matamshi mengine, Bulembo si kigeugeu, si ndumi lakuwili, bali ni mwenye msimamo thabiti kwa matendo na maneno.



Wiki ijayo tutaendelea kuwachambua makada wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara. Itaendelea