Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo limepokea na kupitisha bajeti ya shilingi Bilioni 38,982,000,000.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku shilingi Bilioni 6,482,058,127.00 ikitarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani na shilingi 32,496,016,000.00 ruzuku kutoka Serikali kuu.
Bajeti hiyo imepitishwa Tarehe 30 Januari 2024 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, ambae pia ni Diwani wa Kata ya Nianjema, Abdul Pyallah amesema ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji isimamie kikamilifu mikakati ya ukusanyaji mapato.
Akizungumza katika Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mhe. Mohamed Usinga, amemtaka Mkurugemzi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wakuu wa idara ambao watakamilisha miradi huku ikiwa na madeni.
Usinga alisema ipo tabia ya baadhi ya wakuu wa idara kutekeleza Miradi huku wakiwa wanakopa kwa wazabuni na kuisababishia Halmashauri kuwa na madeni yasiyo ya lazima.
Alisema ni Mkuu wa idara atekeleze Mradi wake kwa mujibu wa bajeti ilivyo na si vinginevyo.
Alisisitiza kwa kisema kuwa, Mkuu wa idara atakasababisha deni kwenye Mradi achukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka.
Nae Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo amesema atahakikisha anasimamia bajeti hiyo ili kufikia malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji pamoja na utekelezaji wa Miradi mbalimbali.