Mgeni
rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)
ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul
akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu Desemba Mosi, kulia kwake ni Mkuu wa
TaSUBa, Dkt. Herbert Makoye.
........................................
Na
Mwandishi Wetu Bagamoyo
Naibu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameupongeza uongozi
wa Taasisi ya Sanaa na utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa usimamizi mzuri wa fedha
zinazoletwa katika taasisi hiyo kwa kuzitumia vyema kuendana na mahitaji ya
taasisi ili kuifanya taasisi kufikia malengo yake.
Mbali na
hilo, pia ameipongeza TaSUBa kwa ongezeko kubwa la udahili wa Wanafunzi katika
chuo hicho hata kufikia hatua ya kuweka historia ya kudahili idadi kubwa ya
wanafunzi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Naibu
Waziri Gekul ametoa pongezi hizo leo Desemba Mosi, 2022 akiwa ni mgeni rasmi
katika mahafali ya 33 ya TaSUBa yaliyofanyika katika kampasi ya TaSUBa Bagamoyo
mkoani Pwani na kusisitiza kuwa, taaluma ya utamaduni na sanaa inayotolewa
chuoni hapo ni taaluma muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote duniani.
Kufuatia
hilo naibu waziri Gekul amebainisha kuwa, serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona wazi umuhimu wa taaluma
hiyo na hivyo kuanzisha sera maalum kusimamia.
“Taaluma
inayotolewa hapa chuoni ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote duniani,
ndio maana serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, imeweka sera
ya kusimamia sanaa na utamaduni kwa ujumla wake” alisema Naibu Waziri Gekul na
kuongeza.
“TaSUBa ni
taasisi ya pekee nchini kwetu na ukanda wa Afrika Mashariki inayotoa mafunzo ya
sanaa kwa ngazi ya stashahada na astashahada hivyo basi kuna umuhimu mkubwa wa
kuboresha taaluma hii ili iendane na mazingira ya sasa ya utandawazi”
Naibu
Waziri huyo ameutaka uongozi wa TaSUBa kuendeleza ubunifu zaidi kwa kuanzisha
kozi ambazo zitawavutia watu wengi kujiunga na chuo hicho.
Naye Mkuu
wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye amesema
kuwa, kwa miaka mitatu mfululizo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi chuoni
hapo na hiyo ni kutokana na jitihada mbalimbali zilizochuliwa na serikali ya
awamu ya sita, wadau pamoja na wao wenyewe kama taasisi.
Dkt.
Makoye amezitaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uamuzi wa serikali
kuwapangia wahitimu wa kidato cha nne moja kwa moja kujiunga na chuo hicho
pamoja na uhamishaji wa kila siku unaofanywa na TaSUBa pamoja na wadau wengine
katika kukitangaza chuo hiko.
Dkt.
Makoye ameongeza kuwa, kwa mwaka huu wa masomo pekee wameweka kudahili
wanafunzi 835 kutoka kwenye lengo la kudahili wanafunzi 700 na hivyo kuweka
historia ya udahili mkubwa chuoni hapo.
“Kumekuwa
na ongezeko kubwa la wahitimu na kwa mwaka huu tuna wahitimu 217. Aidha, mwaka
huu wa masomo 2022 /2023 tumeweza kudahili wanafunzi 835, lengo lilikuwa ni
kudahili wanafunzi 700. Hii ni rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu
kuanzishwa kwa TaSUBa” alisema Dkt. Makoye.
Kuhusu
maono ya TaSUBa kumiliki kituo chake cha redio na televisheni kwa ajili ya
kuwezesha wepesi wa utendaji kazi na mazingira wezeshi ya ufundishaji na
kujifunza Dkt. Makoye amesema.
“Endapo
tukipata fedha ambazo tuliziomba katika mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi
milioni 200 kwa ajili ununuzi wa vifaa vya kuanzisha na kusimika mitambo ya
televisheni na redio, basi TaSUBa itakwenda kumiliki televisheni na redio yake”
Awali
akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TaSUBa, Bw. George
Yambesi ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika taasisi
hiyo unalenga kupanua wigo zaidi wa vijana wa Kitanzania kupata mafunzo katika
tasnia za sanaa na utamaduni.
Aidha, Bw.
Yambesi ametumia fursa hiyo, kuishukuru serikali kwa uwezeshaji mkubwa
unaoendelea kutolewa kwa TaSUBa, uwezeshaji ambao umeleta matokeo chanya katika
taasisi hiyo ikiwemo kufanikisha uboreshaji wa miundombinu kujifunzia na
kufundishia kinyume na iliyokuwa awali ambao pia ameendelea kuisihi serikali
kuendelea na uwezeshaji huo ili malengo mahususi yaliyowekwa na TaSUBa yaweze
kutimiza na taasisi hiyo iweze kuleta tija kw mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa
kwa ujumla.
Nao
wahitimu wa chuo hicho kupitia risala yao iliyosomwa na Richard Julius Mtambo
wameeleza kuwa changamoto kubwa mbili zinazowakabili chuoni hapo ni ukosefu wa
basi la taasisi na hivyo kupata adha kubwa pale wanapopanga kufanya safari za
kimasomo, utalii, maonesho, mafunzo, mashindano na za kikazi.
Changamoto
nyingine ni ukosefu wa uzio kwenye taasisi hiyo jambo ambalo linahatarisha
usalama, kuwa kichocheo cha wizi na kupelekea kukosekana kwa faragha.
Taasisi ya
Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni kituo chenye ubora uliotukuka Afrika
Mashariki katika kutoa mafunzo ya sanaa za maonesho na ufundi ambapo majukumu
yake makubwa ni kuhudumia mahitaji ya nchi washirika wa jumuiya ya Afrika
Mashariki katika kutunza, kuhamasisha na kuendeleza sanaa za maonyesho na
ufundi ikiwa na majukumu makuu matatu ambayo ni utoa mafunzo,
kufanya utafiti katika masuala yanayohusu sanaa na utamaduni pamoja na
kutoa ushauri katika masuala yanayohusu sanaa na utamaduni.
Mgeni rasmi katika
mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akitoa hotuba
yake.
Mwenyekiti wa Bodi
ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Bw. George
Yambesi akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya taasisi hiyo ambayo
yamefanyika Desemba Mosi, 2022 katika kampasi ya TaSUBa Bagamoyo mkoani
Pwani. Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa ni Naibu Waziri wa Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul
Mkuu wa Taasisi ya
Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye akitoa hotuba yake wakati wa
mahafali ya 33 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Desemba Mosi, 2022 wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani.
Mgeni rasmi katika
mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akisaini kitabu
cha wageni mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo Desemba Mosi,
2022.
Wahitimu wa ngazi za
stashahada na astashahada katika tasnia za sanaa na utamaduni.