Sunday, December 18, 2022

HAKUNA MAENDELEO WALA AMANI BILA YA UHURU WA HABARI.-NAPE.

 No description available.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mnauye, amesema hakuna Maendeleo, hakuna amani na hakuna furaha katika jamii ikiwa hakuna uhuru wa habari katika jamii hiyo.

Waziri Nape amebainisha hayo wakati akifungua Kongamano la kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini lililofanyika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambalo limehudhuriwa na washiriki wasiopungua 1000 wa ndani na nje ya nchi.

Alisema uhuru wa habari ni muhimu katika maendeleo ya nchi kwani jamii inapaswa kupata habari za mambo mbalimbali ambazo serikali inatekeleza.

Alifafanua kuwa, ikiwa wananchi hawatapata habari ni wazi kuwa watakuwa hawaelewi mambo mengi yanayotekelezwa na serikali yao na hivyo kuwafanya kuwa na manung’uniko ambayo yataondoa furaha yao na kuwakosesha amani.

Aidha, Waziri Nape aliwapongeza wanahabari kwa kufanya kazi yao kwa weledi, juhudi na moyo wa kujituma kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zilizo sahihi na kwa wakati.

Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini uhuru wa habari hali iliyopelekea Rais Dkt. Samia kuiagiza wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuandaa mkutano mkubwa wa wanahabari ili kuangalia mambo mbalimbali yanahusu habari hapa nchini.

Waziri huyo wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema kwa umuhimu huo, serikali imeandaa kongamano hilo ambalo lengo ni kujadili namna ya kuboresha sekta ya habari ambapo majadiliano yanatakiwa kutoka na maazimio yatakayotekelezwa.

Aliendelea kusema kuwa, uhuru wa habari unapaswa kulindwa na sheria na wala sio utashi wa mtu ili kuufanya uhuru wa habari uwe ni endelevu kwa kiongozi yeyote atakaekuwepo madarakani.

Aliwahakikishai wanahabari kuwa ifikapo januari 2023 muswada wa marekebisho ya sheria ya habari utawasilishwa bungeni ili kupitisha baadhi ya vingele vya sheria kwa lengo la kutoa uhuru wa habari.

No description available.

 

No comments:

Post a Comment