Thursday, March 20, 2025

TCRA KUSHIRIKIANA NA TBN KUSADIA KUZALISHA MAUDHUI YENYE TIJA

 


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeahidi kufanyakazi na Mtandao wa Wana Blogu Tanzania (TBN), pamoja na vyama vingine vya waandishi wa habari ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe  19.Machi 2025 Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alipokutana na ujumbe wa TBN ofisini kwake, katika kikao cha kujadiliana changamoto mbalimbali zinazowakabili Bloga nchini.

“Sisi huwa tunapenda kufanya kazi na vyama ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao, badala ya kufanyakazi na mwaandishi mmoja mmoja…tunafurahi sana kufanyakazi na waandishi kupitia vyama vyao,” amesema Mhandisi Kisaka.

Mhandisi Kisaka amesema kuwa TCRA imefurahi kukutana na TBN kwa kuwa wanafahamu kuwa Bloga wanasehemu kubwa sana kwenye maudhui ya ndani, na hata kwenye usajili wa TCRA Bloga wanachukua nafasi kubwa sana katika maudhui ya mtandaoni.

“Kwa hiyo TBN mtakuwa silaha moja wapo nzuri sana yakutuwezesha sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano nchini, tunao simamia utangazaji pamoja na maudhui ya mtandaoni kuwa karibu na nyinyi na kuhakikisha maudhui ya mtandaoni yanaleta tija na maendeleo kwa wananchi,” amesema Mhandisi Kisaka.

Monday, March 17, 2025

MFUMO WA USAJILI WAANDISHI WA HABARI KIDIJITALI UPO MBIONI KUKAMILIKA- MSIGWA

 


Na Mwandishi Wetu, 

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa mfumo wa Usajili na utoaji wa vitambulisho vya kidigitali kwa Waandishi wa Habari nchi nzima - Journalists Accreditation & Registrations System (JARS).


Mfumo huo unaotengenezwa na chini ya Idara ya Habari (Maelezo) na Wataalamu wa Mifumo wa e- GA, unalenga kurahisisha, kuongeza uwazi na kuimarisha utendaji kazi wa waandishi wa Habari kwa kuwapatia huduma ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya kazi katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es salaam kupata huduma hiyo.


Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita wakati wa mkutano na waandishi wa habari tarehe 16 Machi, 2025 katika Bandari Kavu ya Kwala, mkoani Pwani.


Amebainisha kuwa Mfumo huo pamoja na mambo mengine utakuwa na uwezo wa kusajili, kuhakiki na kuhifadhi taarifa za waandishi wa habari wote nchini


"Mwandishi wa habari atakuwa na uwezo wa kujaza taarifa na kuweka mambo muhimu kama vile picha, mahali anapofanya kazi, taarifa za uraia wake n.k, na Mfumo utatoa alama za usalama ambazo mtu hawezi kughushi," amesema Bw. Msigwa na kuongeza;


"Kupitia mfumo huu Mwandishi wa Habari atakua na uwezo wa kuomba na kupata kitambulisho chake (physical ID). Mfumo una uwezo wa kuonesha taarifa kwenye ukurasa wa nyuma back-end ambazo zitahakikiwa na kutumiwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB kutoa kitambulisho (Press Card) kwa njia ya mtandao".


Amesisitiza kuwa Mfumo utakuwa na uwezo wa kumpatia mwandishi wa habari taarifa kabla ya muda wa kuisha matumizi ya kitambulisho chake (alert when the ID is about to expire) pia utamtumia ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi


Bw. Msigwa amesema kupitia mfumo huo Mwandishi anapoomba kitambulisho atapatiwa namba ya malipo “control Number” ya kulipia mtandaoni na akishalipia malipo yake yataonekana na kupitishwa na mamlaka husika (approved) na kwamba utakuwa na mwonekano wa aina mbili (madirisha) kwa ajili ya waandishi wa ndani na wa nje (International). 


"Mfumo utamwezesha Mwandishi wa Habari kupakia nyaraka muhimu kama vile vyeti vya taaluma kwa ajili ya uhakiki (VERIFICATION) na pia mfumo utapokea maombi ya waandishi wa nje ya nchi na wao kama ilivyo kwa wale wa ndani utawataka kupakia (Requirements) wakiwa wamekidhi vigezo ndipo hatua nyingine itafuata," amesema.


Mfumo utakuwa na uwezo wa kuhakiki taarifa za waandishi kwa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali kama GePG, NIDA, NECTA, Uhamiaji n.k kwa ajili ya malipo, uhakiki wa vyeti na taarifa (Verification).


Aidha, Bw. Msigwa amesema mfumo utakuwa na uwezo wa kuondoa wale wote waliokosa sifa/wasiohuisha taarifa zao pale wanapotakiwa kufanya hivyo, utamwezesha mtumiaji kuweka saini mahali panapohusika (Digital signature) pamoja na kuruhusu taarifa za kitaaluma na eneo la kazi kupatikana kwa njia ya msimbo papo (QR CODE).


"Huduma hii ya kupata vitambulisho vya kidigitali itapatikana kwa Waandishi wa habari wote watakaokuwa wamekidhi vigezo vya kitaaluma (Taaluma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma),"










Monday, February 24, 2025

WAZIRI KIKWETE KUFANYA ZIARA YA SIKU TATU MKOANI SONGWE.

 

Anatarajiwa kukagua na Kuzindua Miradi ya Maendeleo  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu -Mhe. Ridhiwani Kikwete Februari 23, 2025 amewasili mkoani Songwe kwa lengo la ziara ya  kukagua miradi ya Maendeleo ikiwemo ya sekta  ya Elimu, Afya na Miundombinu   kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya wananchi .


Mhe. Waziri Kikwete anatarajiwa kukagua na kuweka Mawe ya msingi katika miradi hiyo ambayo inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 700 katika Halmashauri zote za mkoa huo.


Mara baada ya kuwasili katika  mkoa huo , Waziri Kikwete alipokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Ndg. Daniel Chongolo ambaye alimpa hali ya maendeleo ya Mkoa huo na maandalizi ambayo yameshafikiwa kwa ajili ya ziara hiyo.


Vile vile Mhe.  Kikwete anatarajiwa pia kukagua Maendeleo ya Kituo cha Vijana cha Sasanda wilayani   Songwe ambapo atakagua  mradi wa Shamba la vijana lililopo kituo hicho.


 Mhe Waziri Kikwete ameambatana  na watendaji mbalimbali ambapo amemhakikishia Mkuu wa mkoa huo  kuwa timu yake ipo tayari kwa ajili ya kazi iliyowaleta.







Saturday, January 4, 2025

MRADI WA MAJIKO YA GESI YA RUZUKU WATUA LINDI

 







NA HADIJA OMARY,  LINDI.


Ili kufikia azma ya Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati kupikia wakala wa  umeme  vijijini (REA) imekuja na program ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku


Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya Leo January 3, 2025 alipokuwa akimtambulisha mtoa huduma hiyo Katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, 


Amesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited kwa ajili ya kutekeleza mradi wa shilingi milioni 317.3 wa kusambaza majiko ya gesi 16,275 (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% sawa na shilingi 19,500 kwa jiko katika maeneo ya vijijini ndani ya Mkoa huo


Amesema Katika program hiyo kwa Mkoa huo wa Lindi Jumla ya Kaya 16,275 Katika Maeneo tofauti ya vijijini linatarajiwa kunufaika huku akibainisha  kuwa lengo la mradi huo ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za Nishati Safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti. 


"Mradi huu unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya, pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza Mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi," alifafanua Mhandisi Yesaya.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa majiko ya ruzuku ambao  utaongeza matumizi ya nishati safi kupikia hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini. 


Pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujaza mitungi pale inapoishiwa gesi ili kuendelea kutumia huku akimuelekeza Mtoa huduma (Taifa Gas) kuhakikisha anakuwa na mawakala kwenye kila kata na vijiji ili kumrahishia mwananchi kubadilisha mtungi pale gesi inapomalizika.


"Ili kuwa na uendelevu wa matumizi ya gesi kupikia, natoa wito kwa Taifa Gas kuwa na mawakala ili kumrahishia mwananchi; tusikubali kumpoteza mtu kurudi kwenye kuni na mkaa kwa sababu ya kukosa mahala pa kubadili mtungi," alielekeza. 


Kwa upande wake, Meneja   mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Kusini, Hawa Omari amesema kuwa wanejipanga vyema kufika kwenye maeneo yote Mkoani hapo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi watakaonunua majiko hayo kabla ya kutumia.


Wednesday, January 1, 2025

NANI ATAKUWA MRITHI WA KINANA CCM?

 

Na Mwandishi Wetu.



NANI atakuwa makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara?


Ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na makada wa CCM na hata wafuatiliaji wa karibu wa siasa nchini, hasa mwaka huu ambao Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu Rais, Wabunge na Madiwani.


Jibu la swali hilo linatarajiwa kupatikana kupitia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwezi huu, lakini kitendawili cha nani atakuwa Makamu Mwenyekiti atakitegua Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Makamu mwenyekiti anayetakiwa kwa wakati huu ni yule ambaye atakuja kufanya kazi ya kuivusha salama CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Anahitajika Makamu Mwenyekiti mwenye uwezo wa kukabili jukwaa na hadhira yake. Makamu Mwenyekiti asiye bubu wala mbabe, asiye mwenye ‘makando kando’, asiyekuwa mbinafsi, mchoyo na ambaye akisema atasikilizwa na kuaminiwa na wanachama na viongozi wenzake wa chama hicho tawala.


Pamoja na majukumu mengine, makamu mwenyekiti atasimamia maadili ndani ya CCM. Ilivyokuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa dola, suala la wanachama kuzingatia maadili ni jambo la msingi kabisa maana ulegevu wowote katika hili ni kupata wagombea ambao hawana maadili. 


Kwa jinsi mambo yana vyokwenda CCM, inahitaji makamu mwenyekiti mwenye ushawishi kwa umma, mwenye nguvu na mvuto ambaye hatoyumbishwa kwa namna yoyote ile iwe Abdallah Bulembo ndani ya CCM au hata nje ya chama hicho.


Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, katika hotuba aliyotoa mwa ka 2005 Chimwaga mkoani Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuteua wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, alitaja sifa 13 anazostahili kuwa nazo mtu anayetaka kushika nafasi hiyo.


Pamoja na nyingine nyingi, Mkapa aliwataka wanaCCM wasichague mtu kwa kumpenda, bali achaguliwe kwa sifa. 


Mkapa akatoa mfano wa bangili akisema hata ikiwa nzuri kiasi gani, kama inabana kwenye mkono haifai.


Je, hao wanaotajwa au kujitaja kuwa wanaweza kushika wadhifa wa makamu mwenyekiti CCM Bara sifa yao ni kama bangili yenye kubana mkononi au isiyo bana? 


Kwa vyovyote vile, mtu anayefaa kwa nafasi hiyo asiwe mgeni ndani ya CCM, bali awe mwenye kuvifahamu vikao vya chama, katiba, kanuni na miongozo huku akizingatia sera na hali ya kisiasa.


Hadi sasa kuna watu kadhaa wanatajwa na ku zungumzwa kuwa huenda wana sifa za kuwa makamu mwenyekiti wa CCM Bara kurithi ‘viatu’ vya Komredi Abdulrahman Kinana aliye jiuzulu wadhifa huo mwaka jana.


Miongoni mwa wanaota jwa ni William Lukuvi, Abdulrahman Juma, Mizengo Pinda, Abdallah Bulembo, Paul Kimiti, Dk Asha–Rose Migiro, Anne Makinda, na Stephen Wassira.


Makala haya yanaangazia wagombea hao ambao na wengine wanaotajwa kuwa na sifa za kumrithi Komredi Kinana aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.


Wa kwanza kumuangazia ni kada wa siku nyingi, Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo.

 

Kwa wasiomfahamu Bulembo ni kuwa, kada huyo ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM. Amewahi kuwa Mbunge, Mjumbe wa NEC, Kamati Kuu na kwa sasa ni Mshauri wa Rais Mambo ya Siasa na Jamii.


Mwaka 2015, Bulembo alizunguka nchi nzima kumnadi aliyekuwa Mgombea Urais wa wakati huo, Dk John Magufuli akiwa Meneja wa Kampeni. 

Bulembo ni kada wa CCM mwenye msimamo thabiti, asiyekubali kuburuzwa na hababaishwi na jambo. 


Ilihitaji moyo na ustahamilivu kuweza kuwa meneja wa kampeni wa mwanasiasa aina ya Magufuli, lakini kwa busara zake na uwezo wake wa kisiasa, Bulembo aliweza kumnadi vyema Rais Magufuli na kufanikisha ushindi wa kishindo wa CCM.


Mbali na uzoefu wa kisiasa na utumishi ndani ya CCM, Bulembo anaonekana kuwa na sifa nyingine ambayo pengine wengine hawana. 


Sifa kimsingi, ndiyo inayomfanya awe anatajwa na makada wa CCM kuweza kumrithi Komredi Kinana.


Sifa ya ziada ya Bulembo ni kuwa mwanasiasa anayewakilisha mawazo ya rika tofauti ya wazee, kizazi kipya, umri wa kati na mtu anayeweza kuwa kiungo cha wanasiasa wazee na vijana ndani ya CCM na hata katika vyama vingine vya siasa.


 Je, ni hulka yake ya kujichanganya na watu wa rika tofauti? Ni haiba yake ya utu uzima, busara mpenda watu na aliye tayari kujitolea ikibidi hata vitu vyake binafsi?


Ni upeo wake mkubwa wa kuona mambo? Ni hoja zake za kisasa? Ni uzalendo wake? Ni upungufu walionayo wanasiasa wengine wanaotajwa kufaa katika nafasi hiyo? Ni kitu gani hasa? Wana CCM wanapaswa kuyatafutia jawabu maswali haya.


Bulembo mwenye umri wa miaka 63, bado anabeba matumaini ya zama za sasa.


Hajapitwa na wakati. Ikiwa zama za leo ni za vijana na watu wa umri wa kati. Wapigakura wengi ni vijana na hadhira ya kisiasa imebadilika sana, hivyo anahitajika makamu mwenyekiti wa CCM anayeweza kuyanadi matarajio ya vijana katika ulingo wa kisiasa na zaidi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025.


Bulembo ni muumini wa dhati kabisa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mapinduzi ya Zanzibar, ni mzalendo na ni mwanasiasa mwenye siasa za kati.


Anaonekana pia kuwa mwanafalsafa ambaye amegeuka kuwa tumaini la mabadiliko chanya ndani ya CCM. Anao uwezo wa kusaidia CCM kukabili changamoto za kisiasa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Changamoto kubwa inayomkabili Bulembo ni misimamo yake isiyoyumba kwani ni mtu ambaye habadiliki kama kinyonga katika jambo mlilokubaliana. 


Kwa matamshi mengine, Bulembo si kigeugeu, si ndumi lakuwili, bali ni mwenye msimamo thabiti kwa matendo na maneno.



Wiki ijayo tutaendelea kuwachambua makada wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara. Itaendelea

Saturday, December 21, 2024

WANAFUNZI KIDOGOZERO WAISHUKURU LION.

 







Na Omary Mngindo, Kidogozero.



WANAFUNZI wanaioishi katika mazingira hatarishi wakilelewa kwenye kituo cha Faraja, Kijiji cha Kidogozero Kata ya Vigwaza Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameishukuru Lion Club (Host) ya jijini Dar esa Salaam kwa kuwapatia misaada.


Shukrani hizo zimetolewa na wanafunzi Enjo Frank na Faraji Ramadhani baada ya kupokea vifaa vya shule na vyakula vyenye shilingi milioni 1.6, vikikabidhiwa na Rais Mahmood Rajvan, Mountazir Barwani na viongozi wenzao walipofika kijijini hapo kuwafariji watoto hao 41.


"Namshukuru Mwenyeezimungu kwani sikutegemea kupata msaada kama huu, utakaonisaidia katika masomo yangu wakati shule ikifunguliwa, mungu awasaidie na awaongezee pale mlipopunguza," alisema Enjo.


Nae Ramadhani alieleza kwamba kwa msaada huo wa begi, madaftari  pamoja na peni vimempatia chachu ya kuendelea na masomo, huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika elimu yake ya Sekondari.


Kwa upande wao wazazi Mohamed Ally aliishukuru Lion huku akiwahimiza wanafunzi kuongeza bidii katika kusoma, na kwamba zawadi hizo ziwe chachu ya kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.


Evat Mapunda alielezea shukrani zake kwa uongozi huo kwa msaada mkubwa ambao wamewapatia watoto hao, na kuwa kijana wake amepoteza wazazi wote wawili hivyo yupo mikononi mwake hivyo msaada huo umekuwa faraja kubwa kwake.


"Kijana wangu hana baba hana mama mimi ndio anayenitegemea hivyo vifaa hivi vimenigomboa, muendelee na moyo huo wa kusaidia watoto kama hawa hasanteni sana," alimalizia Evat.


Katibu wa kikundi hicho Zena Mindu mbali ya kuwashukuru Lion, pia ameuomba uongozi huo kuendelea kukisaidia kikundi hicho kinacholea watoto hao hao, huku wakiwa hawana msaada wowote.


"Nawashukuru sana mlikuja Ruvu Darajani kukabidhi Matenki ya maji pamoja na vifaa vya shule, nami mlinikabidhi msaada, leo mmekuja hukuhuku Kidogozero ambako ndio tunakosihi na kutusaidia vifaa vya shule pamoja na vyakula, tunawashukuru sana," alisema Mindu.


Akizungumza kwa niaba ya Diwani Mussa Gama, Katibu wake Amos Mwakamale alitoa shukrani kwa Lion huku akiwataka wazazi waaoishi na watoto hao kuhakikisha shule ziapofunguliwa wote wanakwenda kusoma.


Mwenyekiti wa Kijiji Said Sango alimshukuru Barwani na viongozi wote, kwa kuendeleza kazi aliyoianza kijana wake Mouhsin Barwani aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo miaka mitano iliyopita.


"Nimefurahi kuona mnaendelea kutusaidia Kata ya Vigwaza, tunaona kama bado tupo na Mohsin Barwani aliyekuwa diwani wetu miaka mitano iliyopita, hapa Kidogozero kuna tenki alilolitoa  shuleni mpaka leo linatumika, tunawashukuru sana," alisema Sango.


Akitoa neno kwa wanafunzi hao, Barwani aliwataka wanfunzi hao kukazania masomo, na kwamba taifa linawategemea katika kulitumikia miaka ijayo panapouhai, hivyo wakazanie elimu.


Tuesday, December 17, 2024

WAZIRI KIKWETE AHUDHURIA MASHINDANO YA QUR ANI KWA WENYE ULEMAVU.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Ridhiwani Kikwete  ameshiriki mashindano ya Usomaji wa Quraan Takatifu kwa Wenye Ulemavu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Riziki Lulida yaliyofanyika jijini Dodoma.


Katika mashindano hayo ambayo yalikutanisha Wenye Ulemavu kutoka makundi mbalimbali, Waziri Kikwete alitoa  salamu za serikali na kuwakumbusha kazi nzuri anayoifanya Mh. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri Ya Muungano ya Tanzania ikiwemo Mkakati wa kusimamia Haki na Ustawi wa Wenye Ualbino, Sera ya Usimamizi wa Teknolojia saidizi na mapitizo ya sera mbalimbali zinazosimamia maslahi ya Wenye Ulemavu ikiwemo sera ambazo haziendani na mazingira ya sasa. 


Aidha alisema Wizara kwa upande wao walieleza walipofikia katika kila maelekezo ya Mh. Rais, Ilani ya uchaguzi na miongozo mingi imetolewa. 

Wameendelea kumpongeza Muandaaji wa mashindano hayo Bi. Riziki Lulida, na taasisi yake na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na washiriki na kwa upekee Mh. Rais kwa kuunga mkono jambo hilo kwa kuchangia Shilingi Milioni 15. kwa vijana washiriki 30 walioshiriki usomaji wa Qur ani tukufu.



Tuesday, December 3, 2024

WATU 7 WAFARIKI AJALI YA GARI KARAGWE.

 

Na Alodia Dominick,  Karagwe.


Watu saba wamepoteza maisha huku wengine tisa wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu ya haice, kosta pamoja na Lori aina ya scania katika kizuizi cha barabarani kilichopo kijiji cha Kihanga kata ya Kihanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera na chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva.


Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea Desemba 03, 2024 saa 5:00 asubuhi  na kuhusisha lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ lenye Tela namba T472 EAQ likiwa linatokea Kayanga wilaya ya Karagwe kwenda Kyaka lilipofika Kihanga katika kizuizi cha barabarani yalikuwepo magari mawili.


Ameongeza kuwa, moja lilikuwa kosta namba T367 ECP pamoja na toyota  haice yenye namba za usajili T973 DGD yakiwa yamesimama yanaendelea kukaguliwa na maafisa uhamiaji mita kama kumi kutoka kwenye kizuizi ndipo Scania iliyagonga kutokea nyuma na kusababisha ajali hiyo.


"Gari hilo limetokea Mbeya likiwa limebeba mchele kuupeleka Mtukula na baada ya kushusha mchele lilipata mzigo mwingine Karagwe wa kurudi nao Mbeya ambao ni parachichi, huyu dereva ni mgeni katika eneo hilo kwa uzembe na kutokuchukua tahadhari alikuja katika mwendo ambao ni mkali akaigonga toyota haice pamoja na kosta" amesema Chatanda.


Aidha, katika ajali hiyo vimetokea vifo saba wanawake wanne, mwanaume mmoja na watoto wawili huku majeruhi wakiwa tisa wanaume wanne na wanawake watano.


Amesema uzembe wa dereva umesababisha ajali kwani inaonekana alikuja katika mwende mkali lakini ajali haikusababishwa na kufeli breki kwani huko nyuma alikotoka alipita katika mlima wa Kishoju na kwenye kona hivyo ingekuwa breki ule mteremko asingeumaliza.


"Ni wazi kwamba tahadhari za alama barabarani hakuzichukua kwani barabara hiyo inazo alama za barabara na hata kabla ya kizuizi kuna alama pia" amesema Chatanda.


Mmoja wa mashuhuda Adamu Alon mtengeneza majokofu kutoka Kayanga amesema kuwa, ameitwa na mteja Kyaka wilaya ya Misenyi na kupanda Kosta ambayo imehusika kwenye ajali walivyofika Mgakorongo walikuta hilo lori likiwa limesimama dereva anaongea na askari wa usalama barabarani wakapita.


Amesema, wakati gari hilo limefika Kihanga katika kizuizi cha barabarani ndipo Scania hiyo imegonga gari lao likiwa linakaguliwa na maafisa uhamiaji yeye alikuwa amekaa kiti cha mbele na dereva huku akitakiwa kuonyesha kitambulisho na afisa uhamiaji ndipo amesikia kishindo kikubwa na gari alilokuwemo likahama na kwenda mbele.


Ameeleza kuwa, yeye na afisa uhamiaji wamedondoka chini baadaye alipopata fahamu alikuta scania waliyoipita Mgakorongo ndiyo iliwagonga.


Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Karagwe iliyopo Nyakanongo pamoja na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.







Friday, November 29, 2024

VIONGOZI WATEULE WA VITONGOJI NA VIJIJI WAAPA BAGAMOYO.

 







Viongozi wa Vitongoji na Vijiji pamoja na Wajumbe wao walioshinda katika uchaguzi uliofanyika tarehe 27 Novemba 2024. Leo tarehe 29 Novemba 2024 wameapishwa rasmi kushika nyadhifa zao katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. 

Akifungua kikao cha kuwaapisha Viongozi hao, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bagamoyo Bw Shauri Selenda aliwakaribisha na kuwashukuru kwa kuchaguliwa  na kuaminiwa na wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 27 mwezi huu .

"Nichukue nafasi kwa niaba yangu mimi mwenyewe na kwa niaba ya Halmashsuri kwa kuteuliwa kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa,  "Mchakato haukuwa rahisi lakini mmefanikiwa niwapongeze". Alisema Bw Shauri Selenda.

 Katika Uchaguzi huo ulifanyika tarehe 27 Novembe, 2024 vyama mbalimbali vya kisiasa vilishiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwenye vitongoji vyote   167 vya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. 

     Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Shaibu Ndemanga aliwaasa wenyeviti  hao kushirikiana ili kuwahudumia wananchi kama walivyoapa katika viapo vyao.

CCM YASHINDA KWA ASILIMIA 98.82 LINDI

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.


Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Lindi Mkoani Humo bwana Juma Mnwele Leo tarehe 29 November 2024 ametangaza matokeo ya Jumla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa vijiji na vitongoji Katika Manispaa hiyo uliofanyika November 27 mwaka huu 2024


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake msimamizi huyo wa uchaguzi Manispaa ya Lindi amesema Kati ya nafasi za uongozi 1954 zilizoshindaniwa na Vyama vya siasa chama cha mapinduzi kimeshinda nafasi 1931 sawa na asilimia 98.82, chama cha ACT wazalendo wameshinda nafasi 21 sawa na asilimia 1.07


Alitaja chama chama kingine ni chadema ambacho kilishinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.1 kikifuatiwa na chama cha wananchi cuf ambacho kimeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.05 huku chama cha CHAUMA, NCCR MAGEUZI na TLP vikikosa ushindi kabisa