Watu wawili wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko ambao bado haujafahamika ni wa kitu gani.
Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salim Morcase, amesema tukio hilo limetokea leo tarehe 31 Agosti 2025 Mtaa wa kichemchem kata ya Nianjema wilayani Bagamoyo majira ya saa moja na dakika ishirini asubui.
Amesema chanzo cha vifo hivyo ni mlipuko wa chuma ambacho Doto Mrisho (Marehemu) alikuwa anakikata kwenye karakana yake ya kuchomelea mageti.
Waliofariki katika tukio hilo ni Doto Mrisho mwenye umri wa miaka 24 fundi wa kuchomelea mageti mkazi wa kichemchem kata ya Nianjema na Saidi Ramadhani mwenye umri wa miaka 53 mkazi wa Sanzale Bagamoyo, na aliyejeruhuwa katika tukio hilo ni Hassan Omari, mkazi wa Sanzale Bagamoyo.
Kamanda Morcase amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanyika na jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kubaini chanzo cha mlipuko huo na ni wa kitu gani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuokota vyuma ambavyo hawavijui na pia waache tabia ya kukata vyuma ambavyo ni aina ya mitungi ya gesi, au chochote chenye duara au mfano wa kibuyu kidogo kilichozibwa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.