Friday, December 15, 2023

RMO KAGERA ATENGULIWA KWA KUZUILIWA MWILI WA MTOTO MCHANGA KWA MADAI YA DENI LA MATIBABU HOSPITALINI.

 


Na Alodia Babara

Bukoba.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amemwagiza katibu mkuu wa TAMISEMI nchini kutengua nafasi ya mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Issesanda Kaniki baada ya hospitali ya rufaa ya Bukoba ya mkoa huo kuzuia mwili wa mtoto mchanga kwa muda wa siku mbili kutoruhusiwa kwenda kuzikwa wakati wakijua watoto wanatibiwa bure.


Maagizo mengine ameyatoa kwa viongozi wa serikali, siasa na watumishi mbalimbali nchini.


Waziri Mchengerwa ametoa maagizo hayo  Desemba 15, mwaka huu wa 2023, wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani kinachokarabatiwa ambapo pia alishuhudia utiaji wa saini ya mikataba ya usanifu miradi ya uboreshaji wa miundomninu ya miji Tanzania (TACTIC) kwa miji 15 ya kundi la pili.


Ameagiza katibu mkuu TAMISEMI kwa kushirikiana na sekta ya afya kufanyika mapitio ya menejimenti nzima ya hospitali hiyo na kutoa maamuzi kwani alipata malalamiko kuwa wapo baadhi ya watumishi wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa.


Amesema,  muda wa kubembelezana haupo tena kwa nyakati hizi watu wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea sasa hatuwezi kuendelea na watumishi wa namna hiyo kwa sababu wananchi wana imani na serikali yao.


Wakati huo huo waziri Mchengerwa alisema mtu yoyote au kiongozi yoyote awe wa kisiasa au mtendaji yeyote wa serikali atakaye jaribu kufanya ubadhilifu au kukwamisha miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika manispaa ya Bukoba ikiwemo stend kuu, soko kuu, barabara ya kilomita saba na kingo za mto Kanoni na kufunga taa za barabani
hatofumbiwa macho atachukulia hatua kali za kisheria.


"Tunataka  tubadilishe muonekano wa Kagera mhe. Rais alizitafuta fedha hizi maeneo mbalimbali anataka kuibadilisha Kagera hivyo, kiongozi yoyote awe wa kisiasa au serikali atakayejaribu kuingiza mkono bila kujali nafasi yake nitashugulika naye ikiwemo kumfukuza kazi, hatutaki ubabaishaji katika miradi hii"amesema Mchengerwa.


Aidha amesema, kama kuna viongozi wa siasa ndani ya manispaa ya Bukoba au mkoa wa Kagera wanaokwamisha miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ni kiu ya wanakagera kwa muda mrefu atasimamisha baraza la madiwani mpaka miradi hiyo ikamilike.


"Maagizo yangu ujenzi wa soko uzingatie wale wafanyabiashara  wa zamani waliondolewa kinyume na taratibu wapate vibanda ndipo wapya wapewe mabanda na wale waliko nje ya soko wote wapate nafasi hii pia tukikamilisha hatutaki kuona wafanyabiasha wakiendesha shughuli zao nje ya soko hili ambalo Dk.Samia anakwenda kulijenga katika maeneo haya kiongozi yoyote atakaye kaidi maagizo, ujeuri na kiburi aliyeko kwenye mamlaka yangu nitamfukuza kazi na walioko kwenye mamlaka za juu nitawafikisha kwa Rais awafukuze kazi”alisema.


Pia waziri aliwaagiza  wakurugenzi wote nchini kuendana na kasi ya Ras Samia ambapo kila mkurugenzi anatakiwa kuanzisha vyanzo viwili vya kuingiza mapato atakayeshindwa kufanya hivyo atahovumiliwa.


Mratibu wa miradi ya ushirikiano na benki ya dunia TACTIC  mhandisi Humphrey  Kanyenye alisema miradi hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa miezi nane ikiwezekana mwezi Machi mwakani ujenzi uanze mara moja.


Ujenzi wa kituo cha mabasi Bukoba na soko kuu kimekuwa kitendawili cha muda mrefu baada ya kukwama kujengwa takribani miaka 15 iliyopita baada ya kutokea mgongano wa masrahi ya kisiasa.


Miradi hii ya uboreshaji wa miundombinu ya miji Tanzania TACTIC  kwa miji 15 ya kundi la pili (Tier) ambapo Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji itakayonufaika na miradi hiyo zilitengwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi huo kati ya sh moja trilioni ya miradi yote.


Thursday, December 14, 2023

POLISI KAGERA WAKAMATA SILAHA 11. NA RISASI 115.

 

Na Alodia Babara

Bukoba.

Jeshi la polisi mkoani Kagera limekamata silaha 11 zikiwemo bunduki 2 aina ya AK 47 zikiwa na magazine tatu, risasi 115, bastola aina ya glock 17 na bunduki aina ya gobore.


Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. Blasius Chatanda, akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 14, 2023, amesema kuwa, jeshi hilo  linaendelea kufanya oparasheni mbalimbali na kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi katika mkoa huo ambapo katika oparasheni iliyofanyika kuanzia Septemba, 2023 hadi sasa silaha 11 zilikamatwa.


“Katika kudhibiti matukio ya utekaji  nyara hasa kwa wafugaji katika mkoa wetu wa Kagera tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 14 wa utekaji, tumekamata silaha mbili aina ya AK 47 zikiwa na magazine tatu pamoja na risasi 115 na bastola aina ya grock 17” amesema Chatanda.


Aidha amesema katika kudhibiti matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ujagili jumla ya bunduki nane aina ya gobore zimekamatwa na kati ya hizo nne zilisalimishwa na watuhumiwa watano kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.


Amesema jeshi hilo limeendelea kudhibiti wimbi la wizi wa watoto na kufanikiwa kukamata watu wanne ambao walihusika na wizi wa watoto na watoto wanne walikamatwa wakiwa hai.


Ameongeza kuwa, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kwa hatua mbalimbali ili kujibu tuhuma zinazowakabili.


Wakati huo huo, amesems pikipiki za wizi ambazo hazikuwa na nyaraka zozote zipatazo 157 zimekamatwa mkoani Kagera pamoja na nchi jirani ya Burundi baada ya kufanyika oparashen.


Amesema pikipiki 157 zilizokamatwa kati ya hizo 92 zilikamatwa nchini Burundi zikiwa na usajili wa namba za Tanzania zikiwa zinatumika nchini humo, huku pikipiki 65 zikikamatwa mkoani Kagera.


“Kwa sasa pikipiki hizo bado ziko Burundi baada ya kukamilisha taratibu zote za kuzirejesha hapa nchini tutawatangazia wananchi ili waje kuzitambua, na pikipiki zilizopo mkoani hapa watu waje kuzitambua” amesema Chatanda.


Mmoja wa waendesha pikipiki maarufu boda boda manispaa ya Bukoba, Enock Novath, ameliomba jeshi la polisi kuimarisha ulinzi ili kudhibiti matukio ya wizi wa pikipiki ambayo yameshamiri katika mkoa wa Kagera.


Joanes Festo mkazi wa manispaa ya Bukoba amedai kuwa mwaka huu ameibiwa pikipiki mbili na kutoa taarifa kituo cha polisi na kuwa hakuna pikipiki yake ambayo imeishapatikana.


Ameliomba jeshi la polisi kuwa zinapotolewa taarifa za wizi wa pikipiki msako uanze mara moja na siyo kusubili oparasheni kwani kufanya hivyo zitakamatwa pikipiki kabla hazijasafirishwa kwenda nje ya mkoa






Tuesday, December 5, 2023

WAHITIMU ADEM WAPEWA SOMO NA PROF. MKENDA.

 

Wahitimu katika chuo cha Wakala wa Maendeleo ya uongozi wa elimu
­(ADEM) wametakiwa kwenda kusimamia vyema taaluma ya uongozi na utawala katika maeneo yao ili kutimiza malengo ya serikali katika
maboresho ya elimu hapa nchini.

Katika Mahafali ya 31 ya waahitimu hao yaliyofanyika tarehe 01 Desemba
2023, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Prof. Adolf Mkenda, amesema katika kipindi hiki cha mageuzi ya elimu,
serikali inawategemea sana walimu hasa waliosomea uongozi na utawala
katika kuhakikisha yale yote yanayotakiwa kuboreshwa yanasimamiwa ipasavyo.

Amesema tayari serikali inaendelea na mchakato wa maboresho ya elimu
nchini kwa kuangazia mambo saba muhimu ambayo ni sera ya elimu,
mabadiliko ya sheria ya elimu ya mwaka 1978 ambapo sasa elimu ya
lazima ni miaka 10 kwa kila Mtanzania.

Prof. Mkenda ameongeza kwa kusema kuwa, katika maboresho hayo , kuna
marekebisho ya mitaala, kuwa na walimu, wakufunzi na wahadhiri kwa
mgawanyo uliokuwa sawa, Ubora wa walimu, wakufunzi na wahadhiri,
vitendea kazi pamoja na miundombinu.

Alisisitiza kuwa ili kuweza kupata matokeo mazuri ya utekelezaji wa
maboresho hayo viongozi wa elimu wa ngazi mbalimbali wana mchango
mkubwa katika kufikia malengo hayo.

Alisema walimu ni walezi kama walivyo wazazi, mwalimu anapokuwa na mtoto shuleni anapaswa kujiona yeye ni mzazi ambae atamuangalia mtoto sio tu kwa kumfundisha bali pia ni kwa kumpa ulinzi anaostahiki ili
asidhurike kimaadili na na kimwili kwakuwa mzazi anatarajia pia
usimamizi mahiri wa mwalimu.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Siston Masanja, amesema
malengo ya ADEM ni kutekeleza azma ya serikali ya kuboresha Uongozi,
Usimamizi, na Uendeshaji wa Elimu nchini katika shule za Msingi,
Sekondari Vyuo vya ualimu na kwa maafisa elimu wote, ambapo mafunzo
yanayotolewa yanawawezesha kuimarisha utendaji katika ngazi zote za elimu.

Dkt. Masanja ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa
kuendelea na maboresho ya elimu hapa nchini kwa kuhuisha sera ya elimu
na mafunzo na kusema kuwa ADEM ipo tayari kutoa mafunzo ya Uongozi,
Usimamizi na uendeshaji wa Elimu pamoja na kufanya tafiti zitakazosaidia kutoa majibu mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika elimu.

Awali wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi, wahitimu hao walisema wamejifunza namna Uongozi bora unavyoweza kuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya Elimu na kuleta tija na matokeo chanya katika ukuaji wa Taifa kwa ujumla.

Waliongeza kwa kusema kuwa wamejifunza jinsi ya kutoa elimu kwa watu wazima pamoja na kutambua mazingira rafiki kwao katika kujifunza. Hali hiyo  itasaidia uendelezaji wa vituo vya Elimu ya watu wazima katika vituo
vyetu vya kazi.

Mahafali hayo yalikuwa ya whitimu wa stashahada ya uongozi na usimamizi wa elimu, (DEMA), Stashahada ya uthibiti ubora wa shule (DSQA) na Astashahada ya uongozi, usimamizi na utawala katika elimu (CELMA)