Saturday, December 21, 2024

WANAFUNZI KIDOGOZERO WAISHUKURU LION.

 







Na Omary Mngindo, Kidogozero.



WANAFUNZI wanaioishi katika mazingira hatarishi wakilelewa kwenye kituo cha Faraja, Kijiji cha Kidogozero Kata ya Vigwaza Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameishukuru Lion Club (Host) ya jijini Dar esa Salaam kwa kuwapatia misaada.


Shukrani hizo zimetolewa na wanafunzi Enjo Frank na Faraji Ramadhani baada ya kupokea vifaa vya shule na vyakula vyenye shilingi milioni 1.6, vikikabidhiwa na Rais Mahmood Rajvan, Mountazir Barwani na viongozi wenzao walipofika kijijini hapo kuwafariji watoto hao 41.


"Namshukuru Mwenyeezimungu kwani sikutegemea kupata msaada kama huu, utakaonisaidia katika masomo yangu wakati shule ikifunguliwa, mungu awasaidie na awaongezee pale mlipopunguza," alisema Enjo.


Nae Ramadhani alieleza kwamba kwa msaada huo wa begi, madaftari  pamoja na peni vimempatia chachu ya kuendelea na masomo, huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika elimu yake ya Sekondari.


Kwa upande wao wazazi Mohamed Ally aliishukuru Lion huku akiwahimiza wanafunzi kuongeza bidii katika kusoma, na kwamba zawadi hizo ziwe chachu ya kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.


Evat Mapunda alielezea shukrani zake kwa uongozi huo kwa msaada mkubwa ambao wamewapatia watoto hao, na kuwa kijana wake amepoteza wazazi wote wawili hivyo yupo mikononi mwake hivyo msaada huo umekuwa faraja kubwa kwake.


"Kijana wangu hana baba hana mama mimi ndio anayenitegemea hivyo vifaa hivi vimenigomboa, muendelee na moyo huo wa kusaidia watoto kama hawa hasanteni sana," alimalizia Evat.


Katibu wa kikundi hicho Zena Mindu mbali ya kuwashukuru Lion, pia ameuomba uongozi huo kuendelea kukisaidia kikundi hicho kinacholea watoto hao hao, huku wakiwa hawana msaada wowote.


"Nawashukuru sana mlikuja Ruvu Darajani kukabidhi Matenki ya maji pamoja na vifaa vya shule, nami mlinikabidhi msaada, leo mmekuja hukuhuku Kidogozero ambako ndio tunakosihi na kutusaidia vifaa vya shule pamoja na vyakula, tunawashukuru sana," alisema Mindu.


Akizungumza kwa niaba ya Diwani Mussa Gama, Katibu wake Amos Mwakamale alitoa shukrani kwa Lion huku akiwataka wazazi waaoishi na watoto hao kuhakikisha shule ziapofunguliwa wote wanakwenda kusoma.


Mwenyekiti wa Kijiji Said Sango alimshukuru Barwani na viongozi wote, kwa kuendeleza kazi aliyoianza kijana wake Mouhsin Barwani aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo miaka mitano iliyopita.


"Nimefurahi kuona mnaendelea kutusaidia Kata ya Vigwaza, tunaona kama bado tupo na Mohsin Barwani aliyekuwa diwani wetu miaka mitano iliyopita, hapa Kidogozero kuna tenki alilolitoa  shuleni mpaka leo linatumika, tunawashukuru sana," alisema Sango.


Akitoa neno kwa wanafunzi hao, Barwani aliwataka wanfunzi hao kukazania masomo, na kwamba taifa linawategemea katika kulitumikia miaka ijayo panapouhai, hivyo wakazanie elimu.


Tuesday, December 17, 2024

WAZIRI KIKWETE AHUDHURIA MASHINDANO YA QUR ANI KWA WENYE ULEMAVU.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Ridhiwani Kikwete  ameshiriki mashindano ya Usomaji wa Quraan Takatifu kwa Wenye Ulemavu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Riziki Lulida yaliyofanyika jijini Dodoma.


Katika mashindano hayo ambayo yalikutanisha Wenye Ulemavu kutoka makundi mbalimbali, Waziri Kikwete alitoa  salamu za serikali na kuwakumbusha kazi nzuri anayoifanya Mh. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri Ya Muungano ya Tanzania ikiwemo Mkakati wa kusimamia Haki na Ustawi wa Wenye Ualbino, Sera ya Usimamizi wa Teknolojia saidizi na mapitizo ya sera mbalimbali zinazosimamia maslahi ya Wenye Ulemavu ikiwemo sera ambazo haziendani na mazingira ya sasa. 


Aidha alisema Wizara kwa upande wao walieleza walipofikia katika kila maelekezo ya Mh. Rais, Ilani ya uchaguzi na miongozo mingi imetolewa. 

Wameendelea kumpongeza Muandaaji wa mashindano hayo Bi. Riziki Lulida, na taasisi yake na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na washiriki na kwa upekee Mh. Rais kwa kuunga mkono jambo hilo kwa kuchangia Shilingi Milioni 15. kwa vijana washiriki 30 walioshiriki usomaji wa Qur ani tukufu.



Tuesday, December 3, 2024

WATU 7 WAFARIKI AJALI YA GARI KARAGWE.

 

Na Alodia Dominick,  Karagwe.


Watu saba wamepoteza maisha huku wengine tisa wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu ya haice, kosta pamoja na Lori aina ya scania katika kizuizi cha barabarani kilichopo kijiji cha Kihanga kata ya Kihanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera na chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva.


Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea Desemba 03, 2024 saa 5:00 asubuhi  na kuhusisha lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ lenye Tela namba T472 EAQ likiwa linatokea Kayanga wilaya ya Karagwe kwenda Kyaka lilipofika Kihanga katika kizuizi cha barabarani yalikuwepo magari mawili.


Ameongeza kuwa, moja lilikuwa kosta namba T367 ECP pamoja na toyota  haice yenye namba za usajili T973 DGD yakiwa yamesimama yanaendelea kukaguliwa na maafisa uhamiaji mita kama kumi kutoka kwenye kizuizi ndipo Scania iliyagonga kutokea nyuma na kusababisha ajali hiyo.


"Gari hilo limetokea Mbeya likiwa limebeba mchele kuupeleka Mtukula na baada ya kushusha mchele lilipata mzigo mwingine Karagwe wa kurudi nao Mbeya ambao ni parachichi, huyu dereva ni mgeni katika eneo hilo kwa uzembe na kutokuchukua tahadhari alikuja katika mwendo ambao ni mkali akaigonga toyota haice pamoja na kosta" amesema Chatanda.


Aidha, katika ajali hiyo vimetokea vifo saba wanawake wanne, mwanaume mmoja na watoto wawili huku majeruhi wakiwa tisa wanaume wanne na wanawake watano.


Amesema uzembe wa dereva umesababisha ajali kwani inaonekana alikuja katika mwende mkali lakini ajali haikusababishwa na kufeli breki kwani huko nyuma alikotoka alipita katika mlima wa Kishoju na kwenye kona hivyo ingekuwa breki ule mteremko asingeumaliza.


"Ni wazi kwamba tahadhari za alama barabarani hakuzichukua kwani barabara hiyo inazo alama za barabara na hata kabla ya kizuizi kuna alama pia" amesema Chatanda.


Mmoja wa mashuhuda Adamu Alon mtengeneza majokofu kutoka Kayanga amesema kuwa, ameitwa na mteja Kyaka wilaya ya Misenyi na kupanda Kosta ambayo imehusika kwenye ajali walivyofika Mgakorongo walikuta hilo lori likiwa limesimama dereva anaongea na askari wa usalama barabarani wakapita.


Amesema, wakati gari hilo limefika Kihanga katika kizuizi cha barabarani ndipo Scania hiyo imegonga gari lao likiwa linakaguliwa na maafisa uhamiaji yeye alikuwa amekaa kiti cha mbele na dereva huku akitakiwa kuonyesha kitambulisho na afisa uhamiaji ndipo amesikia kishindo kikubwa na gari alilokuwemo likahama na kwenda mbele.


Ameeleza kuwa, yeye na afisa uhamiaji wamedondoka chini baadaye alipopata fahamu alikuta scania waliyoipita Mgakorongo ndiyo iliwagonga.


Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Karagwe iliyopo Nyakanongo pamoja na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.