Mwandishi wetu, Malinyi
Mkuu wa wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro, Mathayo Masele,
ametoa rai kwa walimu wa umma wenye uwezo wa kufundisha somo la elimu ya dini
ya Kiislam (EDK) kufanya hivyo mara moja huku akisisitiza kuwa hakuna haja ya
kuona haya, woga au hofu yeyote.
Akizungumza katika semina ya walimu wa somo hilo
kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Afisa Tarafa ya Malinyi Ms Rehema Rajabu amesema
haoni sababu ya walimu kuwa na hofu ya kufundisha elimu ya dini huku wakijua
wazi kuwa kufanya hivyo sio kosa kisheria
“Nitashangaa sana kama bado wapo walimu wenye
uwezo wa kufundisha somo hili lakini wanajificha kwa kuogopa watu, serikali
inapenda kuona jamii inalelewa katika maadili mema na somo hili linajikita
kwenye maadili, kwa nini sasa mwalimu uogope kutoa elimu yako,” alihoji Ms
Rehema
Aidha, Rehema amewahamasisha wananchi wa Wilaya
ya Malinyi kufanyia pupa mambo ya heri ili kukabiliana na tatizo la mmomonyoko wa maadili
ambalo linaota mizizi kila kukicha.
“Hapa wilayani bado muamko wa dini uko chini,
wengi wamejikita kwenye utamaduni wa asili, nadhani muda umefika wa kubadilika,
tuanze kuwapeleka vijana wetu madrasa kujifunza wajibu wao na sababu za kuletwa
duniani, naamini nyoyo za watoto wetu zitajengeka kimaadili kwani watakuwa ni
watoto wenye hofu na Mungu,” aliongeza.
Vilevile, ameitaka jamii ya Malinyi kuwa na moyo
wa kutoa mali zao kwa ajili ya kuendeleza dini, na kwa kuanzia ameshauri
kutatua changamoto ya vitabu vya EDK ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi
“Walimu wamesema hapa tunalo tatizo la vitabu vya EDK, kwa kuanzia vinatakiwa vitabu vyenye thamani ya Milioni tatu, jambo hili lipo ndani ya uwezo wetu, tutowe mali zetu ili vijana wetu wapate elimu hii muhimu,” alisema.
Ms Rehema
amesema katika mambo yanayomuhuzunisha licha ya ukweli kuwa jamii ya Malinyi ni tajiri lakini wamekuwa na moyo
mgumu wa kujitoa kwenye mambo ya dini.
Alisema kitendo hicho kimepelekea muamko wa dini
kuwa chini na hivyo vijana wengi wa eneo hilo wamejikuta wakiitanguliza Zaidi dunia
kuliko akhera yao.
Katika hatua nyingine walimu wa shule za msingi
na sekondari wilayani humo wameungana na Kaimu Mkuu wa Wialaya huyo, Ms Rehema kwa
kusema kuwa bado kuna changamoto ya somo la dini wilyani humo.
Mmoja wa walimu hao, Bw. Fadhiri Chuma, Mwalimu
wa shule ya sekondari Mtimbira alieleza kuwa kunahitajika vitabu vya kutosha
ili kufundisha somo hilo, kwani walimu wapo wa kutosha shida ni vitendea kazi.
Alisema licha ya uwepo wa vipindi vya dini,
lakini wamejikuta wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa kukosa miongozo ya
somo la EDK hali inayopelekea somo hilo kuwa geni kwa watoto wa Malinyi
Pia Mwalimu Shaabani Mandanda kutoka shule ya
msingi Nawigo iliyopo Wilaya ya Malinyi amewaomba waislam na jamii kwa ujumla kujitoa
kwa hali na mali ili vitabu vya elimu ya dini vipatikane na vijana waanze kupatiwa
mafunzo yatakayo wasaidia katika maisha yao.
Hali ya somo la EDK Malinyi…
Aidha, akizungumzia hali ya somo la EDK wilayani Malinyi,
mmoja wa wazazi wa eneo hilo, Matano Matano alisema ni mbaya sana kwani Wilaya
nzima haina watoto wanaosoma somo hilo
“Mtoto akichukua somo hilo kwake inakuwa ni
mtihani mkubwa, hakuna Mwalimu wa kufundisha, mwanangu amejitahidi kulichukua kwa
sababu msingi wake umejengwa kwenye dini akiwa Zanzibar lakini walimu wa
kufundisha somo hilo hapa katika wilaya yetu hakuna.
Nimejaribu kuwafuata walimu kadhaa ambao najua
wanafahamu kidogo kuhusu EDK kwa kuahidi kuwalipa kwa mwezi 100,000, ajabu ni
kwamba hakuna hata mmoja aliyejitokeza.
Kila mmoja anatoa udhuru, yaani 100,000 kwa
mwezi, alafu unafundisha kwa wiki mara moja, watu wanaona shida, vipi mtoto
anaweza kupenda somo hilo,” alisema kwa uchungu bwana Matano
Kwa upande wake Amiri wa Islamic
Education Panel Kanda ya Mashariki, Abuuswaburi akielezea maendeleo ya somo hilo
amesema maendeleo ni ya kuridhisha ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Amesema kwa mujibu wa Matokeo ya
Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Dini ya Kiislamu nchini (EDK) kwa mwaka 2022 kiwango
cha ufaulu kimepanda kutoka wastani wa asilimia 49.78 kwa mwaka 2021 hadi
kufikia wastani wa 66.77.
Aidha idadi ya watahiniwa nayo
imeongezeka kutoka watahiniwa 126,088 mwaka 2021 hadi kufikia watahiniwa
142,522 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 16,434 sawa na asilimia 13.3
Aidha Wanafunzi 3,567 wamefanya vizuri
katika mitihani yao kwa kupata Daraja A huku waliopata Daraja B wakiwa 22,587
na C wakiwa 69,012.
Akifafanua ufaulu huo alisema kwa
ujumla waliofaulu kwa kupata Daraja A hadi C ni watoto 95,166 sawa na asilimia
66.77, huku watoto 47,356 sawa na asilimia 33.23 wakipata Daraja D na E. Daraja
D watoto 45,781 na E watoto 1,575.
Naye Mratibu wa Islamic Education
Panel Taifa (IEP), Suleiman Daudi, amewakumbusha waislam wa Malinyi na Taifa
kwa ujumla kutoa mali zao kwa ajili ya kutengeneza nyoyo za kizazi cha kesho
kimaadili.
No comments:
Post a Comment