Wednesday, July 6, 2022

SERIKALI KUWAKOPESHA WAVUVI ZAIDI YA BOTI 300.

 No description available.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Mashauri Ndaki,akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) mjini Bagamoyo, Julai 05, 2022.

.......................................................

Na Athumani Shomari

Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuboresha sekta ya uvuvi hapa nchini ili kuwawezesha wavuvi kuvua samaki katika mazingira ya kisasa.

Akizungumza katika uzinduzi wa jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) mjini Bagamoyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Mashauri Ndaki, alisema Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa kipaumbele kwenye sekta ya uvuvi hali iliyopelekea bajeti ya wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka huu wa 2022/2023 kuongezeka kutoka Bilioni 168  ya mwaka uliopita hadi kufikia Bilioni 268, ili kuondoa changamoto zinazowakabili wavuvi.

Alisema katika bajeti hiyo serikali imepanga kununua boti za uvuvi za kisasa ili kuwawezesha wavuvi kuvua kisasa na kwenda kwenye maji yenye kina kirefu hali itakayowasaidia pia kuzingatia kanuni za uvuvi zinazowakataza kuvua katika maji machache yanye kina chini ya mita 50.

Alisema kuwa, serikali itanunua jumla ya Boti 320, ambazo zitapelekwa kwa wavuvi wa ukanda wa pwani kwa kuwakopesha ili waondokane na zana duni wanazotumia sasa, na badala yake wawe na zana za kisasa zitakazowawezesha kwenda kwenye maji yenye kina cha mita 50 au zaidi.

Aliongeza kwa kusema kuwa, lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kuongeza uzalishaji wa mazao yatokanayo na uvui ili kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja, kuongeza mapato yatokanayo na uvuvi kwa serikali na kupata lishe bora ya samaki kwa wanachi wote.

Alesema rasilimali za uvuvi kwa ukanda wa Pwani ni nyingi sana lakini wavuvi wanashindwa kunufaika na rasilimali hizo kutokana na zana duni wanazotumia kuvulia hali inayopelekea kukiuka kanuni za uvuvi zinazowakataza wasivue kwenye maji yenye kina kifupi chini ya mita 50 na hivyo kupelekea vipato vyao pia kuwa duni.

Alifafanua kuwa, uvuvi duni unasababishwa na Zana duni, Mtaji mdogo na ujuzi usiokidhi katika kuvua ambapo yote hayo serikali ya awamu ya sita imeyaona na kuja na bajeti itakayopelekea kutatua changamoto mbalimbali za wavuvi.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 50 kwaajili ya ujenzi wa Bandari ya uvuvi Kilwa Masoko ili kuwezesha meli kubwa za uvuvi kutia nanga katika eneo hilo.

Alisema tayari serikali imetoa leseni kwa meli kubwa za uvuvi ili zivue katika Bahari ya hindi katika eneo la Tanzania lakini haziwezi kutia nanga kwenye maeneo yetu kwakuwa hatuna Bandari maalum ya uvuvi inayowezesha meli kubwa kutia nanga ambapo kwa sasa tutaweza kuziona meli hizo katika ukanda wetu wa pwani.

Aliendelea kusema kuwa, Bandari hiyo itakapokamilika licha ya kuingia meli kubwa za uvuvi katika Bandari hiyo, pia kutakuwa na mambo yanayoambatana na hiyo bandari ikiwemo karakana ya itakayotoa matengenezo kwa meli hizo, Vituo vya mafuta kwaajili kujaza mafuta katika meli na chumba maalum cha barafu ambacho kitasaidia kuhifadhi samaki watakaovuliwa kabla ya kusafirishwa sehemu mbalimbali.

 

Akizungumzia Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) Waziri Ndaki alisema serikali haitasita kuvifuta vikundi vya BMUs vitakabainika kupokea rushwa kwa wavuvi haramu ili kuwafichia siri.

Alisema, lengo la serikali kuunda vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi ni kuimarisha ulinzi ili kulinda maeneo ya bahari dhidi ya uvuvi haramu unaokiuka kanuni za uvuvi na kwamba ikitokea BMUs zinashirikiana na wavuvi haramu hakuna sababu ya kuwepo BMUs hizo na wataweza kuzifuta na kuchagua timu ya watu wengine.

Ujenzi wa ofisi za  Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) umetekelezwa na Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi Mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambapo majengo hayo yamejengwa Halmashauri za Bagamoyo, Chalinze, Pangani, Mkinga na Lindi Vijijini.

No description available.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallaah, akitoa utambulisho wa viongozi wakati wa shughuli ya uzinduzi wa jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) iliyofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo.

No description available.

Mbunge wa jimbo la Chalinze ambae pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akizungmza wakati wa kumkaribisha Waziri wa Mifugo na uvuvi Mashimba Mashauri Ndaki, katika shughuli ya uzinduzi wa jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) iliyofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo.

No description available. 

Waziri wa Mifugo na uvuvi Mashimba Mashauri Ndaki, (kushoto) akifungua kitambaa ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) uliofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo.

No description available.

Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Editor Komba (kulia) akisaini hati ya makadhiano ya jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) yaliyofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo, pamoja nae ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda (kushoto).

 No description available. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda (kushoto). akisaini hati ya makabidhiano ya jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) yaliyofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo, pamoja nae ni Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Editor Komba (kulia)

No description available. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda (kushoto), na Mwanasheria wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Editor Komba (kulia) wakibadilishana hati ya makabidhiano ya jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) yaliyofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo.

No description available.

Wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi wa jengo la Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) uliofanyika Julai 05,2022 mjini Bagamoyo.



No comments:

Post a Comment